Date::1/23/2009Ukosefu wa maji : Kero iliyokosa ufumbuzi wa kudumu Dar
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Professa Mark MwandosyaNa Jonas Songora
MALALAMIKO juu ya ukosefu wa maji safi na salama kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam, yamezidi kuwa mengi huku lawama lukuki zikipelekwa kwa Kmpuni ya Maji Safi na Maji Taka jijini Dar es Salaam (Dawasco).
Wakazi wa jiji hili wanaokadiriwa kufikia milioni nne, wamekuwa wakiishi kwa taabu kutokana na ukosefu wa maji safi kuwa tatizo la kawaida kwa kipindi kirefu sasa, huku hatua zinazochukuliwa kumaliza tatizo hilo zikisua sua.
Mara kadhaa Mkurugenzi Mtendaji wa Dawasco, Alex Kaaya, amekuwa akikaririwa akisema kuwa, ukosefu wa maji safi na salama kwa wakazi wa jiji hilo, unachangiwa zaidi na miundo mbinu isiyotosheleza iliyopo sasa.
Anadai kuwa miundo mbinu hiyo imekuwapo kwa miaka takriban ishirini na tano ilioyopita wakati jiji hili likiwa na idadi ndogo ya watu tofauti na sasa ambapo pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watu, jiji hilo linapanuka kwa kasi.
Hali hiyo inachangia baadhi ya watu kujikuta katika maeneo ambayo hakuna kabisa miundo mbinu ya kufikisha maji safi na salama na wakati mwingine bado kunakuwepo na shida ya vyanzo vya maji kuhudumia wakazi wote wa jiji.
Ukweli huu wa mambo unaungwa mkono na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Professa Mark Mwandosya, ambaye anakiri kuwa huduma ya utoaji maji safi kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Pwani, hairidhishi na inatakiwa kuboreshwa.
Prof. Mwandosya anasema kuwa, takribani watu milioni tano wanaoishi katika jiji la Dar es Salaam, Bagamoyo na Kibaha mkoani Pwani, hawafikiwi na huduma ya maji safi na salama.
Hili ni tatizo kubwa, kwani kutokana na tatizo hili idadi kubwa ya watu huathirika kiafya kutokana na maradhi yanayosababishwa na utumiaji wa maji yasiyo safi na salama. Miongoni mwa maradhi hayo ni ugonjwa wa kipindupindu ambao umekuwa wa kawaida masikioni mwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.
"Watu hawa milioni tano ambao ni sehemu ya watu milioni saba wanaoishi katika mikoa hiyo miwili, hawafikiwi na huduma ya maji safi na salama kutokana na miundo mbinu mibovu na isiyoendana na hali halisi ya ukuaji wa idadi ya watu," anasema Prof.Mwandosya.
Anaongeza kuwa, ili kuhakikisha kuwa wananchi walio wengi wanapata huduma nzuri ya maji, Dawasco hawana budi kupanua wigo wake wa miundo mbinu.Kwa kufanya hivyo, watatoa huduma ipasayo kwa wananchi wa mikoa hiyo.
Akionyesha kuwa bado hajaridhishwa na utendaji wa Bodi ya Dawasco, Prof. Mwandosya anasema kuwa muda uliosalia hadi kufanyika uchaguzi mkuu nchini ni mchache, hivyo Bodi ya Dawasco inalo jukumu kubwa kuhakikisha kuwa inatekeleza majukumu yake katika kipindi hiki kifupi.
"Tuna mwaka mmoja na miezi michache tu ili kufikia lengo hilo, hivyo bodi inatakiwa kusoma na kuelewa kwa makini malengo na viashiria vilivyowekwa kwenye mkataba wao, ili waweze kupima utekelezaji wake mara kwa mara," anasema Mwandosya.
Lakini tatizo ni kubwa zaidi ya hapo, kwani imebainika kuwa ukosefu wa maji pia unachangiwa na wafanyakazi wenyewe wa Dawasco ambao wamekuwa mstari wa mbele kufanya vitendo vichafu vilivyo nje ya maadili yao ya kikazi hivyo kudhoofisha utoaji wa huduma bora.
'"Wafanyakazi wanashirikiana na baadhi ya wateja wasio waaminifu katika kuchepusha dira ya maji, wizi wa maji, vitendo kama hivi haviwezi kuwa vinafanywa na wananchi wasiokuwa na utaalamu bali ni wafanyakazi wetu wenyewe kwani wao ndio wenye utaalamu katika sekta hiyo," anaeleza Prof Mwandosya.
Anaongeza kuwa kutokana na hali hii ya uhujumu inayofanywa na wataalamu, athari zake ni kubwa kwani miundo mbinu iliyopo huhujumiwa. Hali hii inasababisha kutolipwa kwa ankara sahihi hivyo kuikosesha Dawasco mapato stahili.
Pia kuna changamoto nyingine ambazo ni kikwazo katika utoaji wa huduma nzuri ya maji kama vile uwezo mdogo wa mitambo ya Ruvu Juu, Chini na Mtoni, huku kukiwepo na uvujaji wa maji kwa asilimia hamsini ya maji yote yanayopatikana.
"Matatizo hayo yanachangia kwa kiasi kikubwa kutofikiwa kwa malengo ya ukusanyaji wa mapato ambacho ni kiasi cha Sh 2.5 bilioni kwa mwezi,"anaeleza.
Mwenyekiti wa Bodi ya Dawasco, Mhandisi Suleiman Suleiman, anasema kuwa vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na wafanyakazi wa Dawasco hadi kufikia kufifisha juhudi za kusambaza huduma za maji ipasavyo kwa wateja wake,vinatokana na wafanyakazi hao kutopewa maslahi mazuri.
"Kampuni imejipanga kutoa maslahi mazuri kwa wafanyakazi wake ili hatimaye wajiepushe na vitendo vya kihalifu. Kwa kufanya hivyo, huduma zetu kwa wateja zitakuwa bora zaidi," anasema Suleiman.
Anasema kuwa mipango mingine iliyopo ni kuhakikisha kuwa wanakabiliana na changamoto zinazochangia ukosefu wa maji kwenye baadji ya maeneo na kudhibiti uvujaji wa maji, wizi wa miundo mbinu na kuongeza upatikanaji wa maji anagalau katika maeneo yote.