Chadema wasema CCM wamefulia
CCM wataka kura zihesabiwe upyaa
Wafuasi wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika jimbo la Biharamulo mkoani Kagera, usiku wa kuamkia leo hawakulala…wamekesha mitaani wakicheza na kuimba baada ya kuelezwa na viongozi wao kwamba, piga ua galagaza chama chao kimeshashinda uchaguzi huo mdogo.
CCM wamefulia…CCM wamefulia, yalikuwa ni baadhi ya maneno waliyokuwa wakitamka kwenye nyimbo zao za shangwe. Wakati Chadema wakishangilia ushindi, zoezi la kuhesabu kura limelazimika kurudiwa upya baada ya kutokea mkanganyiko.
Ulazima wa kurudia zoezi la kuhesabu kura ulitokana na kila chama, Chadema na CCM kudai kwamba kimenyakua kiti hicho cha ubunge katika uchaguzi huo mdogo uliofanyika jana.
Kwa mujibu wa Chadema, mgombea wao, Dk. Antony Mbassa ameshinda baada ya kupata kura 17,313. Chadema wanadai mgombea wa CCM, Oscar Mukasa amepata kura 16,882.
CCM, kwa upande wao wanadai kuwa mgombea wao ndiye aliyepata kura 17,313 na wa Chadema akapata kura 16,886 na hivyo mgombea wao ndiye kashinda.
Kutokana na mkanganyiko huo kura zililazimika kuhesabiwa upya. Leo asubuhi wafuasi wa chama cha Chadema walidamkia kwenye ofisi za Halmashauri ya Wilaya huku wakiimba nyimbo zao zile zile za CCM wamefulia.
Wafuasi wa CCM waliokuwa wamevalia sare za chama chao na kofia, walijikusanya katika ofisi yao iliyopo katika ofisi za Halmashauri hiyo. Nao walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali ukiwemo ule maarufu wa "Wembe ni ule ule ushindi…wembe ni ule ule ushindi". Askari wa kikosi cha kutuliza ghasia, FFU, waliokadiriwa kufikia 200 walionekana wakivinjari katika viunga vya Halmashari hiyo.
Hata hivyo hadi tunakwenda mitamboni zoezi la kuhesabu upya kura lilikuwa bado linaendelea.
CHANZO: ALASIRI