Wakuu nimekutana na makala moja CNN kuhusu utafiti ulioonesha kuwa Watu wanaotumia Bangi wako hatarini kupatwa na matatizo ya Shambulio la Moyo au Moyo kushindwa kufanya kazi (Heart Failure). Hii imakaaje wakati hivi karibu kumekuwa na maelezo kuwa Bangi husaidia kutibu baadhi ya Seli za Saratani?
- Tunachokijua
- Bangi ni mmea unaopatikana sehemu nyingi duniani. Historia ya kale zaidi ya mmea huu iliandikwa na Mtawala wa China, Shen Nung mnamo mwaka 2727 B.C. Dola za Rumi na Ugiriki zinatajwa kuwa jamii za kwanza kabisa kutumia mmea huu ambapo mwaka 1545 ulisambaa Kwenda Bara la Amerika Kusini (Chile).
Majani ya Bangi yakiwa na Mbegu zakeKisayansi, bangi huitwa Cannabis sativa, ambapo THC (Delta-9-tetrahydrocannabinol) hutajwa kuwa kemikali kuu inayopatikana kwenye mmea huo.
Matumizi ya Bangi kwenye tiba
Ukiachia mbali matumizi ya Bangi kama sehemu ya starehe, inaweza pia kutumika katika tiba rasmi za magonjwa ya binadamu. Hata hivyo, hupaswa kupitia michakato kadhaa kabla haijaruhusiwa kutumika.
Kwa asili yake, mmea wa Bangi hubeba kemikali Zaidi ya 100 ambazo hufahamika kama Cannabinoids. Kila kemikali huwa na athari tofauti mwilini, lakini kemikali za Delta-9-tetrahydrocannabinol (THC) na cannabidiol (CBD) ndizo hutumika katika tiba.
Kwa mujibu wa tovuti ya afya ya WebMD, tafiti kadhaa kuhusu matumizi ya bangi kwenye kutibu Saratani, Kupoteza hamu ya kula, degedege, Presha ya macho, Kiungulia, kutapika na maumivu ya misuli zinaendelea.
Bado haijathibitika pasipo shaka uwezo wake wa kutatua changamoto hizo.
Hadi sasa, Mamlaka Udhibiti wa Dawa na Chakula (FDA) ya Marekani imepitisha dawa 3 zilizotengenezwa kwa bangi ambazo ni Epidiolex kwa kutibu degedege Pamoja na Dronabinol na Nabilone kwa kutibu kiungulia na kichefuchefu kinachosababishwa na tiba za Chemotherapy kwa watu wenye ugonjwa wa saratani.
Athari za Bangi kwenye afya ya Moyo
Kwa mujibu wa Taasisi ya Moyo ya Marekani (AHA), matumizi ya mara kwa mara ya bangi yanaweza kusababisha magonjwa ya moyo.
Haya yanabainika kutoka kwenye utafiti uliohusisha zaidi ya watu 150,000 ambapo watumiaji walikuwa na 34% zaidi ya kuoatwa na shambulio la Moyo kuliko wale wasiotumia.
Utafiti huu unafafanua zaidi kuwa athari hizi hazitokani na matumizi ya mazao ya bangi (dawa) kwa tiba maalum zinazotolewa na wataalamu wa afya.
Utafiti mwingine wenye kichwa cha habari “Recurrent stroke associated with cannabis use” wa I Mateo et al, unafafanua kisa cha mwalimu wa shule ya msingi mwenye umri wa miaka 36 aliyepata kiharusi baada ya kutumia bangi.
Pamoja na mambo mengine, utafiti huu unabainisha kuwa bangi sio bidhaa salama kama watu wengi wanavyodhani, kwani matumizi yake yanaweza kusababisha kiharusi kwa vijana wadogo.
Kutokana na uwepo wa Changamoto hizi, Taasisi ya Moyo ya Marekani (AHA) hushauri kutokuvuta au kutumia kwa namna yoyote ile bangi kwa kuwa hudhuru moyo, mapafu na mishipa ya damu.
Baadhi ya tafiti za awali zinaeleza kuwa uvutaji wa Bangi huongeza kiasi cha hewa ya Carbon monoxide kwenye mishipa ya damu ambayo huleta athari hasi kwenye moyo.
Mamlaka za Tanzania zinasemaje?
Mamlaka уа Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Novemba 13, 2023 ilisema bangi ni dawa haramu inayoongoza kwa kupatikana na kutumiwa zaidi nchini ikifuatiwa na heroin, mirungi na cocaine na hivi karibuni methamphetamine ambapo amesema dawa hizo zina madhara ya kiafya ikiwemo Mtu kuona visivyokuwepo na kupelekea kufanya vitu visivvyofaa kwenye Jamii.
Kamishna Msaidizi wa Kinga na Huduma za Jamii DCEA, Moza Makumbuli alibainisha kuwa bangi ni miongoni mwa vileta njozi ambavyo humfanya Mtumiaji kuhisi, kuona au kusikia vitu visivyokuwepo au tofauti na uhalisia.
Makumbuli aliwataka Watanzania kujiepusha na matumizi ya bangi na dawa nyingine za kulevya kwakuwa zina madhara huku akishangaa Watumiaji wa mitandao kutofurahia pale madhara ya bangi yanaposemwa au bangi ikikamatwa.
"Suala la bangi ni mtihani inaonekana wengi wanatumia, hata ukiangalia habari mfano ile ya biskuti za bangi mtandaoni comment za Watu ni kama vile wanaona bangi inachelewa kuhalalishwa, bangi haifai tujiepushe kutumia" alisema Makumbuli