Mbinu tano (5) halali za kuchelewesha mnada wa hadhara wa nyumba yako uliyoombea mkopo

Mbinu tano (5) halali za kuchelewesha mnada wa hadhara wa nyumba yako uliyoombea mkopo

Aliko Musa

JF-Expert Member
Joined
Aug 25, 2018
Posts
209
Reaction score
315
Nyumba yako au ardhi yako kuuzwa kwa njia ya mnada wa hadhara ni jambo ambalo linaweza kutokea ikiwa umeamua kujenga utajiri kupitia uwekezaji huu.

Chanagamoto ya kuuzwa nyumba au ardhi yako kwa njia ya mnada wa hadhara inaweza kutokana na sababu za kibinadamu au sababu ambazo zipo nje kabisa ya uwezo wako.

Ingawa wengi uzembe wao wa kutojifunza na kutofanyia kazi maarifa waliyonayo umepelekea nyumba au ardhi zao kuuzwa kwa njia ya mnada.

Kuna sababu tofauti tofauti zinazo ifanya nyumba yako au ardhi yako iuzwe kwa njia ya mnada wa hadhara.

Kwenye somo hili nimelenga sababu moja tu; kushindwa kukamilisha marejesho ya mkopo wako.

Kushindwa kulipa mkopo kutoka kwenye taasisi za fedha ni chanagamoto inayowakumba wawekezaji au wamiliki wengi.

Kuchukua mikopo mibaya ndiyo sababu kuu ya kushindwa kukamilisha marejesho ya mkopo ambayo nyumba au ardhi yao imetumika kama rehani.

Watu wamechukua mikopo ya majengo na kutumia mikopo hiyo kununulia nguo, chakula, starehe na kadhalika.

Hii imepelekea kwenye chanagamoto ya kushindwa kukamilisha marejesho ya mikopo yao.

Mikopo Mizuri.

Mikopo mizuri inatakiwa kulipwa na wapangaji wako au wanunuzi wa viwanja au mashamba yako.

Mikopo ambayo unaichukua ili ulipe kwa mshahara wako au faida ya biashara yako nyingine tofauti na ardhi na majengo ni mikopo mibaya.

Mikopo hiyo mibaya imekuwa kikwazo kwa wawekezaji wengi sana kwenye uwekezaji huu.

Na minada ya hadhara ya nyumba nyingi imekuwa ni kwa wamiliki wa nyumba na sio wawekezaji.

Mtu anatumia nyumba yake ya familia kuombea mkopo. Kisha hutegemea kulipa kwa mshahara wake mdogo au faida ya biashara yake.

Inapotokea chanagamoto ndogo kwenye ajira yake au kuyumba kwa biashara yake hukosa fedha za kurejesha mkopo alionao.

Hatimaye taasisi husika ya mikopo hupewa ruhusa ya kuuza ardhi au nyumba kwa njia ya mnada. Hapo ndipo anakuwa amepoteza sifa ya kuwa mmiliki wa ardhi au nyumba husika.

Mbinu hizi zinaweza kuchelewesha kufanyika kwa mnada wa nyumba yako au kuzuia kabisa mnada wa nyumba yako. Usikubali upoteze umiliki wa nyumba au ardhi yako bila kuweka juhudi za aina yoyote.

Mbinu Tano (5) Za Kuchelewesha Mnada Wa Nyumba Yako.

Moja.

Fanya Mazungumzo Na Timu Yako Ya Mikopo.

Hii ni mbinu ya mwanzo unayotakiwa kuifanya mara baada ya kugundua kuwa huwezi kumudu kurejesha mikopo yako kwa miezi kadhaa.

Mtoa mkopo wako ni moja ya wanatimu wako wa uwekezaji kwenye ardhi na majengo. Hivyo unatakiwa kumuambia ukweli na akushauri njia mbadala za kuweza kurejesha fedha zake kwa wakati.

Wanatimu wengine muhimu kufanya nao mazungumzo kuhusu kushindwa kwako ni kama ifuatavyo;-

✓ Mhasibu mzoefu wa uwekezaji kwenye ardhi na majengo.

✓ Wakili mzoefu kwenye ardhi na majengo.

✓ Wakala wa mikopo.

✓ Mshauri mbobezi kwenye ardhi na majengo.

Hawa wanaweza kukushauri mambo ambayo yanaweza kuondoa kabisa chanagamoto yako ya kushindwa kukamilisha marejesho ya mkopo wako.

Muombe mtoa mikopo akufanyie tena tathimini ya hali yako ya kifedha. Hii itakupa nafasi ya kuendelea kupata muda wa kutafuta njia bora zaidi za kukamilisha marejesho ya mkopo wako.

Mbili.

Mazungumzo Kuhusu Marejesho Uliyoshindwa.

Hakikisha unawasiliana na afisa mtoa mkopo wako kuhusu marejesho ambayo umeshindwa kurejesha kwa wakati.

Afisa mkopo anaweza kufanya yafuatayo kuhusu marejesho hayo;-

✓ Kukusamehe marejesho uliyoshindwa.

✓ Kuhamishia marejesho hayo kwenye malipo ya miezi ijayo. Mfano, kama umeshindwa kurejesha tshs.240,000 (laki mbili na elfu arobaini). Afisa mikopo anaweza kuigawanya hiyo kwenye marejesho ya miezi 12 ijayo.

Hivyo utakuwa na ongezeko la tshs.20,000 kwenye marejesho ya awali kwa kila mwezi ndani ya miezi 12.

Baada ya miezi hiyo 12 utarudi kuendelea kufanya marejesho yako ya kawaida kama ilivyokuwa awali.

Hii inaweza kuwa ni suluhu ya kudumu ya nyumba yao kutouzwa kwa njia ya mnada wa hadhara.

Endapo hauna kiasi kingine cha kukamilisha marejesho yako unaweza kuomba nafasi ya kuuza ardhi yako au nyumba yako.

Njia za kuondokana na hili litategemea sana na hali uliyonayo ya kifedha kwa sasa.

Tatu.

Mazungumzo Ya Kuboresha Masharti Ya Mkopo.

Taasisi za fedha zinaweza kubadili masharti ya mkopo ulioomba kutoka masharti magumu na kuwa masharti rahisi kwako.

Taasisi inaweza kukupunguzia kiasi cha riba ya mkopo wako na ukaweza kumudu kukamilisha marejesho ya mkopo huo.

Mto mkopo anaweza kuongeza miaka au miezi ya wewe kukamilisha marejesho ya mkopo kulingana na maombi yako na ukubali wake.

Mbinu hii inaweza kuwa suluhisho la kudumu la nyumba yako kuuzwa kwa njia ya mnada wa hadhara.

Pia, inaweza kuwa ni mbinu ya kuchelewesha kufanyika kwa mnada wa hadhara wa nyumba au ardhi yako.

Nne.

Kuchelewesha Machakato Wa Shauri Mahakamani.

Kuna njia tofauti tofauti za kuchelewesha kufanyika kwa maamuzi ya shauri la kushindwa kukamilisha marejesho ya mkopo wako.

Baadhi ya njia hizo ni kama ifuatavyo;-

✓ Mwenyekiti wa baraza kuomba mapitio ya kujiridhisha na taarifa na muenendo wa shauri hilo.

✓ Mshitakiwa au mshitaki kukosea moja ya nakala kwenye shauri husika.

✓ Kutoa taarifa ya kuumwa au kuuguza ndugu au jamaa wa karibu. Ni vizuri kuwa na uthibitisho kutoka kwa daktari wa binadamu.

✓ Kutokuwepo kwa mwenyekiti wa baraza siku ya kusikilizwa shauri kutokana na sababu mbalimbali.

✓ Kutokuwepo wahusika wengine wakiwemo wazee wa baraza, watu wa upande wa mshitakiwa na mshitaki na kadhalika.

✓ Kuchelewa kufika kwa nyaraka muhimu kwa sababu ya changamoto za shirika la posta Tanzania.

✓ Upande wa mmoja (mshitakiwa au mshitaki) kuomba kutokuwa tayari kusikiliza shauri siku husika.

Wakati wa kuchelewesha kufanyika kwa maamuzi haya, hakikisha unapambana kutafuta mbinu za kukamilisha marejesho ya mkopo wako.

Shauri litafutwa mara baada ya kukamilisha marejesho ya mkopo wako. Pia, shauri linaweza kusubirishwa kwa kuonyesha uwezo ulionao wa kukamilisha marejesho endapo utaongezwa miezi mitatu, sita au 12.

Tano.

Mazungumzo Ya Kusitishwa Kwa Mchakato Wa Mnada Wa Hadhara.

Unaweza kuonyesha uhakika wa kulipia deni lote endapo utaongezwa muda wa ziada wa kufanya marejesho.

Jambo hili linawezekana kwa uangalizi mkubwa kutoka kwenye mahakama yenye mamlaka.

Hii itakuwa ni njia ya kudumu ya kutokuuzwa nyumba yako kwa njia ya mnada wa hadhara.

Pia, njia hii inaweza kuwa ni mbinu ya kuchelewesha kufanyika mnada wa hadhara wa nyumba yako ili upate muda ya kutafuta fedha huku na kule.

Kwenye hatua zote hizo hutakiwi kumuacha wakili mzoefu unayefanya naye kazi.

Hata hivyo, somo hili haliwezi kamwe kuondoa umuhimu wa wakili mzoefu kwenye mchakato wa kufanikisha jambo hili.

Somo hili nina hakika limekupa mbinu mbadala ya kupanga mipango na wakili wako mzoefu. Mbinu nyingine bora sana atakupatia wakili wako.

Pia, mimi ninaweza kuwa mmoja wanatimu wako. Ukiwa na mimi nitahakikisha ninakupa ushauri bora kabisa wa kujenga utajiri wako kupitia uwekezaji kwenye ardhi na majengo.

Rafiki yako,

Aliko Musa.

WhatsApp; +255 752 413 711
 
Back
Top Bottom