Serikali ya Marekani inaendelea kuwafukuza wakimbizi weusi kutoka Afrika na Carrebian na kuwarejesha katika nchi zao zenye matatizo, huku Rais wa nchi hiyo Joe Biden, akitangaza hivi karibuni kuwakaribisha wakimbizi wa Ukraine. Wakimbizi wengi weusi wamesema kwa hasira kwamba huo ni ubaguzi wa rangi.
Mwaka 2020, rais wa zamani wa Marekani Donald Trump alipitisha sheria inayoitwa “Kifungu cha 42” cha kuzuia wahamiaji kwa kisingizio cha kukabiliana na janga la COVID-19. Baada ya Joe Biden kuingia madarakani, serikali ya Marekani imeendelea na sheria hiyo, ambayo inalenga zaidi wakimbizi weusi kutoka Afrika na sehemu za Carrebian. Takwimu zinaonesha kuwa, tangu rais Biden aingie madarakani, makumi ya maelfu ya wakimbizi weusi kutoka Afrika na Carrebian wamefukuzwa nchini Marekani, wengi wao wakiwa wameishi Marekani kwa miaka mingi.
Picha na video ambazo zimesambazwa hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii zinawaonesha askari polisi wa Marekani waliovaa kofia za cowboy na kupanda farasi, wakipunga kamba ndefu kwa wakimbizi weusi huko Del Rio katika mpaka wa nchi hiyo na Mexcio. Baadhi ya wanamtandao wamesema picha hizo zinakumbusha jinsi watu weusi walivyodhulumiwa na wazungu wakati wa enzi ya utumwa nchini Marekani.
Wakati huohuo, tarehe 25 mwezi uliopita, rais Biden alipohudhuria mkutano wa NATO nchini Ubelgiji, alitangaza kwamba, Marekani itawapokea wakimbizi 100,000 wa Ukraine waliokimbia makazi yao kutokana na vita kati ya nchi hiyo na Russia, na kutoa dola bilioni 1 za ziada kama msaada wa chakula, dawa, maji na vifaa vingine kwa ajili yao. Mbali na hayo, Marekani itatoa hadhi ya kulindwa ya muda kwa Waukraine wengine 30,000 ambao tayari wako Marekani, na kuhakikisha hawaathiriwi na Kifungu cha 42.
Tangu kutokea kwa vita nchini Ukraine, ubaguzi wa rangi ulioota mizizi katika jamii ya Magharibi umezidi kudhihirika kupitia suala la wakimbizi. Kauli kama vile “watu hawa wanaokimbia vita sio kama wakimbizi wa Syria”, “hii sio Afghanistan, hii sio Iraqi, vita inafanyika Ulaya iliyostaarabika” zimesikika mara kwa mara katika vyombo vya habari vya nchi za magharibi. Ikiwa hizi ni kauli tu zinazoonesha wazo la “Wazungu wako juu zaidi”, basi njia tofauti za kuwatendea wakimbizi ni kitendo halisi cha ubaguzi wa rangi.
Kama Rais Biden wa Marekani alivyosema mwenyewe, ubaguzi wa rangi ni doa la Marekani. Wakati Marekani inatekeleza ubaguzi wa rangi dhidi ya wakimbizi, kinachoitwa “mtetezi wa haki za binadamu” na “Mnara wa uhuru” kinamaanisha unafiki na aibu tu kwa nchi hiyo.