Source:
Na Waandishi Wetu
FAMILIA ya aliyekuwa mbunge wa Tarime, marehemu Chacha Wangwe, imesema inamtambua Bibi Mariam, kuwa miongoni mwa wajane watatu wa marehemu ndugu yao.
Na imemtaka Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Wilbroad Slaa, kutorudia kutamka kuwa mwanamke huyo hakuwa mke halali wa marehemu.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, msemaji wa familia hiyo Profesa Samwel Wangwe, alimtaka Dkt. Slaa kuacha kuingiza siasa katika familia yao na kama alitaka kujua alipaswa kuuliza.
"Yule (Mariam) ni mke wa mdogo wetu, yeye (Dkt Slaa) hapaswi kuhoji mambo ya familia," alisema na kusisitiza kuwa familia inamtambua. Alisema wake wote watatu wa marehemu Wangwe waliolewa kwa ndoa ya kimila na kulipiwa mahari, hivyo alimalizana na wazazi wao.
Alisema anaamini Dkt. Slaa amekosea kwa kutoa kauli hiyo na anaamini kuwa hatarudia kutoa maneno ya aina hiyo.
Kauli hiyo ya Profesa Wangwe iliungwa mkono na mdogo wake, Bw. Gideon Wangwe, ambaye alimtaka Dkt. Slaa kuacha mara moja kuingilia masuala ya familia kwa kuwa Bibi Mariam alikuwa mke halali wa marehemu ndugu yao.
"Dkt. Slaa ameanza kuwa mwongo, kwa sababu huyo anayemsema ndiye anaishi na watoto wote tisa na ni ndiye anayewasomesha," alisema na kusisitiza kuwa wanamtambua kwa muda mrefu kuwa ni mke wa marehemu Wangwe.
"Kama anasema si mkewe basi awataje wale anaowafahamu ... ana ushahidi gani kuwa yeye si mke wa marehemu?," alihoji Profesa Wangwe na kuongeza kuwa kutokana na kauli yake hiyo, kwa sasa familia inafikiria kumpeleka mahakamani, kwa kuwa ameanza kudhalilisha familia na kutumia kifo cha ndugu yao kujitafutia umaarufu kisiasa.
Kwa upande wake, Bibi Mariam alisema madai yaliyotolewa na Dkt. Slaa dhidi yake kuwa si mke halali wa marehemu, inaonesha kuwa ni mwendelezo wa chuki dhidi ya familia yao hata baada ya kifo cha Bw. Wangwe.
Aliitafsiri kauli hiyo kuwa "ni ya kihuni na ya kike, kwani haikutakiwa kutolewa na mtu kama Dkt. Slaa, ambaye aliwahi kuwa padri.
"Kama anasema mimi sikuwa mke wake, aeleze yeye alihudhuria harusi ya nani kati ya wake watatu kati ya Ghati, Dotto na mimi (Mariam), wakati ndugu walioshiriki kunilipia mahari wananitambua," alisema Bibi Mariam.
Alisema Dkt. Slaa anapaswa kutambua kuwa hoja iliyopo mbele yao si nani mke wa marehemu, bali ni utata uliogubika mazingira ya kifo cha mumewe.
Huku akionekana wazi kukerwa na kauli hiyo, Bibi Mariam alisema hata wao wakiamua kumchambua Dkt. Slaa, si msafi, lakini hawawezi kufanya hivyo kwa sababu watakuwa wakifanya mambo aliyoyaita ya kike.
Alisema kama anasema yeye si mke halali wa marehemu ilikuwaje kifo kilipotokea alipewa nafasi ya kutambua mwili na kusimamia kazi ya uchunguzi iliyokuwa ikifanywa na madaktari.
"Dodoma aliniona nikiutambua mwili wa marehemu, iweje sasa ananikana?," alihoji na kuongeza kuwa hata kwenye mikutano ya CHADEMA alikuwa akipewa nafasi ya kujitambulisha kama mke wa marehemu Wangwe na Dkt. Slaa alikuwa akiona, iweje ahoji sasa?," alihoji.
Alimtahadharisha kuwa hizo siri ambazo Dkt. Slaa anadai atazitoa dhidi yake, awe na uhakika nazo vinginevyo akiendelea kumchafua, atamburuta mahakamani.
"Atakachokisema awe na uhakika, vinginevyo 'nitakufa' naye mahakamani," alisema na kusisitiza kuwa hawezi kunyamaza kutokana na vitisho vya Dkt. Slaa, badala yake ajiulize yale anayosema ana uhakika nayo vipi ndani ya jamii.
"Mimi ninachokisema kina maslahi kwa familia, aliyekufa ni mume wangu nataka uchunguzi ufanyike ili kuondoa majungu," alisema na kuongeza kuwa tangu kifo cha mumewe kitokee, hajawahi kusema kitu chochote hadi alipozungumza na waandishi wa habari Ijumaa wiki iliyopita.
Kuhusu kauli ya Spika wa Bunge, Bw. Samuel Sitta ya kupuuza ombi lake la kutaka aunde Tume ya kuchunguza kifo cha marehemu Wangwe, alisema hakutarajia majibu yaliyotolewa na Spika.
"Kama anaona nilikosea, alipaswa kunishauri, anajua uchungu nilionao na yeye alikuwa na uchungu mwingi na alilia sana siku ya msiba, sasa leo anataka kutuambia uchungu aliokuwa nao umekwenda wapi?," alihoji Bibi Mariam.
Alisema kauli ya Bw. Sitta kuwa Bunge lisitwishwe mzigo wa kuchunguza kifo hicho, inalenga kuonesha kuwa leo hii kifo cha mumewe kimeishageuka mzigo kwa Bunge.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki iliyopita, Bibi Mariam aliomba kufanyika upya kwa uchunguzi wa kifo cha mumewe. Pia alidai viongozi wa CHADEMA wamemtelekeza.
Wakati huo huo, viongozi wa CHADEMA wilaya ya Kinondoni, wamemtaka Dkt. Slaa kumwomba radhi mjane huyo, kutokana na kauli aliyoitoa kuwa hamtambui kama mke wa marehemu.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa Vijana wa Wilaya ya Kinondoni, Bw. Maulid Mkwanja, alisema umoja huo umesikitishwa na kauli ya Dkt. Slaa kwa sababu Bi. Mariam anatambulika kama mke wake tangu zamani.
"Tangu zamani anafahamika kuwa ni mke wa marehemu Wangwe na kila alipokwenda iwe kwenye mikutano ya kichama alitambulishwa kuwa ni mke wake, iweje leo hii wamkane?," alihoji Bw. Mkwanja na kuongeza:
"Sisi kama chama wilaya, tunamtaka Dkt. Slaa amwombe radhi huyo mjane na kama hatafanya hivyo, watakutana ili kujua hatua za kuchukua."
Alisema kama Dkt. Slaa alikuwa na chuki binafsi na marehemu Wangwe asiziingize kwa mkewe au familia yake.
Kiongozi huyo alimtaka Dkt. Slaa awe anatafakari kauli zake kabla ya kuzitoa hadharani kwa sababu amemdhalilisha Bibi Mariam na watoto wake kwa ujumla.
Akizungumzia kauli ya Spika Bw Sitta, aliyoitoa baada ya mjane huyo kumwomba aunde Tume, alisema haikuwa busara kumwambia kuwa amekurupuka, bali alitakiwa kumsaidia.
"Alitakiwa amsaidie kwa kuunda Tume kwa kuzingatia kuwa kifo chake kiligubikwa na mazingira ya utata," alisema.
Dkt. Slaa alikaririwa akisema hawamtambui mjane wa Wangwe, Bibi Mariam aliyeomba kufanyika kwa uchunguzi upya, kwani wake za marehemu wanaowatambua wako Tarime.
Dkt. Slaa kupitia taarifa ya habari ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC Taifa) juzi alimtaka mjane huyo kuweka wazi ni kwa vipi CHADEMA haikushiriki mazishi ya Wangwe.
Marehemu Wangwe alikufa katika ajali ya gari iliyotokea Julai 28 mwaka huu, wilayani Kongwa eneo la Pandambili mkoani Dodoma akiwa njiani kuelekea Dar es Salaam.
Mazingira ya kifo chake yalizua utata ambapo hadi sasa baadhi ya watu hawaamini kama alikufa kifo cha ajali ya kawaida.