Shirika la afya duniani (
WHO) linafafanua kuwa Kisukari ni ugonjwa wa muda mrefu unaotokea pale ambapo kongosho (pancreas) haitoi kiasi cha kutosha cha insulini, au mwili haukutumia vizuri insulini inayozalishwa.
Kumbuka kuwa Insulini ni homoni inayosaidia kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu (glucose). vilevile Hyperglycaemia, ambayo pia inajulikana kama kuongezeka kwa sukari kwenye damu, ni matokeo ya kawaida ya kisukari kisichodhibitiwa, na kwa muda mrefu inaweza kusababisha madhara makubwa kwenye mifumo mbalimbali ya mwili, hasa mishipa ya fahamu na mishipa ya damu.
WHO inaendelea kueleza kuwa mwaka 2022, asilimia 14 ya watu wazima duniani waliishi na kisukari, ikilinganishwa na asilimia 7 mwaka 1990. Zaidi ya nusu yao hawakuwa wanatumia dawa, hasa katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati.
Mwaka 2021, kisukari kilisababisha vifo milioni 1.6, ambapo karibu nusu ya vifo hivyo vilitokea kabla ya miaka 70. Pia, kisukari kilichangia vifo 530,000 vya ugonjwa wa figo na takribani asilimia 11 ya vifo vya magonjwa ya moyo na mishipa.
Madai
Mtumiaji mmoja katika mtandao wa TikTok alichapisha ujumbe alioeleza kuwa mchanganyiko wa Aloe Vera na Mayai unaweza kusaidia kutibu Kisukari huku akitaka ujumbe huo usambazwe ili uwafikie watu wengi.
Je, ni upi uhalisia wa madai hayo?
Tovuti ya
Healthline iliyojikita katika machapisho ya kiafya inabainisha kuwa Virutubisho na vinywaji vya aloe vera havipendekezwi rasmi kwa watu wenye kisukari. Hadi sasa, hakuna uthibitisho wa kisayansi kuhusu aina bora ya maandalizi au kiwango sahihi cha matumizi.
Tafiti mbalimbali zilitumia aina na viwango tofauti vya aloe vera. Baadhi walikunywa juisi ya aloe vera, huku wengine wakitumia unga wenye kiambato kinachoitwa acemannan, ambacho ni polysaccharide inayoweza kusaidia kuongeza mwitikio wa kinga ya mwili.
Kutokana na utofauti huo mkubwa wa aina na viwango, ni vigumu kubaini kipimo bora na njia sahihi ya matumizi bila tafiti za ziada.
Tovuti ya Uk.news inamnukuu
Dkt. Phyu Phyu Thin Zaw, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Hong Kong, Kitivo cha Afya ya Umma, ambaye anasema hakuna ushahidi wa kisayansi unaothibitisha madai kwamba mchanganyiko huo unaweza kutibu kisukari.
Aidha anaeleza kuwa kutegemea tiba ambazo hazijathibitishwa kisayansi kunaweza kuwa hatari kunaweza kuchelewesha matibabu sahihi, na matumizi ya kiasi kikubwa cha aloe vera au mayai mabichi yanaweza kusababisha madhara kama matatizo ya tumbo au maambukizi.
Ameshauri wagonjwa wa kisukari au shinikizo la damu kufuata utaratibu wa matibabu wa daktari, kula chakula bora, kufanya mazoezi, na kwenda kliniki kwa uchunguzi wa mara kwa mara.
Kadhalika shirika la afya duniani (
WHO) linaeleza kuwa Lishe bora, kufanya mazoezi mara kwa mara, kudumisha uzito wa mwili wa kawaida na kuepuka matumizi ya tumbaku ni njia zinazoweza kusaidia kuzuia au kuchelewesha kuanza kwa ugonjwa wa kisukari cha aina ya pili (Type 2 diabetes).
Kisukari kinaweza kutibiwa, na madhara yake yakazuiwa au kucheleweshwa kupitia lishe sahihi, mazoezi ya mwili, matumizi ya dawa, pamoja na uchunguzi na matibabu ya mara kwa mara ya matatizo yanayoweza kujitokeza.