Makamba ni kama Waziri anapokwenda bungeni
Na Zephaniaanjela
KATIBU Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba ameingia kwa kishindo katika Jambo Forums. Baadhi ya wachangiaji wakiwemo wachanga na wazoefu wanahoji ubunge wake wakidai hachangii katika vikao vya bunge.
Wanajaribu kuwasadikisha watu ili waamini eti hafai kuwa Mbunge na kuhoji uhalali wa kuteuliwa kwake kiasi cha wengine kutaka Rais Jakaya Kikwete atengue uteuzi wake kwa vile hauna faida yoyote.
Wanataka kila Mbunge asikike akizungumza bungeni iwe kwa kuuliza maswali ama kuchangia miswada kwa kusimama na kuonekana akighani mashairi yake huku "akirushwa" moja kwa moja ama vinginevyo na vituo vya televisheni.
Wanadhani ubunge ni kuzungumza sana, kuuliza maswali au kupinga hoja za serikali ili kutafuta sifa hata kama unachopinga hakina maana. Mimi nasema Makamba anafanya kazi nzuri kwa asilimia 100.
Akiwa Katibu Mkuu wa chama kinachotawala, Makamba ni sehemu ya watawala na viongozi waandamizi wa umma ambao kazi yao ni kupokea matatizo na kero za Watanzania, kuzifanyia utafiti wa kina kwa kuzifuatilia kwa karibu, kuzitafutia ufumbuzi, kusimamia utekelezaji wa mahitaji ya kero hizo na hatimaye kupeleka majibu kwa wananchi kuhusu nini kimefanyika katika lipi na kwa namna gani.
Mbunge kama Zitto Kabwe na Wilbroad Slaa wa CHADEMA, John Cheyo wa UDP, Anne Kilango - Malecela au Christopher ole Sendeka wa CCM, Mohammed Mnyaa wa CUF na wengine kama hao hawamo katika orodha ya watendaji na viongozi wa umma na ndiyo maana wanasikika sana wakipiga kelele bungeni.
Kama ilivyo kwa Wabunge ambao pia ni Wakuu wa Mikoa kama Dk. James Msekela (Mwanza), Monica Mbega (Ruvuma), Mohammed Abdulaziz (Tanga), Dk. Christine Ishengoma (Pwani) au Waziri Mkuu, Mawaziri au Naibu Mawaziri, kazi ya Makamba bungeni kamwe si kuuliza maswali au kuipinga serikali.
Wasiojua siasa hawafahamu kuwa kazi ya Makamba anapokwenda bungeni akiwa Mbunge ambaye ni Katibu Mkuu wa chama kilichopo madarakani kwa maana ya kuwa mtendaji wake mkuu ni kusikiliza matatizo yanayotolewa na Wabunge kama akina Zitto, Slaa, Anne Malecela na kadhalika na kuyatafutia ufumbuzi kwa kushirikiana na Wakuu wa Mikoa, Naibu Mawaziri, Mawaziri au Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Lakini kama ana mchango anaotaka kuishauri serikali kupitia wizara moja ama nyingine anafanya hivyo kama ilivyo kwa Wabunge ambao pia ni watendaji wa dola kama vile Mawaziri, Naibu Mawaziri, Mawaziri au Waziri Mkuu wanaochangia kwa njia ya maandishi.
Hivyo ndivyo Mbunge Yussuf Makamba anavyofanya na ndiyo maana si lazima kila kikao aingie ukumbini maana anaweza kuchangia namna hiyo akiwa ofisini kwake na kupeleka mchango huo kwa Spika, Naibu Spika au Mwenyekiti wa Bunge kwa njia ya barua.
Mbali na hilo, wanaodhani kwamba Makamba amekuwa akilipwa posho hata asipokwenda bungeni nao pia wana upeo mfupi wa masuala ya utawala na uongozi wa kisiasa.
Posho wanazolipwa Wabunge wanapokuwa katika shughuli za bunge hazitolewi kama zawadi, hivyo hakuna hata mmoja anayeweza kulipwa chochote huku akiwa katika shughuli zake mwenyewe au za chama chake kama ilivyokuwa mwezi uliopita wakati baadhi ya Wabunge wa CCM na CHADEMA walipokwenda Kiteto kufanya kampeni za uchaguzi mdogo wa kiti cha ubunge katika jimbo hilo.
Kwa hiyo, hata wanaohoji ilikuwaje Mbunge huyo wa Kuteuliwa akaenda Kiteto na kuacha Mkutano wa 10 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiendelea mjini Dodoma wote hawako makini, vinginevyo inawezekana hawana upeo mpana wa masuala ya kisiasa.
Kama ilikuwa haramu kwa Makamba kwenda huko ili kumfanyia kampeni aliyekuwa mgombea ubunge wa CCM, Benedict ole Nangole; inakuwaje iwe halali kwa Zitto, Slaa na Grace Kiwelu na kuliacha bunge na kwenda kusaidiana na Mbowe kusaka ubunge kwa aliyekuwa mgombea wa kiti hicho kutoka CHADEMA?