Upinzani una nafasi nyembamba kushinda Mbeya Vijijini Jumapili
2009-01-21 10:48:36
Na Theodatus Muchunguzi
Mwelekeo mzima wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Mbeya Vijijini, mkoani Mbeya sasa ni dhahiri kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kina nafasi kubwa na kitaibuka na ushindi katika uchaguzi huo utakaofanyika Jumapili ya wiki hii Januari 25.
Katika uchaguzi huo ambao CCM kimemsimamisha Mchungaji Jackson Mwanjale; Chama Cha Wananchi (CUF) kimemsimamisha Daudi mponzi wakati Chama Cha Sauti ya Umma (Sau) kimemsimamisha Subira Mwakipiki, Mchungaji Mwanjale anapewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi.
Dalili za ushindi wa Mchungaji Mwanjale na CCM zinatokana na mwenendo mzima wa kampeni hizo zilizoanza Januari 4, ambazo kwa kiasi kikubwa zimebainisha kuwa CCM na mgombea wake wamefanya mikutano mingi ya kuomba kura.
Ni jambo lisilo na ubishi kuwa kampeni za vyama vya CUF na Sau zimekuwa ni za kusuasua kwa kipindi chote.
Hata hivyo, CCM kimepata bahati ya kukosa upinzani kutokana na kutoshiriki kwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho aliyekuwa mgombea wake, Sambwee Shitambala, kumeenguliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika orodha ya wagombea wakati wa uteuzi kwa maelezo kuwa alikiuka sheria ya viapo.
Shitambala ambaye kugombea kwake kulikuwa kumeshaanza kuonyesha dalili kuwa kungesababisha ushindani mkali na kuzichangamsha kampeni hizo, baada ya kuenguliwa kampeni hizo zikadorora na CCM kukosa upinzani.
Ilitarajiwa kuwa wanasiasa machachari wa Chadema wangekwenda Mbeya Vijijini kuchuana na timu ya kampeni ya CCM inayowajumuisha vijana wa chama hicho pamoja na wazee hususan mwanasiasa mkongwe ambaye ana rekodi ya kukibeba chama tawala katika uchaguzi mdogo, John Samwel Malecela maarufu kwa jina la ``Tingatinga``.
Wanasiasa kama Mbunge wa Karatu na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrood Slaa; Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe; Mkurugenzi wa Vijana, John Mnyika; Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe; Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu, ni miongoni mwa wanasiasa hao ambao wangeongoza kampeni hizo na kuzungumzia mambo mbalimbali mazito ya kitaifa.
Ingawa hakuna utafiti rasmi uliokwishafanywa kubainisha nguvu za vyama vya upinzani nchini, lakini mwenendo wa hali ya kisiasa nchini hivi sasa unaonyesha kuwa Chadema kinaongoza kwa kuungwa mkono Tanzania bara wakati kwa upande wa Visiwani kama kawaida CUF kinaendelea kuongoza.
Chadema kimepanda chati kutokana na uwezo wa kuibua ajenda mbalimbali za kuikosoa serikali na ujasiri wa kuzieleza kwa umma baada ya kuzifanyia utafiti.
Miongoni mwa hoja hizo ni pamoja na kashfa kadhaa za ufisadi.
Kwa upande wake, CUF kimeendelea kuwa na mvuto upande wa Visiwani pengine kutokana na chama hicho kujikita zaidi katika harakati za kushindana na CCM kutaka kushika dola ya Zanzibar. Kwa upande wa Tanzania bara hivi sasa CUF hakina hata mbunge mmoja wa jimbo.
Udhaifu huo umekifanya chama hicho kukosa timu imara ya kukitangaza kwa ``kushikia bango`` ajendamuhimu za kitaifa ukimwondoa mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba na Naibu Katibu Mkuu, Wilfred Lwakatare.
NCCR-Mageuzi kwa sasa hakina hata mbunge mmoja na hakijaibua mambo mazito ya kuikosoa serikali hasa kashfa za ufisadi na utendaji mbovu kiasi cha kuwavuta watu wengi zaidi.
Chama hicho kilipata umaarufu mkubwa kuanzia mwaka 1995 baada ya Augustino Mrema kujiunga nacho akitokea CCM.
Tanzania Labour (TLP) nacho kimepoteza nguvu kilichokuwa nazo kuanzia mwaka 1999 baada ya kumpokea Mrema kutokea NCCR-Mageuzi.
Kujiondoa ama kuondolewa kwa timu ya wanachama na viongozi waliohamia katika chama hicho wakiwa na Mrema, kumekipunguzia nguvu kiasi kwamba hivi sasa hakina hata mbunge mmoja.
Kwa maana hiyo, Chadema kinazidi kuwa na nguvu kila kukicha.
Matokeo yaliyokipa ushindi katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa jimbo la Tarime na wa udiwani kata ya Tarime mkoani Mara Oktoba, mwaka jana, ni ushahidi tosha kuwa kina nguvu kubwa hasa kutokana na kuchuana na CCM pamoja na vyama vingine vya upinzani vya NCCR-Mageuzi na Democratic (DP).
Kipimo rahisi cha kujua umaarufu wa chama cha siasa hapa nchini ni kuitisha mkutano wa hadhara na kuona idadi ya ya watu watakaojitokeza.
Kipimo kizuri ni kuitisha mkutano katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam.
Hivi sasa chama cha upinzani kinachoweza kuitisha mkutanokatika viwanja hivyo na kuvijaza ni Chadem na kwa viwanja vya Zanzibar ni CUF.
Kutokana na kupanda chati kwa Chadema ndiyo maana wananchi kadhaa walikuwa na shaukukubwa ya kufuatilia kwa karibu kampeni za Mbeya Vijijini kabla mgombea wa chama hicho kuenguliwa.
Jambo linaloshangaza ni kuwasikia baadhi ya viongozi wa upinzani wakielekeza mashambulizi yao kwa Chadema wakati wa kampeni zinazoendelea Mbeya Vijijini badala ya kuyaelekeza kwa mshindani wao CCM.
Hatua hiyo inaonekana wazi kudhihirisha kuwa ushirikiano wa vyama vinne vya TLP, Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi umekufa rasmi.
Sababu kubwa ya viongozi wa upinzani walioko katika majukwaa ya kampeni jimboni Mbeya Vijijini kukishambulia Chadema ni kubaini kuwa CUF walichokwenda kukipigia debe hakina ubavu wa kuikabili CCM katika uchaguzi huo.
Kauli zinazotolewa kuwa Chadema kimekiukamakubaliano ya kwapinzani kushirikiana hayana ukweli kwa kuwa katika uchaguzi wa Tarime hakuna chama kilichokiunga mkono licha ya kujulikana wazi kuwa ndicho kilichokuwa kinaungwa mkono na kukubalika kwa wananchi wengi wa Tarime.
Madai kuwa CUF ilikiunga mkono Chadema Tarime siyo ya kweli.
Hakuna agizo au kauli yoyote iliyotolewa na viongozi wa Taifa wa CUF kuwaeleza viongozi wa Mkoa wa Mara na Wilaya ya Tarime waiunge mkono Chadema, isipokuwa viongozi wachache wa mkoa na wilaya kama Mwenyekiti wa CUF Mkoa, Mustafa Wandwi walioonyesha nia ya kuiunga mkono Chadema kama watu binafsi, ambao hawakupata maelekezo ya viongozi wa taifa.
Kama Profesa Lipumba na timu ya uongozi wa taifa ingetoa tamko na vile vile kufunga safari ya kwenda Tarime na kusimama majukwaani kuwanadi Charles Mwera,aliyekuwa mgombea ubunge na mgombea udiwani wa tarime Mjini, John Heche, hapo tusingesita kuwaita Chadema kuwa ni wasaliti wa upinzani.
Katika kuonyesha kusikitishwa na uamuzi wa NEC kumwondoa Shitambala kugombea Mbeya vijijini kwa tiketi ya Chadema, kuna mtu mmoja aliyediriki kusema kwa utani kuwa ``wananchi wa Mbeya Vijijini watakosa uhondo wa kuiona Chopper na Mbowe`` akimaanisha kuwa hawataiona helkopta na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Licha ya watu kadhaa kusikitishwa na kuondolewa jina la mgombea wa Chadema, lakini wapo wanaounga mkono uamuzi huo wa NEC baada ya vyama vya CCM na CUF kuweka pingamizi.
Kwa mfano, Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema, alisema mwishoni mwa wiki katika mkutano wa kampeni wa CUF wilayaniMbeya kuwa kuwekewa pingamizi kwa Chadema, Sambwee Shitambala katika uchaguzi huo na vyama vya upinzani siyo kosa kwa sababu alikiuka taratibu na sheria za uchaguzi.
Katika mkutano huo wa hadhara wa kampeni uliofanyika
katika mji mdogo wa Mbalizi kumnadi mgombea wa CUF ,Daudi Mponzi , Mrema alisema sio kosa mgombea kuwekewa pingamizi anapokiuka taratibu za kisheria zilizowekwa na NEC..
Mrema alikwenda mbali zaidi kwa kuwataka wananchi kupuuza propaganda za viongozi wa Chadema wanaodai kuwa vipo vyama vya siasa ambavyo vinashirikiana na CCM kuhujumu demokrasia nchini na kukishutumu kuwa kimeshindwa kutimiza masharti na kwamba hiyo siyo mara ya kwanza kwa chama hicho kukiuka makubaliano ya ushirikiano.
Lakini Mrema alilitumia jukwaa hilo kwa kukisifu CUF kuwa ni chama cha kiungwana kwa maelezo kuwa pamoja na kusalitiwa na Chadema katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Tunduru ilipofika uchaguzi wa Tarime walikiunga mkono Chadema.
Mrema alisema chama chake kimeamua kukiunga mkono CUF katika uchaguzi wa Mbeya Vijijini kwa sababu chama hicho kiko mstari wa mbele kupigania demokrasia nchini.
Kwa upande , Mwenyekiti wa Taifa wa PPT Maendeleo, Peter Mziray, akihutubia katika mkutano huo wa kuipigia debe CUF, aliwataka viongozi wa Chadema kutoa tamko haraka la kuwaunga mkono CUF katika uchaguzi huo.
Katika kampeni hizo, zimetolewa kauli nyingi za kukishutumu Chadema kwa kutokiunga mkono CUF.
Licha ya vyama vingine vinavyokiunga mkono CUF nacho kimetumia muda mwingi wa kampeni kuelezea jinsi Chadema kilivyokisaliti kwa kukaidi kukiunga mkono kutokana na kukubalika zaidi katika jimbo hilo kuliko Chadema.
Kimsingi, kambi ya upinzani imeshiriki katika uchaguzi wa Mbeya Vijijini bila kuwa na ajenda za maana za kuwaeleza wapiga kura na wananchi wa Mbeya Vijini kwa ujumla kuhusu mambo yanayowapa kero na namna ya kuyashughulikia.
Badala yake wametumia kampeni hizo kushambuliana wenyewe hasa Chadema na kusahau kuwa mpinzani wao mkuu ni CCM.
Mwenendo mzima wa kampeni za upinzani unaondoa matumaini ya kushinda katika uchaguzi wa Jumapili na kutoa nafasi kubwa kwa CCM kulitetea jimbo hilo lililoachwa wazi na aliyekuwa mjumbe wake, marehemu Richard Said Nyaulawa, Novemba mwaka jana.
SOURCE: Nipashe