Mbunge Mgalu aipongeza wizara ya ardhi kwa kutatua migogoro ya ardhi Bagamoyo

Mbunge Mgalu aipongeza wizara ya ardhi kwa kutatua migogoro ya ardhi Bagamoyo

Wizara ya Ardhi

Govt Institution
Joined
May 14, 2024
Posts
306
Reaction score
165
4ca062f0-47de-42b0-82e3-d7e975fe86d9.jpeg
472ec0b2-10d3-4704-9999-de134e852b3b.jpeg
026aa870-a2f0-459f-9116-4aa626700dc6.jpeg
e2a8637d-d00a-4f0f-b6e9-b908bb052136.jpeg
7a4be428-5ca4-409c-b9d0-58a76570afcf.jpeg
b5d221fc-6fe4-4331-bf05-9effa4807eaa.jpeg
b4d9f1e1-095d-4221-ad3b-cc3e7829167a.jpeg



Bagamoyo, Pwani

Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo, Mhe. Subira Hamis Mgalu, ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutekeleza kwa ufanisi agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, la kushughulikia migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Bagamoyo kupitia Kliniki ya Ardhi iliyofanyika kuanzia tarehe 19 hadi 23 Oktoba 2026.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha Kliniki hiyo, Mhe. Mgalu amesema hatua hiyo ya Serikali imekuwa suluhisho muhimu kwa migogoro mbalimbali ya ardhi iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa Bagamoyo kwa muda mrefu, huku akieleza kuridhishwa kwake na namna wataalamu wa Wizara walivyoshughulikia malalamiko ya wananchi kwa kuzingatia haki, amani na maridhiano.

Amesema timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ikiongozwa na Kamishna wa Ardhi, iliwasili Bagamoyo tarehe 19 Oktoba 2026 kwa ajili ya kutekeleza agizo hilo, ambapo Waziri mwenye dhamana ya Ardhi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, alishiriki uzinduzi wa Kliniki hiyo na kusikiliza kero mbalimbali zilizowasilishwa na wananchi.

Mhe. Mgalu amesema katika kipindi chote cha Kliniki hiyo, ameshuhudia wananchi wakisikilizwa kwa makundi kulingana na aina ya migogoro yao, huku baadhi yao wakitoa ushuhuda wa kuridhishwa na huduma walizopatiwa baada ya changamoto zao kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya amani na maridhiano.

Aidha, amewataka baadhi ya wenyeviti wa vitongoji kuacha vitendo vya kuuza eneo moja la ardhi kwa zaidi ya mtu mmoja, akieleza kuwa tabia hiyo imekuwa miongoni mwa vyanzo vikubwa vya migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Bagamoyo.

Ameonya kuwa hatasita kushirikiana na vyombo vya sheria kuhakikisha viongozi watakaobainika kuchochea au kuzalisha migogoro ya ardhi wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.Mhe. Mgalu ameeleza kuwa sehemu kubwa ya malalamiko anayopokea kutoka kwa wananchi wa jimbo lake yanahusu migogoro ya ardhi inayowakabili watu binafsi na makundi mbalimbali, hali inayochangiwa pia na ongezeko la mahitaji ya ardhi kutokana na kasi ya uwekezaji na ukuaji wa Mji wa Bagamoyo.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mgalu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri Mkuu, Waziri wa Ardhi, Naibu Waziri wa Ardhi pamoja na wataalamu wote wa Wizara kwa kuhakikisha changamoto za ardhi zinazowakabili wananchi wa Bagamoyo zinapatiwa ufumbuzi.

Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Ardhi, Bw. Hussein Sadick, amesema Kliniki hiyo imetekeleza kikamilifu maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ambapo wananchi binafsi na vikundi mbalimbali wamepata fursa ya kusikilizwa na changamoto zao za ardhi kupatiwa ufumbuzi.

Naye,Afisa Maendeleo ya Ardhi wa Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo, Bw. Deogratias Joseph Matiya, amesema Kliniki hiyo imehudumia wananchi zaidi ya 600, ambapo changamoto zao zimeshughulikiwa kupitia usikilizaji wa malalamiko, utatuzi wa migogoro, utoaji wa elimu na ushauri wa kitaalamu kulingana na aina ya changamoto zilizowasilishwa.

Amesema utekelezaji wa Kliniki hiyo imewezesha wananchi kupata huduma za wataalamu wa ardhi kwa ukaribu, hatua inayochangia kuimarisha uelewa wa masuala ya umiliki wa ardhi, kupunguza migogoro na kujenga mahusiano bora kati ya wananchi na mamlaka zinazohusika na usimamizi wa sekta ya ardhi.
 
Back
Top Bottom