Source ( Kabla Sijaulizwa) Mwananchi
Waandishi Wetu
JABALI la siasa nchini, John Malecela, maarufu kama tingatinga yuko katika hali mbaya kutokana na kubanwa mbavu kwenye kura za maoni, huku baadhi ya mawaziri wakiwa katika hatihati ya kupoteza ubunge, kwa mujibu wa matokeo ya awali ya kura za maoni ndani ya CCM.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Diodorus Kamala, na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Chiligati walikuwa kwenye hali mbaya baada ya matokeo ya awali ya kura za maoni kutangazwa.
Lakini Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe walikuwa miongoni mwa mawaziri waliokuwa wakielekea kushinda, sambamba na naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi huku ushindi wa naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera ukiamsha vurugu wilayani Korogwe.
Mbali na mawaziri, wabunge kadhaa ambao walikuwa vinara kwenye Bunge la Tisa wanaweza kuwa wamefunguliwa mlango wa kwenda nje ya chombo hicho cha kutunga sheria.
Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii, mbunge wa Bumbuli, William Shelukindo, Mudhihir Mohamed Mudhihir (Mchinga), Tatu Ntimizi (Igalula), Siraju Kaboyonga (Tabora Mjini), Wilson Masilingi (Muleba Kusini) na mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro wakiwa kwenye hali ngumu ambayo inaweza kuwafanya wasirudi bungeni.
Lakini wabunge wengine walio kwenye orodha ya wapambanaji, Harrison Mwakyembe (Kyela), Anne Killango (Same Mashariki), mbunge wa Ilala, Mussa Hassan Zungu na Jenister Mhagama (Peramiho) walikuwa wakielekea kuibuka na ushindi na kurejea kwenye chombo cha kutunga sheria.
Wagombea wapya ambao wanaonekana kuelekea kuingia bungeni ni pamoja na katibu mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka (TFF), Frederick Mwakalebela ambaye anaelekea kumuangusha Monica Mbega (Iringa Mjini), Hussein Bashe ambaye anaelekea kumshinda Selelii (Nzega), Donald Max ambaye anaelekea kumshinda Ernest Mabina wa Geita na Januari Makamba, ambaye alikuwa anaelekea kumshinda Shelukindo jimbo la Bumburi.
Hadi tunaenda mtamboni, Habel Chidawali anaripoti kuwa katika jimbo la Mtera mkoani Dodoma mambo hayakuwa yakimwendea vizuri Malecela, ambaye kwa vipindi tofauti amekuwa akipita bila ya kupingwa kutokana na mpinzani wake, Livingstone Lusinde kumkalia kooni.
Habari zinasema kuwa Malecela alikuwa akiongoza kwa tofauti ya kura chache kwenye majimbo ambayo ana nguvu nyingi huku mpinzani wake akishinda kwenye kata za nne za mjini, zikiwemo za Fifi na Ilolo.
Matokeo rasmi kutoka vituo vingine hayakuweza kupatikana, lakini wachambuzi wanaona kuwa mwanasiasa huyo wa muda mrefu anaweza kuibuka na kura nyingi kwenye kata za vijijini.
Lakini Spika wa Bunge la Muungano ambaye amemaliza muda wake, Samuel Sitta alikuwa akielekea kufanya vizuri kwa kuwaacha kwa mbali washindani wake.
Kwa mujibu wa taarifa hizo za awali, hadi usiku wa saa 4:37 wakati Sitta alishashinda kwa zaidi ya robo tatu. "Mambo si mabaya naendelea vizuri na nimeshinda kwa mbali zaidi ya watu waliofuatia," alisema Sitta alipoulizwa kuhusu matokeo ya awali.
Kwenye jimbo la Mtama, Membe, alishashinda bila ya kupingwa kama ilivyokuwa kwa naibu waziri wa Utalii, Ezekiel Maiga. Membe alitamba kwamba alichokuwa akikifanya jana ni kufuatilia unyago wa wenzake tu.
Mjini Songea, katika kata 17 naibu waziri, Dk Emmanuel Nchimbi alikuwa akiongoza katika kata 14 huku matokeo ya kata nyingine zilizobaki yakitarajiwa kutangazwa baadaye.
Mpinzani wake ni Oliver Mhaiki. Kwenye jimbo la Mchinga, Mudhihir alikuwa na wakati mgumu kutokana na upinzani mkali unaowekwa na Said Mtanda ambaye ni msaidizi wa katibu mkuu wa CCM, Yusuph Makamba.
Kwa upande wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kepteni John Chilligati, katika matokeo hayo ya awali, ameweza kushinda katika kata tatu kati ya 19 huku mpinzani wake Dometri Mtaka, ambaye ni mfanyakazi wa Takukuru, akiongoza katika kata 9.
Mkoani Tabora, Victor Kinambile anaripoti kuwa matokeo ya awali yanaonyesha wabunge waliomaliza muda wao, Juma Kapuya wa Urambo Magharibi, Teddy Kasela Bantu (Bukene), Samuel Sitta (Urambo Mashariki), na Rostam Aziz wa Igunga walikuwa wakiongoza kwa zaidi ya asilimia 70. Lakini Selelii (Nzega), Tatu Ntimizi (Igalula), na Siraju Kaboyonga wa Tabora Mjini wakiwa katika hali mbaya.
Upinzani mkali kwenye jimbo la Tabora Mjini ni kati ya Mwanne Mchemba na Ismail Aden Rage. Mkoani Kagera Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Diodorus Kamala wa Nkenge aliangushwa na mwenyekiti wa Jumuiya ya wanawake wa chama hicho, Ansupta Msham. Aliyekuwa mbunge wa Muleba Kusini, Wilson Masilingi aliachwa mbali na Profesa Anna Tibaijuka aliyepata kura 5,275 dhidi ya kura 2,092 katika vituo 33.
Mkoani Tanga, Burhan Yakubu anaripoti kuwa Henry Shekifu anaongoza matokeo ya awali ya jimbo la Lushoto, January Makamba anaongoza Bumbuli dhidi ya William Shelukindo, Dk Abdallah Kigoda anaongoza Handeni, Omar Pamba anaongoza Pangani, huku Korogwe kukiwa na vurugu baada ya matokeo hayo kugubikwa na utata. Katika matokeo hayo ya awali, Nasir alionekana kushinda lakini baadaye mambo yakawa yamebadilika jambo ambalo lilizua vurugu.
Wilayani Temeke, Zaina Malongo anaripoti kuwa kwenye Tawi la Wailes, mgombea anayetetea nafasi Abass Mtemvu amepata kura 142, Salim Chicago kura 43, Tambwe Hiza kura 42, Ngulangwa 12, Manji 6, Kusaga 5, Lukwembe kura mbili na Nyalali alipata kura mbili huku Nondo na Meja Jamson wakipata kura moja moja. Kata ya Mtoni, Chikago 182, Tambwe 109, Ngulangwa 89, Mtemvu 75, Kusaga 69, Nondo 50, Manji 29, Meja Jamson 10 na Lukwembe tano.
Kutoka Ilala, Pamela Chilongola anaripoti kuwa Jimbo la Segerea katika Kata ya Kinyerezi, Milton Makongoro Mahanga alipata kura 188 dhidi ya 164 za Joseph Kessy, 133 za Glorious Luoga, Kibamba Kiomoni kura 59, Selemani Ditopile 43, Solustian Katto kura 15, John Jambele kura 33, Paulo Mahondo kura 10, Zahoro Lyasuka kura 10, Venance Victor kura 13, Jaji Mafuru kura saba, Daudi Nguzo kura sita.
Jimbo la Ilala matokeo ya awali yalionyesha kuwa Mussa Azzan Zungu alikuwa akiongoza dhidi ya wapinzani wake takriban nane. Kutoka Newala, Salim Said anaripoti kuwa mchuano ulikuwa mkali kati ya Rashid Akbal, Juma Manguya na George Mkuchika na kura zilikuwa zinapanda na kushuka.
Jimbo la Singida Mjini, taarifa za awali zilieleza kuwa, Mohammed Dewji alikuwa akiongoza kwa asilimia 96 kwa kura 7988, akifuatiwa Hawa Ngulume kura 390 na Msawira kura 43.
Kutoka Ubungo, Hussein Issa na Raymond Kaminyoge wanaripoti kuwa matokeo ya awali yalionyesha kuwa Shamsa Mwangunga alikuwa akiongoza dhidi ya wapinzani wake 13 akiwamo Nape Nnauye. Pia katika jimbo la Kinondoni nyota iliendelea kungaa kwa Idd Azzan ambaye alikuwa akiongoza dhidi ya wenzake.
Katika jimbo la Arusha Mjini, Batilda Buriani alikuwa anaongoza ambapo katika Kata ya Moshono alipata kura 118, Felix Mrema anayetetea alipata kura 50, katika Kata ya Levolosi Batilda alipata kura 195, huku Mrema akipata kura 103.
Katika kata ya Kati Batilda alipata 108 huku Mrema akipata 35, Kata ya Olorieni Batilda 295, Mrema 97, Kata ya Unga Limited, Batilda 238, Mrema 118, wakati katika Kata ya Sokoni 1, Batilda (256), Mrema (156) na Kata ya Engosheraton Batilda (109) huku Mrema akiambulia 20, huku katika kata ya Sokoni 2, Batilda 236 na Mrema 159.
Kutoka Singida, Awila Sila anaripoti kuwa Mohammed Dewji alikuwa akiongoza kwa kura 5,180, Hawa Ngulume 225, Mariamu Msawila kura 28, bado vituo 14. Kutoka Songea Mwandishi Wet anaripoti kuwa katika Kata ya Ruvuma Emanuel Nchimbi alipata kura 806, huku Mhaiki akipata kura 55 na katika kata ya Ruhuwiko Nchimbi amepata kura 452 na Mhaiki kura 21.
Katika kata ya Mshangano, Nchimbi alipata kura 905 na Mhaiki kura 83, na katika kata ya Mletele, Nchimbi alipata kura 770 na Mhaiki kura 46, huku katika kata ya Subira Nchimbi akijizolea jumla ya kura 1085 na Mhaiki 109.
Kutoka jimbo la Ilala Dar es Salaam Pamela Chilongola anaripoti, katika Kata ya Kisutu, kura zote zilikuwa 310 huku kukiwa hakuna kura iliyoharibika. Mussa Zungu aliongoza kwa kura 268, Juma Chikoka (5), Sakia Kaika (8), Brandina Mruzya (10), Jafari Komeile kura (19). Kwa upande wa Kata ya Gerezani Juma Chikoka alipata kura mbili, Blandina Mruzya (5), Jafari Komeile (8) na Mussa Zungu (384).
Frederick Katulanda, Mwanza anaripoti kata mbili za wilaya ya Nyamagana, Masha alikuwa akiongoza katika kata mbili za Mirongo na Nyamagana kwa kura 420 dhidi ya 194 ambazo amepata David Mtetemela huku akionekana kumuacha kwa mbali mpinzani wake Joseph kahungwa ambaye amepata kura 51 kwa kata hizo mbili.
Kwa upande wa Geita, Mabina alikuwa alikuwa amekaliwa vibaya katika baadhi ya vituo na kituo cha Nyakabale Donald Max alikuwa akiongoza kwa kura 69 huku Mabina akiwa na kura 10, katika tawi la Kalangala Mjini, Max alikuwa na kura 287 huku Mabina akiwa na 27. Kwa upande wa kata Mirongo diwani yahaya Nyohonge alipata kura 300 huku mpinzani wake Juma Iddi akiambulia kura 41.
Kutoka Moshi Daniel Mjema, anaripoti kuwa taarifa zisizo rasmi zinaeleza kuwa mbunge wa Vunjo aliyemaliza muda wake, Aloyce Kimaro alikuwa ameachwa mbali na mpinzani wake mkuu, Chrispin Meela ambaye ni mwanasheria wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF). Hadi kufikia saa 1:20 usiku, Meela alikuwa akiongoza kwa kura 7,000 huku Kimaro akiwa na kura 1,300 na wagombea wengine, James Kombe na Thomson Moshi wakiachwa mbali.
Kimaro mwenyewe alipoulizwa na Mwananchi alikiri kwamba matokeo hayakuwa mazuri kwake japo mchuano ulikuwa mkali, ilihali Meela akitamba kushinda kwa asilimia 70. Katika jimbo la Moshi Vijijini, taarifa zilizothibitishwa na baadhi ya viongozi wa CCM zilieleza kuwa, Dk.
Cyrill Chami alikuwa akiongoza kwa karibu asilimia 75 ya kura zote. Mpinzani wake pekee, Hansy Mmasi ambaye aliwahi kuwa meneja wa kampuni ya simu ya Vodacom kabla ya kuacha kazi kwa hiyari, alikuwa ameachwa mbali katika matokeo ya awali.
Katika Jimbo la Same Mashariki, Anne Kilango Malecela na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Dk Mathayo David ambaye ni mbunge wa Same Magharibi walikuwa wakiongoza kwa kura nyingi dhidi ya wagombea wengine. Habari zisizo rasmi zilizopatikana Jimbo la Moshi Mjini lililokuwa na wagombea tisa, zilieleza kuwa Justine Salakana aliyewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Rombo (1995-2000) ndiye aliyekuwa akiongoza hadi kufikia saa 1.20 siku.
Mchuano mkali ulikuwa jimbo la Mwanga kati ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe na wakili mashuhuri, Joseph Tadayo, ambao hadi kufikia saa 1:15 usiku walikuwa wakienda sambamba. Jimbo la Rombo, Mbunge anayemaliza muda wake, Basil Mramba alikuwa amewaacha kwa mbali wagombea wenzake huku taarifa katika Jimbo la Hai linaloshikiliwa na Fuya Kimbita zikiwa vigumu kupatikana.
Hata hivyo, upigaji huo wa kura za maoni ulitawaliwa na kasoro nyingi.
KIGAMBONI Elizabeth Suleyman anaripoti kuwa vioja na vitimbi viliibuka katika Kata ya Mbagala Kuu baada ya wanachama zaidi ya 40 kukimbia na karatasi za kupigia kura wakidai kutoridhishwa na mwenendo wa zoezi hilo.
Watu walioshuhudia tukio hilo walidai kuwa waliwaona watu hao wakiingia katika kituo hicho na wakafuata taratibu zote, lakini baadaye wakatokomea na karatasi bila hata kuzitumia kupiga kura. Msimamizi wa kata hiyo hakutaka kulizungumzia suala hilo.
Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya vituo vya jimbo la Kigamboni vililazimika kutumia maboksi, ndoo na mifuko ya rambo kama vifaa vya kuhifadhia kura. Akizungumza na Mwananchi jana, katibu wsa CCM Kata ya Mbagala Kuu, Maji Mohammed Majid alisema tawi lao halikupewa kifaa chochote cha kuhifadhia kura zaidi ya karatasi za kupigia kura.
"Kwa kweli baada ya kuona hakuna masanduku ya kupigia kura tuliamua kutumia maboksi na ndoo, baada ya kupewa utaratibu wa kupiga kura tuliletewa maboksi na katibu kata," alisema.
KINONDONI Hussein Issa na Raymond Kaminyoge wanaripoti kuwa madiwani wa Kata ya Kimara, Mahmoud Mringo na Mburahati, Nuru Chaurembo na Ubungo William Massanja walikamatwa juzi usiku na Takukuru na kuhojiwa na wakaachiwa jana. Kwa mujibu wa Takukuru, watu hao walikamatwa juzi usiku wakidaiwa kugawa vitu vinavyosadikiwa kuwa ni vya rushwa.
Sambamba na hilo taasisi hiyo ilikamata kadi za CCm zaidi ya 50 zinazosadikiwa kuwa ni za kughushi na wakati wa kupiga kura wahusika walikamatwa na wanaendelea kuhojiwa.
TANGA, Maingwa Mohamedi anaripoti kuwa wajumbe wa baraza kuu la vijana mkoani Tanga wametishia kutomtambua mshindi wa nafasi ya ubunge kupitia jumuiya hiyo, Mboni Mhita kwa madai alibebwa na vigogo wa chama na jumuiya hiyo taifa.
Katika mkutano wao na waandishi wa habari uliofanyika jana, baadhi ya wajumbe wa mkutano huo walisema uchaguzi huo haukuwa huru na haki kutokana na kutawaliwa na rushwa pamoja na vitisho kwa wapigakura.
Wajumbe hao ambao hawakutaka kuandikwa majina yao gazetini kwa ajili ya usalama wao, walisema, sababu zinazowafanya kupinga uchaguzi huo ni mgombea aliyeshinda kubebwa na vigogo hao.
Timu hiyo ya wajumbe imeulalamikia ushindi wa Mboni kwamba haukuwa halali na wanatarajia malalamiko hayo kuyafikisha ngazi za juu zaidi kwa ajili ya ufumbuzi.
Hoja yao kuu ni kwamba mshindi si mkazi wa Tanga na hafahamiki na kwamba, asingeweza kupata ushindi wa kishindo. Al;ipoulizwa kuhusu suala hilo, katibu wa vijana mkoani Tanga, Acheni Maulidi alisema hayo ni mambo ya kawaida na yapo kwa kila sehemu yenye ushindani.
Acheni, ambaye naye anatuhumiwa kumbeba mshindi huyo, alisema uchaguzi ulikuwa huru na hakuna mjumbe aliyepewa vitisho wala kushinikizwa na kiongozi yeyote na kwamba hizo ni hasira za kushindwa tu.
Mboni aliibuka mshindi kwa kupata kura 33 na kuwashinda Miriam Shemzigwa (kura 6), Amina Kingazi (5), Evelene Kweka (3) huku Esther Mambali na Hidaya Semtumbi ambao hawakuambulia kitu.
UKONGA Geofrey Nyang'oro anaripoti kuwa kura za maoni katika jimbo la Ukongo jijini Dar es Salaama jana zilitawaliwa na vurugu katika baadhi ya vituo kutokana na kuwepo kwa wanachama wanaodaiwa kuwa mamluki.
Wanachama hao walioibukia kituo cha kupigia kura cha tawi la Gongolamboto wanadaiwa ni wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha KImataifa cha Kampala (KIU) kilicho eneo hilo. Watu hao waliwasili majira ya saa 4:00 asubuhi lakini hekaheka ziliibuka saa 7:00 mchana baada ya baadhi ya wanachama kuwakataa.
Sababu za kukataliwa ilikuwa ni kutofahamika kwao kwa wanachama wengi licha ya majina yao kuwemo kwenye orodha ya wapiga kura kutoka kwa wajumbe wa mashiana wa CCM.
Katika kituo cha Gongolamboto, diwani aliyemaliza muda wake, Jerry Slaa alijikuta mikononi mwa Takukuru baada ya kusimamisha gari la maofisa hao lililokuwa limembeba mmoja wa wanachama waliodhaniwa kuwa ni mamluki ambaye alikamatwa eneo la Gongolamboto saa 8:00 na kumpeleka katika kituo kidogo cha polisi.
Kwenye kituo cha Mazizini, zaidi ya wanachama 30 walikataliwa kupiga kura baada ya kukutwa na kadi bandia za CCM. Kadi hizo zilibainika baada ya kufanyika uhakiki wa majina ya wapiga kura kabla ya kuanza mchakato wa kura za maoni.
Mmoja wa wagombea wa nafasi ya ubunge wa jimbo la Ukonga, Godwin Barongo alielezea mchakato huo kuwa si mazuri kutokana na mpangilio kuwa mbovu. Barongo alisema kura za maoni ni nzuri, lakini utaratibu si mzuri na unaweza kuharibu mwendendo mzima wa upigaji kura.
"Hukukuwa na sababu kwa kiongozi kutojua wapiga kura wake, hii hali ya watu kuja leo na kuelezwa eti majina yao hayamo kwenye orodha wakati wana kadi ni ishara tosha kuwa wahusika hawajui kazi yao," alisema Barongo.
TEMEKE Zaina Malongo anaripoti kutoka Temeke kuwa dosari nyingi zilitawala mchakato huo ikiwa ni pamoja na baadhi ya vituo kuchelewa kuanza kazi kwa mujibu wa ratiba na utata wa majina katika madaftari ya orodha ya wanachama.
Makosa hayo ambayo yalijirudia rudia kwa kila kata, yalisababisha wanachama wengi wakose fursa ya kupigakura kutokana na kile kilichoelezwa majina yao hayakuwepo katika daftari.
Hali hiyo ilisababisha vurugu katika baadhi ya vituo hasa kata ya Miburani ambako tawi la Wailes lilikumbwa na vurugu kubwa, Mtongani, Sandari, Azimio na Duce, huku vurugu nyingine zikitokana na wapambe wa wagombea kutaka kufundisha wanachama jinsi ya kupiga kura.
MBEYA Brandy Nelson anaripoti kuwa tatizo la kukosekana kwa majina ya baadhi ya wanachama kwenye orodha ya wapigakura lilitanda kwenye maeneo mengi licha ya wanachama kuwa na kadi zao. Dosari nyingine iliyojitokeza ni baadhi ya wanachama kutoa malalamiko kwa kupiga kelele baada ya kubaini kuwa mke wa mgombea wa udiwani ni mmoja wa watu waliokuwa wakihakiki kadi na kuwalipisha ada wanachma ambao walikuwa hawajalipia kadi zao.
Wanachama hao walibaini udhaifu huo katika kituo cha Benki Kata ya Ruanda ambako mtafaruku mkubwa uliibuka na kusababisha msimamizi msaidizi wa kituo hicho kuomba msaada wa maelekezo kwa viongozi wa CCM ngazi ya Wilaya.
Matukio mengine ya baadhi ya wanachama kufika vituoni na kutoona majina yao huku wakiwa na kadi yalijitokeza maeneo ya Kata ya Forest, Makuguru na Ruanda, ambako sehemu nyingine wanachama waliruhusiwa kupigakura na wengine walizuiliwa kupiga.
HANDENI
Hussein Semdoe anaripoti kuwa mkurugenzi wa uchaguzi wa CCM, Kata ya Vibaoni wilayani Handeni na katibu wa Jumuiya ya Vijana kwenye kata hiyo, wamenaswa na Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa tuhuma za kugawa karatasi za kupigiakura kabla ya uchaguzi.
Viongozi hao walinaswa jana asubuhi wakati waliposhitukiwa na Takukuru wakitoa nakala za karatasi za kupigiakura kwenye duka moja la vifaa vya ofisini lililo Mtaa wa Bomani mjini hapa.
Katibu wa CCM wilayani humo, David Mkude aliwataja watuhumiwa hao ambao ni Anna Mwagilo ambaye ni mkurugenzi wa uchaguzi wa kata hiyo, Ibrahim Manyuti. Mkuu wa Takukuru wilayani hapa, Sultan Ng'aladzi alikiri kuwa viongozi hao wanashikiliwa na kwamba bado wanaendelea kuhojiwa kuhusu tukio hilo.
MOROGORO
Venance George anaripoti kutoka Mvomero kuwa kukosekana majina ya wapigajikura za imeikumba pia jimbo la Mvomero baada ya majina ya baadhi ya wanachama kutokuwemo katika taftari la wapigakura, hali iliyosababisha wanachama hao kutopigakura, licha ya katibu Mkuu wa CCM Yusuph Makamba kuruhusu wapigekura.
Katika baadhi ya vituo, vikiwemo vya Dakawa, Bunduki, Maguruwe na Madizini kulikuwa na msululu mkubwa wa wapiga kura, huku baadhi yao wakilalamika baada ya kuambiwa majina yao hayamo kwenye daftari la wapigakura.
Jumla ya wapigakura 860 waliandikishwa kituo cha Dakawa na walitakiwa kupiga kura, lakini idadi iliongezeka baada ya wapiga kura ambao hawakusajiliwa katika daftari hilo kujitokeza.
Imedaiwa na baadhi ya wanachama wa CCM katika kata hiyo kuwa usiku wa kuamkia leo, baadhi ya wapambe wa wapigakura walipita nyumba hadi nyumba wakitoa kadi za uanachama tukio ambalo limejitokeza pia katika kata ya Bunduki.
Mmoja wa wanachama hao, Elia Joseph, mkazi wa kitongoji cha Mtakuja, alisema alikwenda kujiandikisha katika daftari hilo, lakini alishindwa kutokana na kutokuwa na kitambulisho na aliporudi kwa mara ya pili akiwa na kitambulisho hicho, alijibiwa kuwa tayari ameshasajiliwa.
Leo nakuja kupigakura naambiwa jina lako haliko kwenye daftari, nimechoka kufutilia nazungushwa kama mtoto mdogo, kwa kuwa hata nisipopiga kura napata kula mimi au watakula wao, alisema mwanachama huyo. Hata hivyo, mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mvomero, Poroleti Mgema alisema yuko katika zoezi la kutembelea vituo ambako kasoro zimejitokeza ili kutoa maelekezo na kwamba baadaye atatoa taarifa kamili.
SONGEA Joyce Joliga, anaripoti uchaguzi wa jimbo la Songea Mjini pia umekumbwa na mauzauza ya matumizi ya mifuko ya rambo kuhifadhia kura baada ya kukosekana vifaa huku baadhi ya vituo vikichelewa kufunguliwa kwa zaidi ya saa nne hali iliyosababisha usumbufu kwa wananchama.
Mwananchi katika uchunguzi wake kwenye vituo vya Matogoro Kati, Chemchem, Ndilima, Makambi pamoja na kata ya Mjini umebaini kuwepo na matatizo mbalimbali likiwemo la majina na namba za wagombea wa udiwani kujirudia mara mbili hali ambayo ilisababisha kusimama kwa muda kwa zoezi hilo.
Mwenyekiti wa Kata ya Matogoro Kati, Hamad Mwamba aliiambia Mwananchi kuwa kulikuwepo na udhaifu huo, ikiwa ni pamoja na ucheleweshaji wa karatasi za wagombea pamoja na masanduku yake hali iliyowalazimu wanunue mifuko ya rambo kwa ajili ya kuhifadhia kura zilizopigwa.
Mimi pamoja na kamati ya siasa na mawakala tumekaa na kukubaliana tutumie mifuko ya rambo kwani hata hizo karatasi zimefika saa 3:30 asubuhi, ili kuokoa muda tumeamua kupigakura badala ya kuendelea kusubiri masanduku kwani muda unaenda, alisema.
Hata hivyo, uchunguzi huo zaidi wa gazeti hili umeonyesha wabunge wanaotetea nafasi zao katika majimbo ya Songea Mjini, Peramiho pamoja na Namtumbo, wanaongoza kwa kura nyingi. SHINYANGA Zulfa Mfinanga, anaripoti kutoka Shinyanga kuwa zoezi hilo limezua vuguvugu pamoja na mgomo baridi kutokana na baadhi ya wapigakura kukosa majina yao katika vituo vya kupigia kura.
Wilayani Bariadi katika kituo cha Sima, wapigakura waligoma kwa takribani saa nne kwa kile walichodai kukosekana kwa majina ya baadhi ya wapigakura ambako mgomo huo ulimalizika saa sita mchana na baadaye zoezi la kuendelea tena.
Katika kituo cha Majengo kilichopo mjini hapo, wapigakura walianza vurugu ambazo zilinyamazishwa na askari polisi na zoezi hilo kuendelea chini ya ulinzi mkali. Katibu wa CCM wilayani ya Kahama, hakuweza kupatikana mara moja kuelezea tukio hilo, lakini kiongozi mmoja wa CCM wilayani humo alikiri kutokea kwa vurugu hizo na kusema zilitulizwa na askari.
SEGEREA Pamela Chilongola anaripoti kuwa mmoja wa wapambe wa mgombea amepigwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni wa mgombea mwingine baada ya kumkuta akitoa pesa kwa wananchi waliofika kupiga kura. Hayo yalitokea jana katika Kata ya Kipawa, tawi la Mogo mnamo saa nne ambako mpambe huyo aliyetambulika kwa jina moja la Adia, alikutwa nyuma ya ofisi ya kata akiwaita wanachama mmoja baada ya mwingine na kuwapa fedha ili wafanye upendeleo.
Mpambe huyo alipokutwa alipewa kipigo na kufukuzwa katika eneo la hilo. Wakati huo huo, wanachama wa kata ya Segerea tawi la Misewe shina la sita, 38 hadi 42 majina yao hayakuonekana katika daftari la wapiga kura na kusababisha mtafaruku baina ya mjumbe na katibu wa kata.
Mjumbe wa kata hiyo alisema orodha ya majina aliyakabidhi kwa Katibu Hamis Tazaro lakini alikanusha kuwa yeye hakupata hayo majina. Naye katibu kata wa Segerea Eliminata Madaha, alipotaka ufafanuzi kwa Katibu Msaidizi wa wilaya alimwambia kuwa majina alishayafikisha wayaangaie vizuri kwenye kata yao.
SERENGETI Anthony Mayunga wa Serengeti anaripoti kuwa mkazi wa kijiji cha Kyambahi wilayani Serengeti, Chacha Mwita (29) amelazwa Hospitali Teule ya Nyerere (DDH) baada ya kupigwa risasi mguuni. Tukio hilo ambalo limefanya kura za maoni za CCM kuingia dosari kubwa baada ya Chacha kushambuliwa saa 3:00 usiku na kujeruhiwa mguu wa kulia wakati akilinda wagombea wasitoe rushwa usiku.
Akizungumza na gazeti hili la Mwananchi hospitalini hapo alikolazwa, Chacha alisema usiku huo akiwa analinda wagombea hao, ghafla lilifika gari mmoja ambalo lilikuwa na watu ambao hakuwatambua na kupita, lakini gari la pili lilipofika wakati wakitaka kuwatambua alistukia akipigwa risasi.
Hata hivyo, tofauti na tukio hilo zoezi la upigaji wa kura kwa baadhi ya maeneo hadi majira ya saa 6:30 mchana vituo vilikuwa havijafunguliwa kutokana na kuchelewa kwa vifaa.
Mgombea udiwani kata ya Manchira, Marko Shaweshi alilalamikia mchezo huo na kudai ulikuwa ni wa makusudi na wenye lengo la kutaka kumsaidia mgombea mmoja.