Hivi karibuni, puto moja la China ambalo lilifika Marekani kwa bahati mbaya lilisababisha wasiwasi mkubwa kuhusu “tishio la China” nchini Marekani.Mwishowe, jeshi la Marekani liliangusha puto hilo kwa kutumia ndege zake za kivita aina ya F22, na kutafuta mabaki ya puto hilo ili kuthibitisha kuwa China imetumia puto hilo kuichunguza Marekani.
Lakini ukweli ni kwamba, puto hilo la China ni kwa ajili ya utafiti wa hali ya hewa, na Marekani ndio nchi inayochunguza zaidi nchi nyingine duniani.
Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na mahitaji ya utafiti wa kisayansi, nchi mbalimbali duniani zimerusha maputo ya urefu wa juu mara nyingi zaidi. Takwimu zinaonyesha kuwa katika miongo michache iliyopita, Ufaransa imerusha jumla ya maputo 3,000 ya urefu wa juu, Marekani imerusha zaidi ya 2,000, na Japan ni zaidi ya 800.
Wakati huohuo, matukio ya maputo hayo kuvuka mpaka na kuingia nchi nyingine yanazidi kuwa ya kawaida. Hapo awali, “Google Balloon” iliyorushwa na Google nchini Marekani iliruka na kuwa angani kwa mamia ya siku, ikipita nchi nyingi duniani.
Matukio kama hayo hutatuliwa kwa njia ya mazungumzo. Hata hivyo, mara hii Marekani ilipuuza utaratibu wa kimataifa na kupaza sauti kuwa China ilivamia anga yake na kutaka kuchunguza siri zake, hata mwisho ilitatua suala hilo kwa kutumia njia ya kijeshi.
Kutoka kampuni za Huawei hadi Dajiang, kutoka Tik Tok hadi puto hilo la hali ya hewa, katika miaka ya hivi karibuni, mara kwa mara Marekani inaipaka matope China kwa madai kuwa inataka kuiba siri zake, lakini Marekani ndio nchi kubwa zaidi ya ujasusi duniani.
Kwa muda mrefu, Marekani imekuwa ikitumia vibaya teknolojia zake za juu kuchunguza kisiri nchi mbalimbali duniani, wakiwemo washirika wake, na bajeti yake kwa shughuli za kijasusi kwa mwaka inakaribia dola bilioni 90 za Kimarekani.
Marekani ina miradi na mipango mingi ya kijasusi, na unaojulikana zaidi ni mradi wa “Prism”. Mradi huo unafanya uchunguzi wa kisiri duniani saa 24 kwa siku, hata dhidi ya wakuu wa nchi wenzi wa Marekani. Mradi wa Muscular wa Marekani unaingia seva za wingu za tovuti kama vile Google ili kuiba data za kisiri za watu binafsi duniani.
Licha ya teknolojia ya mtandao, Marekani pia inatumia sana vyombo vyake vya usafiri wa anga kama vile ndege na maputo kufanya ujasusi wa kisiri. Tangu Vita ya Baridi, Marekani ilianza kutumia maputo kuchunguza Umoja wa Soviet. Baadaye ilianzisha mradi wa kutafiti maputo maalumu ya ujasusi.
China ni moja ya nchi inayoathiriwa zaidi na vitendo vya ujasusi vya Marekani. Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani imefanya shughuli zaidi za kijasusi dhidi ya China. Njia inayotumia zaidi ni pamoja na kutuma meli na ndege za kijeshi, na kurusha maputo ya urefu wa juu. Kati ya njia hizo, ndege za kijeshi zimetumiwa zaidi.
Mwaka 2022 pekee, jeshi la Marekani limetuma zaidi ya ndege 600 za ujasusi katika Bahari ya Kusini ya China. Maputo ya urefu wa juu ni njia nyingine muhimu ya Marekani kuichunguza China.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Wang Wenbin hivi karibuni alisema, tangu mwezi Mei mwaka jana, Marekani imerusha idadi kubwa ya puto za urefu wa juu, na kuingia kwenye anga ya China zaidi ya mara 10 bila ya kupata kibali cha China.