Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
Mtoto mwenye umri wa miaka saba, Kurwa Musa, mkazi wa Mwasele A katika Manispaa ya Shinyanga, amekufa baada ya kushambuliwa na mbwa watano, wakati akitafuta kuni.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Charles Nyanda, aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa, tukio hilo lilitokea saa 12:45 jioni, Juni 2, mwaka huu katika eneo hilo.
Alisema wamiliki wa mbwa hao wanashikiliwa na polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kuua bila kukusudia.
Watuhumiwa hao ni Magreth Mambari (39) na Issa Moses (21), wote wakazi wa Mwasele A mjini hapa na kwamba watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
Alisema mtoto huyo alishambuliwa wakati akiwa umbali wa takribani mita 200 kutoka nyumbani kwao.
Nyanda alisema Kurwa alitumwa na wazazi wake kwenda kutafuta kuni kwa ajili ya kupikia chakula cha usiku.
Alisema mtoto huyo akiwa anatafuta kuni, alivamiwa na mbwa hao waliokuwa wametoka nyumba ya jirani, ambapo walimshambulia kwa kumuuma sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kwa mujibu wa Nyanda, mbwa hao walimwangusha chini (Kurwa) na kuanza kumnyofoa baadhi ya viungo vya mwili wake.
Kaimu Kamanda huyo alisema mbwa hao, wanadaiwa kuwa na desturi ya kufungwa tangu asubuhi hadi jioni.
Alisema mbwa hao walipenya kwenye tundu la uzio wa nyumba ya watu wawili wanaowamiliki, na kwenda kumshambulia msichana huyo.
Alisema wakati mbwa hao wakimshambulia Kurwa, mpita njia mmoja aliwaona (mbwa) wakigombania nyama, na baada ya kuchunguza aligundua kuwepo mkono wa binadamu na baadaye mwili.
Nyanda alisema baada ya mpita njia huyo kuuona mwili huo, aliwaita watu waliokuwepo karibu na eneo la tukio, kisha walikwenda kutoa taarifa polisi na kuuchukua mwili huo kuupeleka katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga.
CHANZO: NIPASHE