Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, limesema litamfikisha mahakamani Mbunge wa Jimbo la Rombo, (Chadema), Joseph Selasini (50), kufuatia ajali ya gari alilokuwa akiendesha kusababisha vifo vya watu wanne.
Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Absalom Mwakyoma, ambaye kwa sasa amehamishiwa mkoani Mara, aliieleza hayo NIPASHE Jumamosi, kuhusu hatua zinazofuata baada ya ajali hiyo ambapo mbunge huyo alikuwa dereva wa gari hilo.
Kwa mujibu wa sheria za usalama barabarani, dereva anayesababisha ajali hufikishwa mbele ya chombo cha haki ambacho ni mahakama.
Alisema wanachosubiri ni michoro ya askari aliyepima ajali hiyo, kwani yapo mambo mengi kutokana na ajali hiyo iliyotokea katika barabara kuu ya Moshi Arusha baada ya gurudumu kupasuka.
Polisi tuna maadili, tunasubiri apone kwani alikuwa mahututi na amefiwa na mama yake mzazi, mkwe na ndugu wengine huku mke wake akiwa bado yu mahututi hospitalini, tutapima ajali na tutachunguza...Sheria lazima ifuate mkondo wake na kesi dhidi yake ipo pale pale, alisema Mwakyoma.
Aidha, alisema ajali hiyo inahitaji uchunguzi wa kina kwa kuwa inahusisha mambo mengi ikiwemo gurudumu moja kupasuka na kisha gari kwenda kuparamia kalavati, hivyo mara baada ya uchunguzi kukamilika sheria itafuata mkondo wake.
Ajali hiyo ilitokea Mei 24, mwaka huu, majira ya saa 1 usiku, katika eneo la Chuo cha Ufundi Bomangombe, barabara ya Moshi Arusha, wakati akitokea kwenye msiba wa padri mkoani Arusha, ambapo watu wawili walifariki papo hapo.
Chanzo cha ajali hiyo kinaelezwa ni mwendo kasi na kumkwepa mwendesha pikipiki. Gari lilikuwa likiendeshwa na mbunge huyo ni lenye namba za usajili T 441 BRT aina ya Toyota Land Cruiser VXR s/Wagon.
Katika gari hilo, kulikuwa na abiria sita, ambapo wawili walifariki eneo la tukio, mmoja hospitali ya wilaya ya Hai, na mwingine usiku baada ya kufikishwa hospitali ya rufaa ya KCMC kwa matibabu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mbunge huyo, aliiomba Serikali kufanya ukaguzi wa kina wa bidhaa na vipuri vya magari vinavyoingizwa kutoka nje ya nchi, kwa kuwa ni siku tatu zilizopita alinunua magurudumu ya gari hilo, ikiwa ni pamoja na elimu kwa waendesha bodaboda na baiskeli.
Hii ni ajali ya pili kwa mbunge huyo, baada ya ajali ya kwanza mwaka juzi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, ambapo alivunjika mkono wa kulia mara tatu.
Sosi: ippmedia.com