Matokeo ya Uchaguzi mdogo: Rafu Biharamulo
• Mawakala wa vituo tisa vyenye utata watoweka
na Mwandishi Wetu
DALILI zinaonyesha kuwa, matokeo ya Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Biharamulo Magharibi, yaliyompa ushindi mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Oscar Mukassa, yana kasoro, Tanzania Daima imebaini.
Habari ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka Biharamulo zinaonyesha kuwa, matokeo hayo yamepokewa kwa hali ya mshangao na kutoamini na wananchi wa jimbo hilo, ambao wamekuwa wakifuatilia kwa karibu mwenendo wa kampeni, upigaji kura na uhesabuji wake.
Kwa mujibu wa habari hizo, kikubwa kilichosababisha mshangao huo ni kuibuka kwa mzozo wa wazi wa matokeo kati ya vyama vikuu viwili, CCM na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambavyo kila kimoja kimejitokeza na kudai kuwa kimeshinda uchaguzi huo.
Taarifa ambazo wakazi wa Biharamulo walikuwa nazo hadi kufikia jana asubuhi, ambazo zilitiwa nguvu na habari zilizoandikwa na baadhi ya magazeti, zilikuwa zikionyesha kuwa, mgombea wa CHADEMA, Dk. Anthony Gervas Mbassa, alikuwa akielekea kushinda katika kinyang'anyiro hicho.
Hata hivyo, matumaini hayo ya CHADEMA ambayo yalichagizwa na taarifa za ushindi zilizosambazwa na viongozi wa chama hicho walioko Biharamulo, zilianza kuzimwa taratibu kuanzia asubuhi hiyo hiyo ya jana.
'‘Wakati tukisubiri mgombea mbunge wetu atangazwe kuwa ameshinda baada ya kuwa tumekusanya matokeo kutoka katika vituo vyote vya uchaguzi kutoka katika kata zote nane, tulianza kusikia taarifa za wanachama wa CCM, nao wakishangilia kuwa wameshinda kwa tofauti ya kura 2,000 kabla ya idadi kupungua hadi 1,500 na mwishoni kuambiwa kwa kura 800.
'‘Taarifa hizi zilianza kututia wasiwasi sana, na tulipokuwa tukipitia matokeo hayo, bado tuliendelea kupata hesabu zilezile kuwa sisi ndio washindi," alisema Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA wakati alipozungumza na Tanzania Daima, jana asubuhi.
Wakati taarifa za kukinzana zikiendelea kusambaa katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo, askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) walionekana kuanza kukusanyika kuzunguka jengo la Halmashauri ya Wilaya ambako ndiko ziliko ofisi za msimamizi wa uchaguzi.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, mzozo wa kupingana kuhusu nani hasa alikuwa mshindi kati ya vyama hivyo viwili, zilisababisha msimamizi wa uchaguzi huo, kuitisha kikao na viongozi wa pande zote mbili na kujadili kile kilichokuwa kimetokea.
Habari ambazo zilipatikana ndani ya mkutano huo zinaeleza kwamba, wakiwa ndani ndipo ilipobainishwa kuwa CCM walikuwa wameshinda, uamuzi ambao ulipingwa na CHADEMA iliyokuwa ikiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu kutoka Biharamulo, Zitto alisema mara baada ya kukutana na mahasimu wao hao, walibaini kuwapo kwa kasoro za uhesabuji kura katika vituo tisa vilivyo katika kata tatu tofauti.
'‘Msimamizi wa uchaguzi amemtangaza mgombea wa CCM kuwa ameshinda. Tumeyakataa matokeo, kwani tumebaini tumeibiwa kura waziwazi katika vituo tisa vya kata tatu ambako kura za CHADEMA zimepelekwa CCM na zile za CCM wamepewa CHADEMA," alisema Zitto kwa masikitiko.
Zitto, mmoja wa wanasiasa wa upinzani ambaye amekuwa mwepesi kukubali kushindwa kwa chama chake katika chaguzi ndogo ndogo kama zile za Busanda, Kiteto na kabla ya hapo Tunduru, alieleza kusikitishwa na hatua ya msimamizi wa uchaguzi kukataa ombi la CHADEMA la kutaka kura katika vituo tisa vyenye utata kuhakikiwa na kuhesabiwa upya.
Chanzo kingine cha kuaminika cha habari kutoka Biharamulo kinaeleza kuwa, CHADEMA walianza kupata taarifa za matokeo ya uchaguzi ‘kuchezewa' kutoka kwa baadhi ya maofisa wa serikali waliokuwa katika vituo kadhaa vya uchaguzi.
Zitto alipoulizwa kuhusu ukweli wa taarifa hizo, hakuwa tayari kukubali au kukataa zaidi ya kusema kwamba, walianza kupata taarifa mapema za kuwapo kwa mkakati wa kura zao kuhamishwa na kupewa mgombea wa CCM.
Katika hali ya kustaajabisha, Zitto alisema, mawakala wa chama chao wa vituo vyote tisa vyenye utata, ambavyo hakuvitaja, walikuwa hawajulikani walipo, tukio ambalo linawatia wasiwasi wa kuwapo kwa vitendo haramu katika zoezi hilo.
Wakati CHADEMA wakilalamika, matokeo ambayo yalitangazwa majira ya saa 7:05, mchana jana yanaonyesha kuwa, mgombea wa CCM, ameshinda kwa kura 17,561 (51%) dhidi ya yule wa CHADEMA aliyepata kura 16,700 (48.4%), huku mgombea wa TLP akiambulia kura 198.
Akitoa sababu za kukataa matokeo hayo, ikiwa ni pamoja na kugoma kusaini fomu ya kukubali matokeo, mgombea wa CHADEMA, Mbassa alisema kuwa, matokeo ya kata tatu yalikuwa yamebadilishwa tofauti na walivyosaini wasimamizi wa matokeo na yalivyohesabika vituoni.
Alisema matokeo ya jumla yaliyokuwa yamebandikwa awali katika vituo vya kupigia kura baada ya kura kuhesabaiwa, yalionyesha kuwa CHADEMA ilikuwa imeshinda.
Baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, hali ya mji wa Biharamulo ilikuwa kimya huku askari wa kutuliza ghasia wakiwa wamezunguka mitaani. Licha ya wafuasi wachache wa CCM kushangilia, watu wengine walionekana kuwa kimya katika vikundi wakijadiliana.
Kwa mujibu wa CHADEMA, matokeo yao yalikuwa yakionyesha kuwa mgombea wao alikuwa amepata kura 17,313 wakati yule wa CCM akipata kura 16,682.
Akizungumzia hali hiyo, Zitto alisema kuwa wamekataa kusaini fomu ya kukubali matokeo kwa sababu wanajua kuwa wamechezewa rafu, na kwamba wananchi wa Biharamulo wamenyimwa haki yao ya kumchagua kiongozi.
"Sisi tulijua kuwa tumeshinda tangu jana usiku (juzi) baada ya kuhesabu kura na kuhakikisha hilo, ndiyo maana wafuasi wa CHADEMA walianza kushangilia," alisema Zitto.
Aliongeza kuwa, wamewatuliza wafuasi wao wasionyeshe hali yoyote ya hasira au kufanya vurugu, wala hawataenda mahakamani, kwani wanaamini chama hicho kitafanya vizuri katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.
"Tumewatuliza wananchi wasifanye fujo yoyote, kwani walikuwa na jazba. Sisi hatuamini kilichotokea, ndiyo maana ukimya umetawala Biharamulo. Ni vigumu kuamini mchezo uliofanyika," aliongeza Zitto.
Habari nyingine kutoka huko zinaeleza kuwa, wakati matokeo yanatangazwa, baadhi ya wafuasi wa CHADEMA waliokuwa wakihofiwa kuwa wangeweza kufanya vurugu, walikuwa wakishuhudia ulinzi mkali wa polisi katika maeneo mbalimbali.
Akizungumzia hilo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Kapteni mstaafu, George Mkuchika, alisema kuwa, wao walihesabu kura tangu juzi usiku, wakajua mapema kuwa wameshinda.
Alisema walipolibaini hilo, walianza kuwawatuliza wafuasi wao wasishangalie mpaka hapo Tume ya Uchaguzi itakapotoa matangazo rasmi.
Aliitaka CHADEMA kuyatambua matokeo hayo kwani ushindi wao ulionekana wazi tangu awali. "Tunaitaka CHADEMA itambue matokeo hayo, kwani hata sisi tulihesabu kura tangu jana usiku (juzi), tukajua kuwa tumeshinda," alisema Mkuchika ambaye alikuwa akizungumza akiwa jijini Dar es Salaam. Katika taarifa za awali, mpaka zinapatikana hesabu za mwisho kutoka katika vituo vya kupigia kura kukiwa bado kituo kimoja cha Nyabugombe B chenye wapiga kura 394, CHADEMA ilikuwa ikiongoza kwa asilimia 50.6, huku CCM ikiifuatia kwa karibu ikiwa na asilimia 48.8 ya kura zote na TLP ikiwa imejinyakulia asilimia 0.55.