Hizi nyimbo za kusema uongozi bora tumeanza kuzisikia toka enzi za uhuru,i.e,watu,siasa safi,uongozi bora...Wako wapi? Tunaambiwa wapo,watajitokeza lini??
Wote tunajua hii nchi inahitaji nini,lakini how do we get it?It has to come from us.Sisi wabongo hatuwezi kubadilishwa na viongozi wetu hata siku moja.Sasa hivi kuwa kiongozi imekuwa ni short cut to riches.Kiongozi mlarushwa siku hizi sio siri tena kama zamani,tokea Azimio la Zanzibar mambo yamekuwa waziwazi kabisa.Sisi wananchi kila siku humu tunawataja viongozi wala rushwa,tena kufuatana na dili zao,sio mambo ya kukisia tu kama zamani.Hata madereva wa taxi utawakuta wanaongelea rushwa za viongozi,utasikia dereva anakuonyesha ghorofa na anakwambia hii ni ya Anna Mkapa,huyo ni dereva wa taxi,yaani imekuwa ni kitu cha kawaida.
Sisi wananchi wa kawaida ndio tunatakiwa tubadilike ili uongozi ubadilike.Viongozi hawa wanatoka humuhumu amongst us.
Leo hii,majority yetu humu tukipewa platform tuseme tunachoandika humu hakuna atayejitokeza,labda tutampata Freeman Mbowe pekeyake!Do we need a kiongozi to change us even for that?
Mzee Zanaki, Heshima yako,
Ni kweli, viongozi wetu sasa hivi wanafanya juhudi za kuitamadunisha rushwa. Wanataka tufikie mahala kama Zaire ambapo mtu asiyepokea rushwa au kuiba ndiye anaonekana tofauti na anaweza kuhadhibiwa. Tumekwisha anza kuzoea ntaratibu. Mtu anaiba, akitekenywa, anasema wanamuonea wivu kwa sababu anataka kugombea uraisi na watu wanakaa kimya. Hivyo, sifa ya kugombea uraisi lazima kwanza uwe fisadi.
Hata hivyo, binafsi, siamini dhana ya kuwa kuna kundi fulani la watu wachache ndani ya jamii ya Tanzania, ambalo miongoni mwao wapo watu waliozaliwa na sifa kamilifu za kuongoza. Kana kwamba kazi yetu, ni kuainisha hao watu na kuwakabidhi dhamana ya taifa letu ili watuongoze. Hata hivyo, naamini kuwa nchi nzima, au jamii yote ya watanzania kwa ujumla wake, ni bwawa ambamo kuna watu wana vipaji mbalimbali na bongo bora kiasi kwamba tunaweza kuvua mawazo ya busara ambayo yanaweza kutuendeleza na mwishowe tukawa na taifa tunalotaka kulijenga.
Ni kweli, mojawapo ya matatizo yetu ni ukosefu wa viongozi bora, lakini hili siyo tatizo pekee, na si kweli kwamba tukipata viongozi bora tutapiga hatua muhimu. Kuendelea kuamini hii dhana ni kupalilia mazishi ya umuhimu wa nafasi ya watu wote ndani ya jamii yetu katika ushiriki wa kulipia gharama za maendeleo. Kimatendo, kuna tofauti kubwa baina ya cheo na uongozi. Binafsi naamini kwamba uongozi si cheo, na wala cheo si uongozi. Kushindwa kupambanua hizi tofauti ndiko kumetufikisha mahala ambapo watawala wetu wanaamini kwamba siku wanapopata cheo, busara zinakuja papo kwa papo, hivyo kututaka tuwatambue kuwa wao ni viongozi.
Hakuna mwanadamu aliyemkamilifu. Binadamu asili yetu ni wadhambi na wala sio malaika. Tumeumbwa na karama mbalimbali ambazo ni tofauti, kama unavyoona mtu mwembamba, mnene, mpuuzi, mjinga, mwelevu, kimo cha kati, mrefu, mfupi, au mbirikimo, mwaminifu, mwizi, mwema, mwenye tama, kipofu, kiziwi, kilema, mdokozi, na mrembo. Hakuna mwanadamu aliye na karama zote katika ukamilifu wake. Si haba kumkuta aliyejaliwa na akili nyingi, lakini ana udhaifu wa kudokoa jikoni. Mwingine anaipenda sana nchi yake, lakini hana busara, ahambiliki, hashauriki, au ana udhaifu wa kidikiteta.
Bahati mbaya, karama na baadhi ya tabia zinabadilika kutoka na mazingira, malezi, vichocheo vya kibaiologia ndani ya mwili, au umri. Ndio maana watu wengine wanapopata madaraka wanalewa au wanakuwa limbukeni. Wengine wanapopata fedha ndipo tabia zao zinajitokeza (true color). Mwingine hajijuhi tabia yake mpaka anapokuwa masikini. Hivi ndivyo mungu alivyotuumba. Katika sehemu iliyokubwa ya maisha ya kijamii, kuungana kwa karama zote ndani ya mtu mmoja hakutokei. Hata watu mithiri ya Nyerere ambao wanasifika kuunganisha busara na cheo, ingawa pia alikuwa na udhaifu mwingine, hawazaliwi kila mwaka.
Lazima tutambue kwamba hazina ya uongozi wa jamii yetu haiko katika uongozi rasmi tu, kwa maana ya wale waliochaguliwa na ambao wamekalia vyeo, au wale walioteuliwa kufanya kazi za utendaji. Katiba ya nchi yetu inagusia umuhimu wa wananchi kwa ujumla wao katika maendeleo ya nchi. Hakuna mbadala wa maoni ya wananchi na utashi wao. Viongozi wote wa kisiasa wanawajibika kusikiliza wananchi wanasema nini na kuyatia maanani hayo yanayosemwa na wananchi. Wananchi ndio chimbuko la madaraka na nguvu ya watawala na wote wanaotarajia kuzungumza kwa niaba yao.
Utamaduni tunao ujenga wa kujiaminisha kuwa tatizo letu ni ukosefu wa viongozi bora, na wala si ukosefu wa wananchi wenye uwezo wa kuwajibisha viongozi wao, unajenga mazingira ya kuwatenga wananchi katika nafasi ya uwajibishaji na kuwafanya viongozi waamini kuwa wao peke yao ndio wanaweza kuleta maendeleo na kuiacha jamii nzima usingizini ikiwa inasubiri hayo maendeleo. Ndio maana viongozi wetu wanajiaminisha kwamba wanajua matatizo ya wananchi kuliko wananchi wenyewe wanavyoyajua. Binafsi naona tuachane na huu utamaduni kwa sababu unawafaa wale waliomo madarakani kwa sababu tu ya kupata maslahi ya muda, na hawajali nini kitatokea wakiisha kuondoka madarakani au kufa. Ni utamaduni ulioangamiza tawala nyingi katika historia ya mwanadamu.
Hivyo basi, naamini msingi wa maendeleo ni watu, ardhi, siasa safi, na uongozi bora. Kupigwa kaputi kwa sifa mojawapo katika huo mlolongo kuna athili mpangilio mzima wa maendeleo. Vyote vinategemeana kama ifanyavyo kazi milango ya fahamu ya mwili wa binadamu, na si rahisi kuvitenganisha. Nadhani ni makosa kuweka mustakabari wa maisha ya watanzania wote chini ya fadhila za kiongozi mmoja au kundi la watu (viongozi) tukidhani kwamba wao ni wakamilifu wa sifa zote. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tunapingana na sheria ya asili au ya yule aliyetuumba.
Imekuwa ni kawaida ya mwanadamu kunyoosha vidole au kumtafuta mchawi pindi mambo yaendapo mrama. Tunaliengua neno watu kwa sababu linatutaka na sisi tuwajibike. Neno watu halimaanisha wale wanaovaa Sketi na Blauzi, au Suluali na Shati tu. Si wakulima ambao mazao yao yanakopwa na wajanja bila malipo, alafu wao wanalidhika. Si wafanyakazi wanaonyanyaswa na baadae kila mmoja akaamua kuchukuwa chake mapema. Watu maana yake ni wale wabunifu, wanaohangaika kuyabadili mazingira yao. Wasio kubali kuonewa, kunyanyaswa, kutapeliwa, kupuuzwa, kutokusikilizwa, kuibiwa, kudanganywa, na kufanywa vichwa vya wendawazimu. Ni wale wanaoiwajibisha serikali, waliopita shule na shule ikawapitia.
Ingawa idadi ya watanzania imefikia milioni 35, lakini sio lazima yawepo mahusiano kati ya hiyo idadi ya watu, na idadi ya watu wa kuleta maendeleo. Kamwe, katika maendeleo, neno watu halina maana ya namba (interms of quantity). Lina maana niliyoielezea juu. Hivyo basi, tuna uhaba wa watu pamoja na viongozi. Hakuna nchi yoyote duniani iliyowahi kupata maendeleo thabiti na ya muda mrefu bila ushiriki wa watu katika kuiwajibisha serikali yao. Vivyo hivyo, hakuna nchi iliyojikomboa kutoka katika ukandamizaji wa aina yoyote bila watu wake kujitoa muhanga. Si mara nyingi viongozi wakawajibika kwa hiari yao. Makabulu wa Afrika Kusini waliachia ngazi kwa sababu nyingi, lakini mojawapo kubwa ni kuwa nchi ilifikia mahala ikawa haitawaliki. Philippines wananchi walichoka na mauzauza wakauzingira mji wa Manila mpaka Raisi wao akaamua kuingia mitini.
Ni udhaifu huu wa mwanadamu uliyoyafanya mataifa yaliyoendelea duniani yawe na mfumo wa checks and balance. Hakuna kumwachia kiongozi mambo yote, bali jamii nzima inawajibika katika kuangaliana na kukosoana. Si kweli kwamba viongozi wengi wanaotawala nchi zilizoendelea wana moyo wa kuipenda nchi yao kuliko wanavyojipenda wao. Wengi ni wabinafsi kama walivyo viongozi wa nchi yetu. Majuzi, Bob Ney ameingia kwenye daftari kama mbunge wa 40 kutoka katika bunge la Marekani, kufungwa jela kwa sababu ya vitendo vya rushwa.
lobbyists waliotembeza rupia katika mikataba ya IPTL na RADA nchini kwetu, hawana tofauti na wale walioko Marekani. Kuna mtu anaitwa Jack Abramoff ambaye alipokea $9 milioni kutoka kwa Raisi wa Gabon bwana Omar Bongo ili amfanyie mpango wa kukutana na Bush (New York Times 10, 2005). Rafiki zake wakubwa ni Newt Gingrich, Dick Armey, George Bush, na Tom Delay. Hata hivyo huyu jamaa amehukumiwa miaka 5 na ushee jela kwa sababu ya vitendo vya kuwaonga viongozi wa Marekani. Hajaanza kifungo chake kwa sababu wanataka atoe ushahidi against Tom Delay aliyekuwa spika wa bunge la Marekani.
Clinton anaeleza katika kitabu chake jinsi marafiki zake wa Arkansas walivyosekwa jela wakati anapelelezwa na alikuwa anaogopa kuwapigia hata simu ili asije kumbwa na obstruction of justice. Bush alimuona rafiki yake kipenzi Ken Lay akiendeshwa puta na vijana machachari wanaowakilisha maslahi ya wananchi bila msaada pamoja na kwamba alikuwa ni Raisi wa nchi. Raisi Nixon alikimbia miiba kwenye kiti chake cha enzi iliyowekwa na wananchi wanaoiwajibisha serikali yao. Matendo ya hawa viongozi yanatokana na woga waliono juu ya wananchi, na wala sio kutokana na moyo au uzalendo wa nchi zao.
Ni rafiki gani wa Kikwete, Mobutu, Gadafi, Banda, Mkapa, angeweza kwenda jela kwa sababu ya vitendo vya rushwa? Ni viongozi wangapi wa nchi za Afrika wako jela kwa sababu ya rushwa? Ni Raisi gani wa Afrika alijiuzulu baada ya kukiuka miiko ya uongozi?. Tatizo la Tanzania ni kuwa na Raisi mwenye nguvu kubwa kikatiba hivyo, kufanya wananchi wategemee fadhila zake. Katiba yetu imempa Raisi madaraka makubwa kiasi kwamba wananchi hawana huwezo wa kuthibiti matendo yake.Mfano, wananchi wakiamua kuwakilishwa na wabunge NCCR-Mageuzi, alafu wakamchagua Raisi kutoka CCM, Ibara ya 90 (1) (e) ya katiba ya nchi yetu inampa mamlaka Raisi kulivunja Bunge na kuitisha uchaguzi mpya hata kama kufanya hivyo, nikupingana na utashi wa wananchi.
Wabunge wetu ambao ni wawakilishi wa wananchi, hawana uwezo wa kikatiba wa kukusanya mawazo ya wananchi wanao wawakilisha na kuyapeleka bungeni kama muswada ili yapigiwe kura na wabunge wote. Mfano mzuri ni issue ya madawa ya kulevya iliyosimamiwa na Amina Chifupa. Kikatiba, Amina hawezi kukusanya mawazo ya watu ambao wanakelwa na tatizo la madawa ya kulevya, alafu akawashawishi wabunge ili itungwe sheria kutokana na mapendekezo ya watu. Anachoweza kufanya ni kuiomba serikali ianzishe muswada. Mfumo huu unaweza kuwa kizingiti kama tuna viongozi wa serikali wenye moyo wa kuipenda nchi yetu lakini wako addicted na madawa ya kulevya.
Tanzania tumejaliwa kitu komoja tu Ardhi, vingine inabidi tufanye juhudi za makusudi kuvipata.