Tarehe 12/04/2025 tume huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania ilivitaka vyama vya siasa kwenda kusaini fomu ya maadili na wakabainisha kuwa chama kitokachoshindwa kusaini fomu hiyo kitapoteza sifa ya kushiriki uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu 2025 na chaguzi zitakazofuata ndani ya miaka mitano ijayo.
Chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) kupitia kwa katibu mkuu wake
John Mnyika walisema hawatokwenda kusaini fomu hiyo. Aliandika
"Katibu Mkuu @ChademaTz sitakuwepo kwenye kikao cha tarehe 12 Aprili 2025 cha kushauriana na kusaini maadili ya uchaguzi ya 2025.
Ifahamike kuwa mwenye mamlaka ya kusaini maadili ya uchaguzi kwa niaba ya chama cha siasa ni Katibu Mkuu.
Katibu Mkuu sijateua kiongozi au afisa yoyote kwenda kushiriki kwa niaba yangu katika kikao hicho kitakachofanyika katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi @TumeUchaguziTZ Mkoani Dodoma. #NoReformsNoElection"
Madai
Kumekuwepo na Taarifa inayoambatana na grafiki inayofanania na ya MillardAyo ikieleza kuwa Maria Sarungi amechapisha kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X kuwa suala la CHADEMA kugomea kusaini fomu ya maadili hilo ndilo anguko la rasmi la CHADEMA. Tazama
hapa.
Uhalisia wa madai hayo
JamiiCheck imefanya ufuatiliaji wa kina na kubaini kuwa Taarifa hiyo si ya kweli. Ufuatiliaji kwa njia ya maneno muhimu yani 'keyword search' umebainisha kuwa maneno hayo hayajawahi kuchapishwa kwenye
ukurasa rasmi wa X wa Maria Sarungi.
JamiiCheck imefuatilia pia kwa njia ya mtandao inayooenekana kuwa ni grafiki ya chombo cha mtandaoni cha millardAyo na kubaini kuwa grafiki hiyo
haijachapishwa na chombo hiko katika ukurasa wao wowote ule. Aidha grafiki hiyo inaonekana kuwa na baadhi ya makosa ikiwemo kwenye upande wa tarehe ambapo wemeandika Mei 12, 2025 badala ya Aprili 12, 2025.
Hata hivyo Kupitia ukurasa wake wa X, Maria anaonekana kuunga mkono kilichofanywa na CHADEMA kuhusu kutokusaini fomu ya maadili rejea
hapa.