MATHARE, NAIROBI — Wakazi wa Mathare Number 10, Mabatini Ward, pamoja na Hospital Ward, Mathare 4B, wanakabiliwa na changamoto inayofanana ya mifereji ya majitaka inayopita karibu na makazi yao.Picha kutoka maeneo hayo zinaonyesha maji machafu na taka zikikusanyika katika maeneo yanayozungukwa na nyumba za wananchi.
Kwa wakazi, hili si suala la usafi pekee. Majitaka karibu na nyumba yanaweza kusababisha harufu mbaya, kuongezeka kwa wadudu na mazingira hatari kwa watoto, huku maji machafu yakiongeza hatari za magonjwa yanayohusiana na usafi duni.
Nani anawajibika?
Serikali ya Kaunti ya Nairobi, kupitia idara zinazohusika na maji, usafi wa mazingira na afya ya umma, pamoja na Nairobi City Water and Sewerage Company, ina jukumu muhimu katika kushughulikia huduma za majitaka jijini.
Katiba ya Kenya, Article 43(1)(b), inatambua haki ya kila mtu kupata viwango vinavyofaa vya usafi wa mazingira.
Kwa hivyo, wakazi wa Mabatini na Hospital Ward wanahitaji hatua, si ahadi: uchunguzi wa maeneo yaliyoathirika, kuondolewa kwa majitaka yaliyotuama na suluhisho la kudumu la mifumo ya majitaka.
Swali kwa viongozi wa Nairobi:Wakazi wa Mathare wataishi hadi lini karibu na majitaka? Na ni lini hatua ya kudumu itachukuliwa?