Marekani imepandisha kiwango cha tahadhari kwa raia wake wanaopanga kusafiri kwenda Kenya kutoka Level 2: Exercise Increased Caution hadi Level 3: Reconsider Travel, ikiashiria kuwa wasafiri wanashauriwa kutathmini upya mipango yao ya safari kutokana na hatari zilizotajwa na serikali hiyo.
Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza mabadiliko hayo Jumatatu, Oktoba 19, 2026, ikitaja wasiwasi unaohusiana na afya, uhalifu, utekaji nyara, ugaidi, machafuko na usalama barabarani.
Ebola miongoni mwa sababu za tahadhari mpya!
Elewa hadi kufikia sasa Kenya imethibitisha visa vinane vya Ebola aina ya Bundibugyo.
Tahadhari hiyo pia inataja hatari za uhalifu na ugaidi, pamoja na uwezekano wa maandamano na migomo kusababisha vurugu na kuvuruga usafiri.
Marekani imeendelea kuweka kiwango cha juu zaidi cha tahadhari, Level 4: Do Not Travel, kwa maeneo maalumu, yakiwemo vitongoji vya Eastleigh na Kibera jijini Nairobi na baadhi ya maeneo ya kaskazini mashariki na pwani. Hii haimaanishi kuwa maeneo yote ya Kenya yako chini ya Level 4.
Tahadhari za safari za nchi za kigeni zinaweza kuathiri maamuzi ya watalii na wasafiri wa kikazi, na hivyo kuibua maswali kuhusu taswira ya Kenya kimataifa, sekta ya utalii na namna mamlaka zinavyoshughulikia changamoto za usalama na afya ya umma.
Hata hivyo, kupandishwa kwa kiwango cha tahadhari ya Marekani si marufuku ya safari kwenda Kenya, wala hakumaanishi kwamba kila sehemu ya nchi si salama. Ni ushauri rasmi kwa raia wa Marekani kuzingatia hatari zilizotajwa kabla ya kufanya uamuzi wa kusafiri.
Je, serikali ya Kenya inapaswa kueleza hatua inazochukua kukabiliana na Ebola na changamoto za usalama ili kujenga imani ya wasafiri wa kimataifa, au tahadhari hii inaonyesha haja ya kuboresha zaidi mifumo ya afya na usalama nchini?
Soma pia