JanguKamaJangu
JF-Expert Member
- Feb 7, 2022
- 2,780
- 6,607
Ukipita baadhi ya maeneo yaliyopo pembezoni mwa barabara kwenye Jiji la Dar es Salaam kuna vituo maalumu ambavyo jamii au Mtu anaweza kupita na kupata huduma ya maji ya kunywa bure bila gharama yoyote.
Nimeuliza baadhi ya watu nimeambiwa mashine zilizo nyingi zimefungwa na wadau kwa kujitolea, mfano eneo la Ofisi za Zimamoto karibia na mataa ya Fire, Kariakoo Bigbon, Kinondoni Biafra, Kawe-Malingo eneo la Msikiti.
Hata hivyo licha ya tija hizo lakini watumiaji katika maeneo mengi ambayo nimefanikiwa kufika na kufuatilia wapo katika hatari zaidi ya kupata magonjwa ya kuambukiza pamoja na magonjwa ya mlipuko, na uenda wengine wameshakumbana nayo kwa kujua chanzo au kutokujua.
Ni katika hali ya kuuzunisha maeneo mengi ambapo kuna huduma hizo, unakuta vikombe vinavyotumika ni vitatu au viwili tokea asubuhi mpaka jioni bila kuoshwa, yaani Mtu anafika eneo husika yalipo mabomba yanayotoa maji anachukua kikombe ambacho hakijasafishwa vizuri palepale anakunywa maji na kuondoka.
Pia katika mazingira hayo unakuta Mtu anafika eneo hilo, mfano wanaookota taka za plastiki anashika kikombe na kunywa maji bila kunawa mikono, vilevile wakija na wengine na chombo kilekile nao wanaitumia kwa mtindo huohuo.
Kuna maeneo mengine vyombo hizo zimefungiwa na kamba kabisa, ikiwa ni kuhofiwa kuibiwa, kutokana na hali hiyo nimeshuhudia mara kwa mara Mtu anaishika ‘glasi’ ikiwa kwenye kamba anakunywa maji na kuondoka, bila kuoshwa wala kusafishwa vizuri na mwingine akija anatembea kwenye mtindo huohuo.
Uenda waliojitolea au kuratibu huduma hizo walikuwa na dhamira njema, lakini kwa mtindo huo, afya za Wananchi wengi zipo hatarini ikiwemo Watoto, Wanafunzi ambao wemekuwa wakifika maeneo hayo na kupata huduma.
Wito wangu katika hilo, ni vyema mamlaka kushirikiana na wadau kuja na ubunifu wa kuboresha utoaji wa huduma za aina hiyo ili kuwezesha jamii kujikinga na magonjwa ya kuambukiza pamoja na magonjwa ya milipuko.
Licha hilo ni muhimu mamlaka husika hasa Wizara ya Afya kuchukua hatua za haraka ikiwemo kukagua maeneo hayo, sambamba na kusitisha vituo hivyo kuendelea kutoa huduma kwa sasa mpaka vitakapoboreshwa, maana inavyoonekana athari zake uenda zikawa kubwa zaidi ya faida inayoweza kuwa ipatikana kwa sasa.