Judy, kwanza nianze kwa kusema unafanya vema kuuliza maswali kwa mtazamo wa kitheologia kwa sababu kuuliza maswali hakumaanishi mtu hana imani, ila kama una mashaka na jambo analofanya Mungu kupitia Mchungaji Masapila katika kijiji kidogo cha Samunge hilo ni jambo lingine na unahitaji Mungu akufunulie kwani mambo haya ya imani hufahamika kwa imani. Theologia kama neno lenyewe lilivyo ni muunganiko wa maneno mawili "theos" lenye maana ya Mungu kwa lugha ya Kiyunani na "logia' lenye maana ya elimu. Muungano wa maneno haya mawili ndiyo yanayotupa neno theologia lenye maana kwa kifupi "elimu kuhusu Mungu." Kwa mantiki hiyo, si vibaya kuuliza maswali kwa sababu kuwa mkristo hakumaanishi kuamini bila kuuliza maswali yanayohusu Mungu na imani kwa ujumla kwa sababu maswali husaidia sana katika kuimarisha imani kama yanaulizwa katika msingi wa kuimarisha imani ya mtu.
Hata hivyo, inawezekana kuuliza maswali na tusipate majibu yanayotosheleza utafiti wetu ama kuridhisha akili na ufahamu wetu wa kibinadamu. Hii inatokana na ukomo (limitation) wa uwezo wa ufahamu wa kibinadamu. Judy, naamini utakubaliana nami kwamba binadamu, hata mwenye akili nyingi sana ana ukomo wa ufahamu wake. Hawezi kuelewa kila kila kitu hata mambo ya kawaida sembuse ya Mungu ambayo pasipo ufunuo wa Roho Mtakatifu ni vigumu sana kuyaelewa.
Kwa kuwa wewe ni mtheologia kwani umejitambulisha hivyo, bila shaka unafahamu kwamba Mungu amekuwa akitenda miujiza akiwatumia watu tofauti tofauti kwa nyakati tofauti na kizazi tofauti kulingana na mahitaji yao. Nionavyo mimi suala la msingi hapa siyo jinsi Mungu anavyofanya miujiza ama anamtumia nani na ni wapi ila ni yale anayofanya Mungu kupitia mtu anayemchagua. Suala lingine ni je ishara hizo zinathibitishwa kwa Neno la Mungu (Biblia) na zaidi sana ni nani anayepewa sifa, utukufu, enzi na heshima? Kwa maneno mengine, je anayetumiwa anawaongoza watu wamwone Mungu aliyemkabidhi huduma yenyewe ama anajiinua yeye mwenyewe na kujitwalia sifa? Haya pamoja na mambo mengine ambayo sitaweza kuyasema hapa yana umuhimu mkubwa katika kuchunguza huduma ama unabii uwao wote.
Ni vema pia tujihadhari sana tunapozungumza habari za Mungu kwani akili zetu za kibinadamu hazitoshi kuyafahamu mambo haya kikamilifu. Ningeshauri kwamba tuzungumze na Mungu kwa njia ya sala ili atufunulie ukweli juu ya mambo tunayoyaona na kuyasikia kama yanatokana naye ama ni unabii wa uwongo. Kufanya hivyo ni muhimu ili tusijetukagombana na Mungu. Mwisho kwa sasa ningesema kama alivyosema Gamalieli aliyekuwa Rabi aliyeheshimika na jamii ya Kiyahudi, kama kazi hii inayofanyika Samunge ni ya Mungu itasimama la kama si ya Mungu siku si nyingi itapotea na kama dawa ni sumu Mungu anao uwezo wa kuigeuza iwe chakula maana imeandikwa "mtawakanyaga nyoka na nge na nguvu za yule Ibilisi, hata mkinywa kitu cha kufisha hakitawadhuru, mtaweka mikono juu ya wagonjwa nao watapokea afya." Mungu akubariki katika kuyatafakari hayo na ingia kwenye maombi.