Chifu ataka CCM isichaguliwe Mbeya
Na Brandy Nelson, Mbeya
CHIFU mkuu wa kabila la Wamalila, lililo katika tarafa ya Isangati wilayani Mbeya Vijijini, Golian Mpoli, 90, amewataka wananchi wake kutokichagua chama
ambacho kinawanyima maendeleo na badala yake wamsubiri mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Sambwee Shitambala, katika uchaguzi wa mwaka 2010.
Mgombea huyo alienguliwa kwenye kinyang'anyiro cha kiti cha ubunge cha jimbo la Mbeya Vijijini baada ya kugundulika kwa kasoro kwenye kiapo chake. Vyama vya CCM na CUF vilibaini kasoro hizo na kuweka pingamizi ambalo lilikubaliwa na Tume ya Uchaguzi.
Lakini chifu huyo wa kabila la Wamalila anaona kuwa bado kuna haja ya kumsubiri mgombea huyo katika uchaguzi mkuu ujao kwa kuwa hawana la kufanya kwa sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Chifu Mpoli, akiwa na mkalimani kutokana na kutojua vizuri lugha ya Kiswahili, alisema kuwa toka uhuru wamekuwa wakitawaliwa na viongozi wa CCM, lakini hakuna maendeleo yoyote ambayo chama hicho kimewapa zaidi ya kuendelea kuwanyonya.
Alipoulizwa kuwa ni kwanini anamtaka Sambwee Shitambala kuwa mbunge wa jimbo la Mbeya Vijijini wakati hajawahi hata kuwaongoza na pia si mzaliwa wa tarafa hiyo ya Isangati, Chifu Mpoli alisema kuwa kutokana na jinsi alivyomuona na kutafakari anaamini anaweza kuwasaidia wananchi wake.
"Tangu afariki mbunge wetu Edward Shiwa aliyetuongoza kipindi cha mwaka 1995 hadi 2000, tulikuwa hatuna shida yoyote kwa kuwa alikuwa anatusikiliza na kutatua shida zetu na alianza harakati za kuleta umeme. Alifikia hatua ya kuwekwa nguzo na bahati mbaya akafariki dunia kabla ya kulimalizia," alisema.
Alisema tangu alipoondoka mbunge huyo bado nguzo hizo zimelazwa chini na
nyingine zimechimbiwa, lakini hakuna maendeleo yoyote ya suala la kupata umeme kwa wananchi wa tarafa hiyo.
Chifu huyo alisema kuwa Mbunge Shiwa ndiye aliwaletea wazo la kujenga Shule ya Sekondari ya Ilembo na kwamba baada ya hapo tangu mwaka juzi wamekuwa wakichangishwa fedha kila mara kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, lakini hakuna kinachoendelea.
"Baada ya kuondoka Mbunge Shiwa, kuna wabunge wa CCM walikuwepo lakini hakuna walilotufanyia kama huyu wa mwisho... pamoja na kuwa mimi ni chifu mkuu nilikuwa simfahamu... nilikuwa nasikia jina tu mpaka alipofariki dunia. Hivyo kwa niaba ya machifu wenzangu na wananchi, hatuitaki CCM... tunamsubiria Sambwee Shitambala mwaka ujao, ndiyo maana nimeamu kuja huku kuwaeleza," alisema.
Alipoulizwa sababu za kutoitaka CCM, chifu huyo alijibu kuwa viongozi wake wanawanyonya wananchi na wamekuwa na matatizo mengi katika eneo hilo lakini viongozi wa CCM wanashindwa kutatua na kwamba tayari kikao cha machifu kimefanyika katika kujadili suala hilo na kwamba wamekubalina wamsubiri Shitambala mwaka 2010 ili aweze kuwasaidia katika kusukuma gurudumu la maendeleo.
Wakiongea na Mwananchi, baadhi ya wananchi wa kata ya Ilembo walisema kuwa kitendo cha kuondolewa mgombea wa Chadema ni sawa na kunyang`anywa tonge la ugali mdomoni kwa kuwa hali hiyo imewasikitisha sana.
Walisema kuwa kati ya wabunge watatu waliowahi kuongoza jimbo la Mbeya Vijijini, ni Shiwa (CCM) ndiye aliyeweza kuwaletea maendeleo hivyo bado anahitaji mabadiliko na kwamba msimamo wao ni kuchagua chama pinzani.
"Kama Mbunge Yete Mwaliyego ambaye alichaguliwa mwaka 2000 huyo ndiyo hatusemi kwani alikuwa anaomba kura kwa mabavu na alifikia hata kutuambia kuwa mnichague msinichague mimi ni mbunge wenu tu na alipochaguliwa hakuonekana tena hadi naye alipofariki dunia," alisema Sipiti Solomoni wa Kijiji cha Ilembo.
Alisema kuwa wao ni wanachama wa CCM na wana kadi za CCM, lakini dhamira yao ilikuwa ni kumchagua mgombea wa Chadema kwa kuwa ndiye alikuwa chaguo lao hivyo kwa sasa hawana la kufanya.
"Kweli suala la mgombea wa Chaema kuondolewa limetuumiza sana tulikuwa tunampenda na bado tunampenda na tunamuhitaji awe mbunge wetu kwani ndiye tuliyemdhania kuwa angeleta mabadiliko katika jimbo hili... labda kama anaweza kupita huyo wa CCM wakimchagua kwani anasema kwa yeye katumwa na Mungu aje kuwa mbunge," alisema.
Walisema kuwa wanahitaji mabadiliko kwani CCM imekuwa ikiwahaidi lakini hakuna mafanikio yoyote na kwamba wamechoka na chama hicho ambcho wamekuwa wasikilza kiula mara sera zake lakini hakuna zinazotekelezwa katika eneo hilo.
"Msimamo wetu ni ule ule wa kutaka mbunge kutoka katika chama cha upinzani. CUF wamekuja hapa tumewasikiliza sera zao na tunawasubiri kuona sera zao ni nini kama tunaona nao hawaturidhishi, basi tutajua la kufanya," alisema mmoja wao.
Wananchi hao ambao walikuta wamesimama katika vikundi vikundi maeneo ya klabu cha pombe na sokoni katika kijiji hicho cha Ilembo ambacho rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi alizindua kampeni za CCM.
Walipohojiwa kama wangeenda kwenye mkutano huo wa uzinduzi, walisema kuwa wangeenda kwa ajili kumfahamu rais huyo mstaafu kwa kuwa hawajawahi kumuona.
Leo ni leo Mbeya Vijijini
Habari Zinazoshabihiana
CCM: CHADEMA msijisumbue Mbeya Vijijini 09.12.2008 [Soma]
Ajali yaua 4 papo hapo 05.07.2006 [Soma]
Atangaza kumrithi Nyaulawa jimboni 15.11.2008 [Soma]
*Askari wajipanga, kuimarisha ulinzi
*Vigogo, CCM, CUF wajazana Mbeya
*Watu 126,780 kupiga kura
Rashid Mkwinda na Peter Twite, Mbeya
UCHAGUZI mdogo wa Jimbo la Mbeya Vijijini unafanyika leo ambapo jana wagombea na wafuasi wa vyama vinavyoshiriki uchaguziu huo walifanya kampeni za lala salama katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.
Majira Jumapili ilishuhudia askari wakiwa wanavinjari maeneo kadhaa wakiwa kwenye magari ya landrover 110 huku yakiwa yamewasha taa kuashiria kwamba hali ya ulinzi itaimarishwa wakati wa uchaguzi utakapokuwa unafanyika leo.
Msimamizi wa uchaguzo huo Bibi Juliana Malange alisema jana kwamba kuna jumla ya vituo 395 vya kupigia kura na jumla ya wapiga kura 126,780 kutoka kata 17 wanatarajiwa kupiga kura leo katika uchaguzi ambao hata hivyo hauna ushindani mkubwa kutokana na mgombea wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuenguliwa wiki chache zilizopita.
Ili kujiweka sawa katika kampeni za mwisho jana, Chama cha Wananchi (CUF) kilialika baadhi ya wabunge kutoka Tanzania Visiwani huku Chama cha Mapinduzi (CCM) kikiwa kinapigiwa debe na wabunge wote wa chama hicho mkoani Mbeya ambao jana walikiuwa wametawanyika katika maeneo mbalimbali kuhakikisha chama chao kinaibuka kidedea kwenye uchaguzi huo.
Wagombea watakaopigiwa kura leo ni Mchungaji Luckson Mwanjale wa CCM ambaye kwa mujibu wa taaluma yake kama alivyojieleza katika kampeni za uchaguzi jimboni humo ana uzoefu na stashahada yaufundi ambaye hadi anagombea kiti hicho alikuwa ni Katibu mkuu wa Kanisa la Uinjilisti lenye makao yake makuu mkoani Mbeya.
Mgombea mwingine ni Bw. Daud Mponzi mwenye shahada ya uhandisi ambaye kwa mtazamo wa maelezo yake katika kampeni za uchaguzi atatumia utaalamu wake na uzoefu wake wazaidi ya miaka 30 akiwa mtumishi wa Shirika la Posta na simu kuhamasisha na kuboresha mahitaji muhimu ya wakazi wa jimbo hilo ambao wanahitaji maendeleo ya kisiasa kiuchumi na kijamii.
Mwingine ni Mgombea pekee mwanamke katika kinyang'anyiro hicho kutoka chama cha Sauti ya Umma SAU, Bibi Subi Mwakapiki ambaye kwa mtazamo wake kama mwanamke amejitoa mhanga katikati ya kundi la wanaume wenye mbinu mbalimbali za kampeni ambaye kwa mtazamo wake atatumia fursa yeye kama mjasiriamali kuwainua akina mama wenzie ambao anaamini wako nyuma kimaendeleo kutokana na mfumo dume uliopo katika wakati huu ambao kila mtu anahitaji maendeleo.
Aidha kwa kipindi kisichozidi miaka mitatu jimbo hilo lilianza kuonekana kuwepo katika matumaini kwa juhudi binafsi za aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo marehemu Richard Nyaulawa ambaye kwa hatua za awali aliweka mikakati ya kuanzisha kiwanda cha mbolea, Pembejeo za kilimo Company Limited.
Hata kabla ya kuhitimisha ndoto yake kwa wapiga kura wa jimbo lake Mwenyezi Mungu alimuita kwake huku akiacha fikra zake zikielea hewani ambapo kwa sasa wamejitokeza wagombea kwa tiketi ya vyama vitatu ambao kila mmoja anaangalia ni yupi ambaye anaweza kulivusha jahazi hili ngambo ya mto.
Chanzo: MAJIRA
CCM, CUF vitani Mbeya leo
na Christopher Nyenyembe, Mbeya
UCHAGUZI mdogo wa ubunge katika Jimbo la Mbeya Vijijini unafanyika leo ukivishirikisha vyama vitatu, Sauti ya Umma (SAU), Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), huku upinzani mkubwa ukitarajiwa kuwa baina ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Wananchi (CUF).
Uchaguzi huo unafanyika leo baada ya kampeni kuhitimishwa jana huku zikikosa msisimko uliotarajiwa baada ya mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maaendeleo (CHADEMA) kuenguliwa kwenye kinyanganyiro hicho, baada ya mgombea wake, Sambwee Shitambala kuwekewa pingamizi na vyama vya CCM na CUF.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 CCM iliibuka na ushindi kwa kupata asilimia 80 ya kura zote zilizopigwa.
Ni ukweli usiopingika kuenguliwa kwa mgombea wa CHADEMA, Sambwee Shitambala, kumeonyesha wazi kuipa mwanya CCM kuibuka na ushindi.
Katika uchaguzi huo, jumla ya wapiga kura 127,780 ikiwa ni ongezeko la wapiga kura 10,539 ikilinganishwa na wananchi 117,241 waliopiga katika uchaguzi mwaka 2005.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, Juliana Malange, wapiga kura 127,780 wanatoka kata 17 za jimbo hilo lenye vijiji 89 huku vituo 395 vimetengwa kwa ajili ya kupigia kura.
Ongezeko la wapiga kura zaidi ya 10,000 ndani ya kipindi cha miaka mitatu tangu uchaguzi mkuu ulipofanyika mwaka 2005 kunatia shaka na tayari yapo malalamiko kadhaa kutoka kwa viongozi wa vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo.
Kasoro zilizoainishwa na kulalamikiwa zinahusu Daftari la Kudumu la Wapiga Kura baadhi ya wapiga kura kuonekana na picha zao wamejiandikisha zaidi ya mara mbili, picha zikifanana huku majina yakibadilishwa.
Kasoro nyingine zilizojitokeza ni kuwepo kwa majina ya wapiga kura wa jimbo hilo waliokufa lakini majina yao hayajafutwa kwenye daftari hilo.
Katika uchaguzi wa 2005 uliomweka madarakani marehemu, Richard Nyaulawa alipata kura 65,109, huku CUF ikiambulia kura 6,833, ambazo zilikuwa sawa na asilimia 8.
Katika kampeni zilizomalizika jana, CUF ilijikita zaidi katika miji maarufu jimboni humo ya Mbalizi, Ilembo, Igoma, Iyunga Mapinduzi na Santilya wakati CCM imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kufanya kampeni karibu vijiji vyote 89, huku ikiwa imepanga safu kubwa ya viongozi wake kutoka ngazi ya kitaifa hadi wabunge wote wa Mkoa wa Mbeya.
Chama cha Sauti ya Umma (SAU) kupitia mgombea wake, Subi Mwakapiki, hakikuweza kufanya kampeni za kutosha huku kikiwa kinaitupia lawama CCM iliyoongozwa na wapiga kampeni wake wakidaiwa kumkashifu mgombea huyo, mwanamke pekee katika uchaguzi huo.
Mazingira ya lugha chafu na uchochezi yalisababisha Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, katika dakika za lala salama awaonye viongozi wanaotumia lugha chafu na kukashifu wenzao huku akisisitiza kuwa mgombea wa SAU ana haki ya kulifikisha suala hilo kwenye vyombo vya sheria.
Katika madai yake alisema kuwa kata za Santilya na Ilembo majina ya watu wengi waliokufa yamebainika kuwepo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura wa jimbo hilo na wengine kadhaa kujiandikisha zaidi ya mara mbili.
Chanzo: Tanzania Daima