Meli 2 za Mafuta zilizokuwa zikielekea Kenya zapigwa na drones 'Strait of Hormuz'

Meli 2 za Mafuta zilizokuwa zikielekea Kenya zapigwa na drones 'Strait of Hormuz'

Wakaguongo

Member
Joined
Sep 23, 2026
Posts
95
Reaction score
38
Kenya huenda ikakabiliwa na ucheleweshaji wa usafirishaji wa mafuta baada ya meli mbili zilizokuwa zimebeba bidhaa za petroli kuelekea nchini kupigwa na ndege zisizo na rubani (drones) katika Strait of Hormuz, njia muhimu ya baharini inayounganisha Ghuba ya Uajemi na Ghuba ya Oman.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli (EPRA), Edward Kinyua, alifichua hayo alipofika mbele ya Kamati ya Bunge la Kitaifa inayoshughulikia Hesabu za Special Funds.

Kwa mujibu wa Kinyua, mashambulizi hayo yalitokea katika kipindi cha kuongezeka kwa mvutano kati ya Iran na Saudi Arabia, huku meli zinazohusishwa na Saudi Arabia zikidaiwa kulengwa.

Alieleza kuwa mashambulizi hayo yaliharibu injini za meli hizo na kuzifanya zishindwe kuendelea na safari, lakini mafuta yaliyokuwa ndani yake hayakuharibiwa. Hata hivyo, kuhamisha shehena hizo hadi kwenye meli nyingine si jambo la haraka. Kinyua alisema mchakato huo unaweza kuchukua takribani siku 60, jambo linaloweza kuchelewesha kuwasili kwa mafuta yaliyokuwa yamekusudiwa kwa soko la Kenya.

Kinyua alisema Serikali inategemea mfumo wa makubaliano ya serikali kwa serikali (G-to-G) na wasambazaji wa mafuta kutoka Saudi Arabia kulinda usalama wa usambazaji nchini.

Hata hivyo, tukio hilo linaibua maswali kuhusu athari za mivutano ya Mashariki ya Kati kwa nchi zinazotegemea uagizaji wa mafuta kutoka nje, ikiwemo Kenya. Kwa sasa, taarifa ya mashambulizi haya haimaanishi moja kwa moja kuwa Kenya itakabiliwa na uhaba wa mafuta, lakini ucheleweshaji wa shehena unaweza kuleta changamoto iwapo hautadhibitiwa kupitia mipango mbadala ya usambazaji.

Ufichuzi huo unakuja siku chache baada ya EPRA kutangaza bei mpya za mafuta zilizoanza kutumika Oktoba 15 hadi Novemba 14, 2026. Bei ya lita moja ya petroli ilipanda kwa shilingi 12.33, dizeli kwa 9.90, huku mafuta ya taa yakipanda kwa 28.49. EPRA imehusisha shinikizo la bei na kupanda kwa gharama za mafuta katika soko la kimataifa, miongoni mwa sababu nyingine.

Sasa, japokuwa Serikali inasema mpango wa G-to-G unalinda usambazaji wa mafuta. Lakini iwapo mivutano ya Mashariki ya Kati itaendelea na shehena zikachelewa, unadhani Kenya ina mipango mbadala ya kutosha kuzuia athari kwa Wananchi na biashara, au tunapaswa kujiandaa kwa changamoto zaidi za bei ya mafuta?

Je, bei ya mafuta itimiapo November itakuwaje? Tuna sababu ya kuwa na hofu zaidi?
 

Attachments

  • 1778.jpeg
    1778.jpeg
    42.1 KB · Views: 13
Back
Top Bottom