Mdau mmoja wa Jamiiforums ameonesha wasiwasi wake baada ya kwenda hospitalini kupima VVU ambapo tofauti na namna alivyotarajia, daktari wake alimpima kwa kutumia mate yaliyotolewa kwenye fizi ya juu na chini.
Jambo hili limemfanya atoe ushauri kwa watu kuwa makini wanapokuwa wanabusiana kwa kuwa tendo hilo linaweza kusababisha maambukizi ya VVU kupitia mate.
Ukweli wa jambo hili upoje?
Jambo hili limemfanya atoe ushauri kwa watu kuwa makini wanapokuwa wanabusiana kwa kuwa tendo hilo linaweza kusababisha maambukizi ya VVU kupitia mate.
Ukweli wa jambo hili upoje?
- Tunachokijua
- Ni kweli kuwa maambukizi ya VVU yanaweza kupimwa kwa kutumia majimaji yanayopatikana kwenye sehemu ya ndani ya kinywa cha mtu ambayo mara nyingi huchukuliwa kwenye fizi.
Kipimo hiki cha haraka kinachotoa majibu baada ya dakika 20 hufanya kazi kwa kutambua uwepo wa kinga mwili (Antibodies) anazozalisha mtu baada ya kupatwa na maambukizi ya VVU. Hata hivyo, ni muhimu kuweka sawa kuwa kipimo hiki hutumia majimaji ya kinywa ambayo hupatikana baada ya kusugua sehemu ya fizi na siyo mate halisi kama hoja ya mtoa mada ilivyo.
Je, mate yanaweza kubeba VVU?
Mate huwa na vimeng’enya vyenye uwezo wa kuharibu virusi kabla havijasambazwa na kuanza kushambulia, hivyo hayawezi kusababisha maambukizi ya ugonjwa huu.
Kwa upande mwingine, damu pamoja na mazao yake yanaweza kusambaza VVU. Ikitokea mtu mwenye virusi hivi akawa na damu kinywani inayotokana na uwepo wa michubuko au vidonda, kisha akabusiana na mtu mwingine mwenye michubuko au vidonda kinywani, mtu huyo anaweza kuambukizwa VVU.
Kwa ujumla wake, kuhusu maambukizi ya VVU kwa njia ya kubusiana, tafiti za kisayansi zinathibitisha mambo yafuatayo-
- VVU haiwezi kuambukizwa kupitia mate.
- Kubusiana siyo tendo baya, haliwezi kusababisha maambukizi ya VVU ikiwa wahusika hawatakuwa na vidonda au michubuko kinywani.
- Ikiwa mtu aliyeambukizwa VVU atabusiana na mtu asiye na ugonjwa huku wote wawili wakiwa na michubuko au vidonda, ugonjwa huu unaweza kuambukizwa. Hata hivyo, chanzo kitakuwa ni damu iliyovilia kwenye mate kutoka kwenye vidonda na michubuko na siyo mate yenyewe.