Matumizi ya simu barabarani, je, sheria inasemaje?

Matumizi ya simu barabarani, je, sheria inasemaje?

chambimagaka

JF-Expert Member
Joined
Nov 17, 2017
Posts
288
Reaction score
338
MATUMIZI YA SIMU BARABARANI, JE SHERIA INASEMAJE?
Muda mrefu sasa kumekuwa na maoni tofauti kuhusu matumizi ya simu barabarani wengi wakitaka kujua ni kosa au sio kosa. Na kama ni kosa je ni kosa chini ya sheria ipi? Je, katika ulimwengu wa sasa ni rahisi dereva aendeshe gari bila kutumia simu licha ya madhara yanayojulikana ya matumizi ya simu?Leo tutaangalia iwapo sheria inasema lolote kuhusu matumizi ya simu. Tutaangalia sheria ya Usalama Barabarani na kanuni za SUMATRA.

Je, ni kosa kutumia simu huku unaendesha chini ya sheria ya usalama barabarani Tanzania sura ya 168?
JIBU NI HAPANA sheria hiyo ya usalama barabarani wala kanuni zake haina kipengele chochote kinachopiga marufuku matumizi ya simu, au kuweka headphone masikioni na kuendesha gari, au hata dereva kuangalia video ndani ya gari. Na hili halijatokea kwa bahati mbaya. Sababu yenyewe ya msingi ni kwamba hii sheria ya usalama barabarani ni ya Mwaka 1973, licha ya kufanyiwa marekebisho yam ara kwam ara, marekebisho makubwa kabisa yalifanyika mwaka 1996.

Mwaka 1996 ndio kwanza simu za mkononi zilikuwa zimeingia tu Tanzania. Kwa wale wanaokumbuka kipindi hiki simu nyingi zilikuwa za mezani, na zile za mkononi ni simu za Tri-tel na baadaye Buzz ambayo imekuja kujulikana kama Tigo. Watungaji wa sheria wakati huu hawakuhi kuweka taswira kwamba teknolojia itakua kiasi cha kila mtu kuwa na simu, kwani hata hizo Tritel hazikuwa smartphone na zilikuwa ni simu za gharama mno. Hivyo, kwa hakika kabisa tunaweza kusema sheria haikutarajia hili.

Je, ni kosa kutumia simu huku unaendesha chini ya kanuni za SUMATRA?
JIBU NI NDIYO NA HAPANA, unashangaa? Ndiyo. Ninayosababu ya kutoa jibu hili. Tunapoongelea kanuni za SUMATRA tunaongelea kanuni za mwaka 2007 na pia kanuni za mwaka 2017. Kwa sasa sina jibu iwapo kanuni zipi hasa ndio zinatumika kwani sina uhakika kama zile za mwaka 2017 zimeanza kutumika. Hebu tuangalie kanuni za mwaka 2007.

Kanuni za SUMATRA za usafirishaji abiria za mwaka 2007, Tangazo la serikali No. 218 z amwaka 2007.
Kwa mujibu wa kanuni ya 18(1)(i) ni marufuku kwa dereva kuendesha gari huku akitumia simu.

Kanuni za Leseni ya Usafirishaji-Magari ya Mizigo za mwaka 2012
Kwa mujibu wa kanuni ya 28(1)(h) dereva amekatazwa kutumia simu au kifaa kinachofanana na hicho wakati wa kuendesha gari.

Hivyo basi tunaona kuwa kwa mujibu wa kanuni hizi za usafirishaji ni kosa kuendesha gari huku dereva anatumia simu. Lakini swali la kujiuliza je, marufuku hii inamhusu kila dereva? Jibu ni HAPANA Kanuni za SUMATRA zinamhusu mtu aliyepewa leseni na SUMATRA kuendesha huduma ya usafiri na wafanyakazi wake, mtu huyu anaitwa Licensee. Yaani hadi uwe na leseni ya SUMATRA ndio kanuni hizi zinakuhusu. Hivyo ndio kusema kwamba kama humiliki gari la abiria au la mizigo kanuni hizi hazikuhusu.

Je, ni kosa kuendesha gari huku dereva akiongea na simu kwa mujibu wa kanuni mpya za Sumatra za usafirishaji abiria za mwaka 2017*? [THE TRANSPORT LICENSING (PUBLIC SERVICE VEHICLES) REGULATIONS, 2017] Tangazo la serikali Na. 421/2017?
JIBU NI HAPANA Kanuni hizi hakuna popote zinapompiga marufuku dereva kuongea au kutumia simu huku anaendesha gari.

Je, ni kosa kuendesha gari huku dereva akiongea na simu kwa mujibu wa kanuni mpya za Sumatra za usafirishaji Magari ya Mizigo za mwaka 2017?
JIBU NI NDIYO Kanuni za Kanuni za Leseni ya Usafirishaji (Magari ya Mizigo), 2012 zimefanyiwa marekebisho na Kanuni za Leseni ya Usafirishaji (Magari ya Mizigo) (Marekebisho), 2017 ambapo katika kanuni hizi mpya kifungu cha 29;32;33;34;35;36; NA 37 vimefanyiwa marekebisho. Hivyo utaona kuwa kifungu cha 28(1) hakijafanyiwa marekebisho, hivyo kufanya lile kosa la dereva kuongea na simu huku anaendesha kuendelea kuwa kosa.

KWA HIYO KWA SASA ndio kusema kwamba
(a) Iwapo kanuni mpya za SUMATRA zimeanza kufanya kazi, sio kosa tena kwa dereva wa gari la abiria kuendesha huku akiongea na simu. Wakati huo huo ni kosa kwa dereva wa gari la mizigo kuendesha huku akiongea na simu kwa mujibu wa kanuni ya 28(1).[Hata hivyo sielewi kwa nini SUMATRA wamefanya hivi, sijui ni kupitiwa au vipi]
(b) Iwapo kanuni za zamani zinaendelea kutumika, basi ni kosa kwa dereva wa gari la mizigo na yule wa gari la abiria kuendesha huku akiongea na simu.

TURUDI KWENYE SHERIA YA USALAMA BARABARANI
Hata hivyo, kwa mujibu wa kifungu cha 42(c) askari wanaweza kutoa tafsiri pana ya kifungu hicho kuhusisha na kutumia simu wakati wa kuendesha gari kwa kusema kuwa huo ni uendeshaji wa hatari(dangerous driving) au wa kipuuzi(reckless driving). Kifungu hicho kinasomeka hivi “Any person who, on any road–drives a motor vehicle or trailer in a manner which, having regard to all the circumstances of the case, is or might be dangerous to the public or to any person, shall be guilty of an offence”
Hata hivyo, tafsiri hii itabishaniwa sana labda hadi tupate kesi ambayo mtu atashtakiw akwa kosa hilo na akakata rufaa mahakama kuu na mahakama kuu ikatoa tafsiri pana kama hiyo ambayo sasa itakuwa precedent kwa matukio yote ya dereva kukutwa akiongea na simu.

Nadhani hii ndio sababu katika marekebisho ya sheria ambayo yapo katika mckahato hivi sasa kuna kipengele kinahusu kuongea na simu huku mtu akiendesha kuwa ni kosa.

Hivyo, basi licha ya kuwa matumizi ya simu ni hatari kwa uendeshaji magari barabarani bado sheria zetu hazijitoshelezi kwenye hilo. Wenzetu katika nzi za Ulaya wanaruhusu kuendesha huku unatumia simu iwapo utakuwa na handheld device, kwa maana ya kwamba simu utakuwa hujaishika, hata hivyo kwa magari ya abiria bado wanataka dereva aegeshe ndipo aongee na simu.

Ni matumaini yangu umepata kuongozo wa kukufumbua macho kidogo kuhusu kuongea na simu ukiwa unaendesha gari.
Augustus Fungo
RSAadmin1
RSA TANZANIA
USALAMA BARABARANI NI JUKUMU LETU SOTE.
 
Vitu vingine nk kujiongeza tu

Ni hatari sana kutumia simu ukiwa unaendesha. Huwa sioni tofauti na kulewa alafu ukaingia barabarani na chombo cha moto
 
Back
Top Bottom