Matumizi ya Teknolojia ya Digitali Yanaifanya Elimu Kuwa Mchakato wa Kufurahisha

Matumizi ya Teknolojia ya Digitali Yanaifanya Elimu Kuwa Mchakato wa Kufurahisha

The Sheriff

JF-Expert Member
Joined
Oct 10, 2019
Posts
747
Reaction score
2,112
60e933395aef48f2a3e77d7962aa7ec4.jpg


Mifumo ya Elimu kwa Karne hii ya 21 inapaswa kutambua kwamba tunaishi katika mazingira yanayozidi kuwa ya kiteknolojia. Ubunifu na maendeleo ya kiteknolojia yanaendelea kubadilisha namna tunavyowasiliana, kufanya kazi na kuishi.

Hata hivyo, wanafunzi wengi nchini Tanzania bado hawapati ujuzi wa msingi unaotarajiwa kwa karne hii. Hapa kwetu bado tunasumbuka na masuala madogo kama vile madawati na mahitaji ya kawaida kama vile vitabu vya kiada.

Lakini pia, shule nyingi za umma hazijaunganishwa na huduma ya umeme na hakuna vifaa vya kuwatambulisha vijana kwenye ulimwengu wa teknolojia ya digitali, jambo linalowafanya kulikabili soko la ajira baadaye wakiwa hawana ujuzi unaohitajika.

Tanzania ni sehemu ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ukanda ambapo 89% ya wanafunzi hawana kompyuta za nyumbani na 82% hawana ufikiaji wa mtandao. Hii ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Hata hivyo, elimu ya digitali ni hitaji muhimu la mafanikio katika mazingira ya kisasa yanayoendeshwa na teknolojia. Kwa mujibu wa Population Pyramid (2018) katika mataifa ya Afrika ni asilimia 30 hadi 50 ya watu wako chini ya umri wa miaka 15. Hiyo ina maana sehemu kubwa ya wakazi wa Afrika wapo katika umri sahihi wa kupata ujuzi wa TEHAMA.

Wakati huu, kujifunza kubadilisha mbinu zetu za ufundishaji kwa kujumuisha teknolojia ya digitali ndiyo njia pekee ya kuleta mwanga katika maisha ya wanafunzi wetu.

Kufundisha kwa ubao mweusi na chaki ni jambo la kizamani, na walimu katika nchi zilizopiga hatua wamehamia kutumia projekta, VCD, na mfumo wa elimu-mtandao (eLearning) n.k ili kuonesha video za mafunzo na vipindi vifupi mtandaoni ili kusaidia kuelewa kwamba kujifunza kunaweza kuwa ni mchakato wa kufurahisha na si mapambano kama ilivyo hapa kwetu.

Hili linaweza kuwafanya wanafunzi kuzingatia zaidi kwa vile sasa tuko katika enzi ya kidigitali ambapo Mtandaoni ndio maktaba yetu.

Lakini pia, katika ulimwengu wa teknolojia elimu inaweza kupitwa na wakati kwa urahisi kwani kila wakati kuna kitu kipya kinachotokea. Kuandaa wanafunzi kupata taarifa mpya zinazohusiana na somo fulani ndiyo njia bora ya kuwafundisha wanafunzi kuwa raia wenye taarifa. Kujua ni vyanzo gani wanafunzi wanaweza kurejelea mtandaoni, na kujua ni tovuti zipi zinazotoa taarifa za kuaminika zaidi inaweza kuwa njia nzuri ya kuwaongoza wanafunzi.

Muingiliano kati ya mwalimu na mwanafunzi si lazima uishie shuleni au darasani. Wanaweza pia kutumia majukwaa ya mtandaoni kujadili mada au kutoa mawazo. Hili linaweza kuwa ni njia bora kwa wanafunzi kuwasilisha mawazo yao, mapendekezo na maswali yanayohusiana na masomo yao. Njia hii inaweza kuwafanya wanafunzi kuwa makini zaidi hata nje ya shule, tena bila kutambua ukweli kwamba mchakato wa kujifunza bado unaendelea.

Mwalimu kuwataka wanafunzi kutafiti jambo fulani mtandaoni inaweza kuwa ni njia nzuri pia ya kuwafanya wanafunzi kuwa na hamu zaidi ya somo fulani. Kuwapa zawadi au kuthamini matokeo yao ya mtandaoni kunaweza kuwahimiza wanafunzi kutumia vyema rasilimali za kidigitali walizonazo.

Ikiwa teknolojia inatarajiwa kuendelea kutumika kwa kiasi kikubwa katika mifumo ya elimu duniani, wenye ujuzi wa teknolojia watakuwa wanahitajika zaidi kwenye soko la ajira kwani kila kitu kwa sasa duniani kinahitaji teknolojia.

Ikiwa leo ni Siku ya Elimu Duniani, kama nchi hatuna budi kuhakikisha tunabadilika kutokana na mahitaji muhimu ya dunia. Hatuwezi kuendelea kuwa na kizazi ambacho kinatambulishwa kwa teknolojia ya digitali baada ya kufika chuo kikuu.
 
Back
Top Bottom