Matunda ya FOCAC yawafanya viongozi wa Afrika kuwa na matarajio makubwa na mkutano wa Beijing wa mwaka huu

Matunda ya FOCAC yawafanya viongozi wa Afrika kuwa na matarajio makubwa na mkutano wa Beijing wa mwaka huu

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,116
Reaction score
1,121
1722562362537.png


Wakati Beijing ikiwa inaendelea na maandalizi yake ya mkutano mpya wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) ambao unatarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 4 hadi 6 mwaka 2024, viongozi mbalimbali wa nchi za Afrika wameonesha kuridhishwa na wamekuwa na imani kubwa juu ya ushirikiano huu ambao umeshuhudiwa ukizizindua nchi nyingi ambazo hapo awali zilionekana kuwa kwenye usingizi mzito.

Kuzinduka kwa nchi hizi za Afrika kumezifanya kutaka kuendana na kasi ya dunia hasa kwa nchi ambazo zina miundombinu ya kutosha na ya kisasa, pia kuwa na wataalamu wa kuendesha mambo. Dhamira isiyoyumba ya kidiplomasia ya China ya kushirikiana na nchi za Afrika imezaa matunda makubwa kupitia baraza hili la FOCAC.

Katika miaka ya hivi karibuni, China imepeleka miradi mingi zaidi ya ushirikiano kwa nchi za Afrika ambayo imeleta manufaa yanayoonekana dhahiri. Tangu kuanzishwa kwa FOCAC mwaka 2000, makampuni ya China yamesaidia nchi za Afrika kujenga au kuboresha reli, barabara kuu, madaraja, bandari, usambazaji wa umeme, na huduma ya mtandao wa internet, ujenzi wa shule na hospitali n.k na kuleta faida kubwa kwa watu wa Afrika.

Matunda ya FOCAC ni makubwa sana, kwa sababu mbali na kujikita kwenye ujenzi wa miundo mbinu na kuwaondoa watu kwenye umasikini, pia baraza hili ni jukwaa muhimu sana kwa watu wa China na Afrika kutekeleza kanuni tano za kuishi kwa pamoja na kuhimiza maendeleo ya pamoja kama alivyosema rais Xi Jinping hivi karibuni alipokutana na rais wa Guine Bissau Umaro Sissoco Embalo.

China ikiwa mwanzilishi wa kanuni hizi tano za kuishi pamoja kwa amani, rais Xi amesisitiza kuwa kupitia FOCAC China iko tayari kushirikiana na nchi za Afrika kuongoza pamoja kanuni tano za kuishi pamoja kwa amani, kujadili mipango mikubwa ya ushirikiano wa China na Afrika katika zama mpya, kulinda maslahi ya pamoja ya nchi zinazoendelea na haki na usawa wa kimataifa, na kujenga kwa pamoja jumuiya ya China na Afrika yenye mustakabali wa pamoja.

Eneo jingine ambalo limekuwa likipewa kipaumble na FOCAC kwa sasa ni hili la ushirikiano wa uchumi wa buluu. Nchi ambazo zinaunganishwa na bahari, zinabeba matumaini makubwa juu ya ushirikiano huu. Katika miaka ya hivi karibuni China imekuwa ikichukua hatua madhubuti za kujenga ushirikiano wa buluu na nchi za Afrika hasa zile zinazopitiwa na bahari.

Kwenye Dira ya Ushirikiano kati ya China na Afrika 2035 iliyotolewa kwenye Mkutano wa nane wa Mawaziri wa FOCAC mwaka 2021, ushirikiano wa uchumi wa bluu umeorodheshwa kama eneo jipya la ukuaji ambalo linaweza kuongeza thamani na kutumia rasilimali za baharini kwa njia endelevu. Miradi ya miundombinu katika nyanja hii imetoa nafasi nyingi za ajira kwa wenyeji na kusaidia kutoa mafunzo kwa wahandisi, mafundi na wataalamu wengine wenye ujuzi kwa Afrika.

Mradi wa bandari ya Lamu nchini Kenya ni mfano mzuri kabisa. Mradi huu una nafasi muhimu katika Dira ya Kenya ya 2030, ambao ni mpango wa maendeleo wa muda mrefu wa nchi hiyo. Bandari hiyo iliyojengwa na kampuni ya China ni sehemu ya jitihada za Kenya kuwa kitovu kikuu cha biashara katika Afrika Mashariki.

Halikadhalika, mwanzoni mwa mwaka huu rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, alipokutana na Naibu Waziri wa Maliasili wa China Sun Shuxian, alisema kuwa China na Zanzibar zinatiliana saini hati ya ushirikiano katika sekta ya uchumi wa buluu ikiwemo sayansi na teknolojia ya baharini, uchunguzi wa mazingira ya bahari, utabiri wa ufuatiliaji na tathmini ya maafa, utafiti wa baharini, kujengea uwezo, uwekezaji, uhifadhi wa viumbe hai wa baharini na ulinzi wa mfumo wa ikolojia wa baharini.

Baada ya miradi hii kutekelezwa, Zanzibar kikiwa kisiwa ambacho kina utajiri mkubwa wa bidha za baharini, kupitia ushirikiano huu wa FOCAC itaweza kujiinua na kunufaika zaidi.

Na kwa sasa, wadau na watu mbalimbali wametega masikio yao China, wakisubiri kwa hamu kujua mkutano wa mwaka huu wa FOCAC utatoa matamko gani ya ushirikiano kati ya China na Afrika huku wakiwa na matarajio makubwa juu ya mkutano huu.
 
Back
Top Bottom