Bishop Hiluka
JF-Expert Member
- Aug 12, 2011
- 7,147
- 14,699
“UKIWA Dar es Salaam wauzaji wa maduka ya mchele huwa wanajinadi kwa mbwembwe, ‘mchele safi kutoka mbeya’. Ukishafika Mbeya unakutana na wauzaji wa maduka ya mchele wakijinadi, ‘pata mchele safi kutoka Kyela'. Na ukifika hapo mjini Kyela utakutana na wauzaji wa maduka ya mchele wakijinadi, ‘tunauza mchele safi kutoka Ipinda’. Unakufahamu Ipinda wewe? Ukishakwenda dukani muuzaji anakwambia, ‘huu ni mchele safi kabisa kutoka bonde la Tenende’. Halafu ikitokea ukazurura hadi Tenende wenyeji wanakwambia, ‘mchele safi kabisa ni ule wa Mzee Mwanjoli’. Unashangaa nini? Kila kizuri kina kizuri zaidi yake…”
Haya ni maelezo mafupi niliyowahi kuyasoma mahala fulani, japo yalikuwa yameandikwa kwa namna ya kichekesho lakini kwangu yalikuwa na mantiki na yalinifikirisha sana.
Sifa na ubora wa mchele wa Kyela nilikuwa nimezisikia kabla lakini nilikuwa nashangaa kwa nini tunashindwa kuulinda mchele huu ili usipoteze ubora wake, na tusipoangalia nchi jirani wanaweza ‘kutupiga tena bao la kisigino’ kama ilivyotokea kwenye madini ya tanzanite, Mlima Kilimanjaro, mchoro wa Tingatinga n.k.
Kimsingi, Tanzania tunavyo vitu vingi vizuri ambavyo huwezi kuvikuta sehemu nyingine kama Chipsi zege (chakula ambacho hupikwa kwa mchanganyiko wa viazi mbatata vilivyokatwa vipandevipande vikikaangwa kwa mafuta pamoja na mayai), Mlima Kilimanjaro, Mbuga ya Serengeti, Bonde la Ngorongoro, madini ya tanzanite, vyura wa Kihansi n.k. lakini cha kusikitisha, hadi sasa tumeshindwa kuvitangaza au kuviwekea ulinzi wa kisheria ambao huitwa Miliki Bunifu (Intellectual Property) ili visitumiwe ovyo na kuwafaidisha wasiostahili, jambo linalokatisha tamaa. Sijajua tatizo ni nini?
Kwa kifupi, Tanzania ni nchi iliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu kuwa na rasilimali asilia zisizo na mfano duniani, ukiacha rasilimali nilizoorodhesha hapo juu pia tuna korosho za Mtwara (korosho bora zaidi duniani na huzalishwa kipindi ambacho nchi nyingine hazizalishi), zabibu za Dodoma (nene na zenye sukari nyingi kulizo zabibu zinazozalishwa nchi nyingine duniani), vyura wa Kihansi (wanaishi kwenye maji yanayotiririka na kutoa mvuke mwingi sana kutokana na nguvu ya maji), simba wa Ngorongoro (wanaopanda juu ya miti), hifadhi ya Gombe (yenye sokwe wanaoishi kama binadamu), mchele wa Kyela n.k.
Aidha mengi yamekwisha andikwa kuhusu utajiri wa Tanzania, hasa kuhusu rasilimali na vivutio asilia. Lakini mengi yaliyoandikwa yametokana na mtazamo wa wageni wanavyoiona Tanzania.
Kama nilivyodokeza kuhusu rasilimali asilia zisizo na mfano duniani tulizo nazo, mchele wa Kyela ni moja ya rasilimali asilia za kujivunia sana katika nchi hii (japo sina uhakika kama wengi tunalitambua hili), mchele huu unasifika kwa ubora wake ingawa kwa hali inayoendelea sasa huenda ukapoteza ubora wa kuingia kwenye soko la kimataifa kutokana na hatari inayotokana na kupakwa mafuta (na wafanyabiashara wasio waaminifu) kwa lengo la kuuongezea mvuto.
Hata hivyo, taarifa za Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) zinaeleza kuwa mchele wa Kyela unaaminika kuwa bora zaidi na una upekee fulani ukilinganisha na michele mingine duniani. FAO mwaka 2015 lilieleza kuwa mchele wa Kyela ndiyo unaofahamika kuwa bora zaidi Tanzania ukifuatiwa na ule unaotoka wilaya nyingine za Mkoa wa Mbeya.
Mchele wa Kyela una ladha nzuri na unanukia kutokana na uwepo wa kemikali inayoitwa 2-acetyl-1-pyrroline (C6H9NO) ambayo pia kiasili hupatikana katika mchele wa basmati unaotoka nchini India. 2-Acetyl-1-pyrroline ni kemikali inayojitokeza yenyewe kwenye mchele wa Kyela (kama ilivyo kwa basmati wa India) kutokana na hali ya hewa ya baridi na udongo wenye rutuba unaochangia ukuaji wa taratibu wa nafaka hii, huufanya mchele huu kunukia zaidi, kung’aa na kutoa punje ndefu zilizonyooka. Pia Wilaya ya Kyela ina mvua zaidi ya wastani wa milimita 2,500 kwa mwaka tofauti na maeneo mengine yanayopata mvua kidogo.
Kwa kawaida kemikali ya 2-Acetyl-1-pyrroline huufanya mchele kujitengenezea manukato yake, ingawa mchele mwingine kemikali hii huzalishwa wakati wa mchakato wa usindikaji, kama ilivyoripotiwa katika tafiti kadhaa (mfano kwenye mchele wa jasmine unaopatikana nchini Thailand).
Katika udodosi wangu wakati naulizia kama tumeshausajili mchele huu kwa ajili ya hakimiliki, mtaalamu mmoja aliniambia kuwa hadi sasa anashangaa kwa nini bado tumelala wakati kemikali ya 2-acetyl-1-pyrroline inayopatikana katika mchele wa Kyela ina kiwango mara 12 zaidi kuliko aina nyingine za mchele. Hata hivyo, aliniambia jambo hili linahitaji zaidi utafiti wa kitaalamu kulithibitisha ili tuweze kuupa mchele wa Kyela utambulisho (nembo) wa kimataifa na thamani inayostahili na kuuingiza kwenye soko la kimataifa, kama ambavyo Wahindi wameweza kufanya kwa mchele wa basmati.
Tungeweza kuitumia hali ya kijiografia ya ulimaji mchele wilayani Kyela (geographical indication) kuufanya mchele wa Kyela uwe maarufu kama ilivyo kwa basmati unaolimwa nchini India.
Nchi ya India imefanikiwa kwenye mchele wa basmati, na kuanzia mwaka 2014, nchi hiyo iliweza kuuza nje asilimia 59 ya soko la nje ya nchi la mchele wa basmati, hii ni kwa mujibu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Kilimo na Usindikaji Mazao ya Chakula yanayosafirishwa Nje ya India (IAPFPEDA).
Pia yapo machapisho yanayodai uwepo wa ufumwele (fibre) kwenye mchele wa Kyela kwa asilimia 20 zaidi ikilinganishwa na aina nyingine zaidi ya mchele. Pia habari zisizothibitishwa zinaeleza kuwa, mchele wa Kyela una kiwango cha ‘wastani’ cha kemikali aina ya glycemic index (kati ya gramu 56 na 69), tofauti na mchele mwingine ambao una kiwango cha juu cha glycemic index kinachofikia gramu 89, hivyo kuufanya mchele wa Kyela kufaa hata kwa watu wanaoishi na ugonjwa wa kisukari.
Hata hivyo, kiwango cha glycemic index kinachosemwa kufaa zaidi kwa watu wanaoishi na ugonjwa wa kisukari ni gramu 55 au chini. Hii ni kwa mujibu wa Chama cha Watu wanaoishi na ugonjwa wa Kisukari nchini Canada (CDA). Glycemic index ni kiwango kinachohusishwa na vyakula vya wanga ambacho huleta athari za wanga huo kwa kupandisha kiwango cha sukari kwenye damu ya mtu.
Katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, vyakula vyenye kiwango cha chini cha kemikali hii vimehusishwa na kupungua kwa hatari ya ugonjwa wa moyo na mishipa, ugonjwa wa kisukari aina ya 2 (kisichotegemea matibabu ya insulin), kiharusi, unyogovu (depression), ugonjwa wa figo, mawe kwenye mfuko wa nyongo, uvimbe kwenye kizazi, na saratani ya matiti, utumbo mpana, tezi dume, na kongosho.
Mchele wa Kyela unasifika sana kwa ubora wake na kuwafanya walaji wa wali mijini kuupendelea mchele huu kwa sababu ya kunukia kwake na ladha yake, ukifuatiwa na mchele unaotoka wilaya nyingine za mkoa wa Mbeya na Morogoro. Watu wengi hupendelea kutumia mchele ambao hauna zaidi ya mwaka mmoja tangu uvunwe, unaong’aa (si uliofubaa) na wenye punje ndefu zilizonyooka, ndiyo maana si ajabu siku hizi wafanyabiashara wa mchele usionukia na kung’aa huupaka mafuta mchele huo na wakati mwingine kuuchanganya katika mchele unaonukia ili upate soko.
Wataalamu wa soko la mchele nchini wanasema kuwa bei ya mchele wa Kyela haiwezi kushuka hata kama ushuru wa mchele unaotoka nje utaondolewa, kwani mchele huu una ubora wa aina yake na ladha ya kipekee. Kwa kulitambua hilo, ndiyo maana kuna wafanyabiashara wa mchele wasio waaminifu hulitumia jina la mchele wa Kyela kama matangazo kwa biashara zao za mchele, hata kama mchele wanaouza siyo wa kutoka Kyela, na hii ni kutokana na ubora wa mchele huo.
Hata hivyo, tatizo lililopo ni kuwa wakulima hawajawekewa miundombinu mizuri ya umwagiliaji na kupatiwa huduma stahiki za pembejeo kama mbegu na dawa za kutibu mimea jambo ambalo kama likitatuliwa wakulima wanaweza kuzalisha chakula kwa wingi. Ni suala tu la kuifanya wilaya hii eneo maalumu la kiuwekezaji na kuupa nembo (branding) mchele huu, huku serikali kwa kushirikiana na wadau wakijenga mfumo imara wa masoko ya mazao nchini.
Shirika la Chakula na Kilimo Duniani linaeleza kuwa mahitaji ya mchele nchini na duniani yanazidi kuongezeka na kuongeza fursa zaidi kwa wakulima. Hivyo, badala ya kuendelea kuingiza nchini mchele wa basmati na aina nyingine, tuwekeze kwenye mchele wa ndani, huku tukiupa thamani na utambulisho mchele wa Kyela kutokana na upekee wake.
0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com

Upvote
8