SoC02 Mbuga ya Saadan, dhahabu iliyowekwa kabatini!

SoC02 Mbuga ya Saadan, dhahabu iliyowekwa kabatini!

Stories of Change - 2022 Competition

Zuriel_cfc

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2017
Posts
4,092
Reaction score
9,063
saadani-6.jpg

Saadan! Mbuga iliyopo pembezoni mwa bahari ya hindi, ukanda wa bagamoyo ni eneo la thamani sana ambalo serikali imelisahau, ama limeifumbia macho ama haijui kama inaweza kuwa sehemu ya kuiongezea kipato kwa kiasi kikubwa sana.

Wakati nilipotembelea mbuga hii kwa shughuli za kueneza mawasiliano ya vodacom, tulifika katika vijiji kadhaa ila ningependa kuviongelea vijiji viwili Kitame na Coastal, ambavyo mara tu nilipofika nilipoona mazingira nikaifikiria nchi yangu, ilivyojaliwa na utajiri wa asili na namna ambavyo inawezekana kuwa na maeneo mazuri zaidi ya utalii ukiacha Arusha na sehemu nyingine.

Vijiji hivi ninavyoviongelea vinavutia sana kwa uwekezaji wa hotel za kisasa, hotel ambazo zinajengwa kwa mfano wa kijiji, na vibanda vyake vinakuwa vinaning'inia kwenye maji na huku kukiwa na njia nzuri inayoelekea kwenye vibanda hivyo.

Coastal ipo km10 hivi kutoka mbugani saadani, kuelekea pwani, yaani ipo pembezoni mwa bahari. kuna wapemba wanafanya biashara ya samaki na vitu vidogo vidogo, pia kuna kiwanda cha kuchakata chumvi. Ni sehemu nzuri sana kwa utalii wa kujenga hotel aina hiyo niliyoitaja hapo juu, nyumba kama zile za maldives pale ndo mahala pake, hata hawa wanakijiji wanaoishi pale, wametengeneza nyumba za juu, chini kuna maji. (Wameweka miti)

Panaweza kutengenezwa kwa dizaini hii na pia usafiri ukawa wa aina mbili, kwa barabara kutokea bagamoyo, makurunge, Saadani au kwa boti kutoka Dsm, bagamoyo hadi Saadani Coastal! Fikiria patapendeza kiasi gani kwa Tanzania kuwa na hotel ya kisasa kama ile ya Isaraya ya zanzibar pale Saadan, huku ukikutana na wanyama mbali mbali kama twiga, tembo n.k

saadani1.jpg


Kijiji cha pili ni kitame, huku kuna mashamba ya chumvi. Kuna mzungu mmoja ( sijajua ni wa nchi gani) amewekeza kiwanda cha chumvi hapa kitame. Hiki kijiji watu wanaenda kwa msimu tu kwa ajili ya kufanya kazi kiwandani, msimu ukiisha wanarudi vijiji vya jirani kama matipwili, Saadan n.k

Nako kule ni pazuri sana kwa utalii, kuna minazi mingi na mchanga mweupe wa bahari, upepo mwanana kabisa. Kunafaa kuendelezwa kwa kujenga hotel nzuri ya kitalii, kukawekwa na zile shughuli za baharini kama michezo ya kwenye maji, kudive, hata kuvua samaki kipindi jua linazama.

Natamani sana nchi yangu na wizara ya utalii kwa ujumla kuangalia kwa upya vijiji hivi na kuviendeleza vitatupa pesa nyingi kupitia utalii, pia vijana wengi tutapata ajira kule. Hao wawekezaji wanaokuja wangeoneshwa na Saadan sio Arusha tu kwenye utalii. Tuna rasilimali nyingi za kutuongezea kipato cha Taifa hasa tukitembelea maeneo mengi yaliyojificha. Saadan ukiacha bahari na mbuga pia kuna maporomoko ya mto wami ambayo nayo ni kivutio kikubwa. Pakiboreshwa tutakuwa na kivutio kizuri kuwahi kutokea Tanzania.

Usafiri wa kufika pale ni rahisi tu, na hivi daraja la mto wami linaelekea kukamilika, unaweza kupitia bagamoyo, makurunge, kupitia kiwanda cha sukari cha Bahresa au mkata, au wami pale kwenye kijiji cha mandera, kwa gari.

Ama pia kukawa na magari maalum na boti maalum za kitalii kwa ajili ya kubeba watalii kutoka bagamoyo kuelekea Saadani.

africa_tanzania_saadani_gallery_beach.jpg


Utalii ni sekta pana yenye nyanja mbali mbali za fursa, watu watawekeza kwenye vijiji vinavyoizunguka Saadan ambavyo kwa sasa asilimia kubwa ni mapori. Kuna vijiji vya mandela, miono, mkange, matipwili n.k pamoja na kwamba kuna wananchi wanaishi lakini havina maendeleo. Bado wanachi wake wana maisha duni, wakitegemea kilimo. Kwa kuiboresha Saadan na kuwa moja ya vivutio vikuu vya utalii Tanzania, hata hawa wananchi watanufaika, aidha kwa kufanya biashara pembezoni mwa barabara ya kuelekea Saadan au hata kuvutia wageni kuwekeza kwa kujenga nyumba za kupangisha, ama nyumba za wageni hasa wale wa gharama nafuu au za wafanyakazi watakaokuwa wanafanya mbugani.

Kwa kuhitimisha makala yangu, ninaiomba Serikali kupitia Wizara ya maliasili na utalii kuiangalia mbuga hii ya Saadan kwa namna ya kipekee, inahitajika nguvu ya ziada ili kuiboresha na kuifanya iwe mbuga ya kipekee iliyopo pembezoni mwa bahari, ambayo itaongeza idadi ya watalii nchini mwetu. Ni vizuri kuendeleza rasilimali zetu ili kuongeza pato la Taifa na kuongeza ajira na fursa kwa vijana wetu na wananchi kwa ujumla.

Ama pia kutafuta mwekezaji, awe mzawa ama mgeni akatutengenezea kitu kizuri, kikubwa kwa maendeleo ya Taifa letu. Nasi tujivunie vya kwetu...

Picha kwa hisani ya mtandao.
 
Upvote 1
Umepasahau kwasunga ...handeni napo ni potential sana ardhi ina rutuba mazingira yanavutia sana ....kwasunga iko mbele ya miono

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom