Kupitia ukurasa wa JamiiCheck kwenye mtandao wa Instagram mdau ameshukuru kwa elimu kuhusu dawa za meno, lakini pia ametaka kufamu kuhusu vidonge vinavyotajwa kupunguza unene, je kuna utapeli au vinafanya kazi kweli?
- Tunachokijua
- Afisa Tabibu Isack Chelleah anaeleza kuwa Wizara ya Afya haijapitisha dawa za aina hiyo, na kama zipo basi si rasmi kutokana na tafiti rasmi zilizofanyika. "Nadhani wanaotangaza biashara hiyo wengi wao wanafanya kama utapeli, kwani kwa Tanzania hakuna vidonge vya aina hiyo ambavyo ni rasmi kutumika."
Aidha anaongeza kuwa kupunguza unene au uzito kunaweza kufanyika kwa njia nyingine mbalimbali ikiwemo kuwa na ratiba ya mazoezi, kuwa na mpangilio maalum wa chakula kwa maelekezo (diet), kubadili aina ya maisha fulani yanayochangia mhusika kunenepa na vingine vingi.
Kuhusu madhara ya vidonge hivyo anaeleza kuwa mara nyingi inategemea mtu na mtu yaani afya ya mhusika kwa kuwa vidonge au dawa hizo siyo rasmi hivyo madhara yake pia yanaweza kuwa tofauti kutegemea na afya ya mtu.
"Ni kama vile unavyosikia kuna dawa za kuongeza sehemu fulani ya mwili kama vile makalio, matiti kama vinafanyika katika njia zisizo rasmi, madhara yake huwa ni mengi na yanatofautiana."
Tovuti ya BBC News kuhusu vidonge vya kupunguza uzito inabainisha kuwa mapitio ya vifaa vya kupunguza uzito, kwa niaba ya BBC, yalihitimisha kuwa hakuna ushahidi wowote wa kimatibabu uliochapishwa kuunga mkono madai ya kupunguza uzito yanayohusiana na bidhaa nne kati ya tano zilizochunguzwa. Wataalamu walisisitiza kuwa hakuna kidonge kinachoweza kuchukua nafasi ya lishe bora na mazoezi.
Inaelezwa vidonge vya kupunguza uzito au mafuta vinavyouzwa bila agizo la daktari na visivyodhibitiwa kwa kawaida si salama. Mamlaka za afya, zikiwemo U.S. Food and Drug Administration (FDA), zimeonya kuwa bidhaa nyingi za aina hii zinaweza kuwa na viambato visivyotajwa, hazijafanyiwa majaribio ya kutosha, na zinaweza kusababisha madhara makubwa kiafya.
Mamlaka hiyo inaengeza kuwa bidhaa nyingi zinazodai kusaidia kupunguza uzito kama vidonge vya lishe, vidonge vya kuchoma mafuta, na virutubisho au chai za kupunguza uzito huenda zikawa na viambato hatari vilivyofichwa. Bidhaa hizi zilizochafuliwa ni aina ya ulaghai wa dawa unaohusiana na afya.
Mara nyingi hutangazwa kimakosa kama virutubisho vya lishe, vyakula, au tiba za asili, na huweza kuwa na maoni mengi chanya ya uongo au kusambazwa kupitia mitandao ya kijamii. Bidhaa hizi zinaweza kuhatarisha afya kwa kiwango kikubwa, hazihakikishi matokeo, na zinaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya au hata kulazwa hospitalini. Pia huuzwa mtandaoni na katika maduka mbalimbali.