• Ahofiwa kulenga nafasi ya kisiasa 2010
na Mwandishi Wetu
HATUA ya Mwenyekiti wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi, kutangaza kuwa ni mwanachama wa CCM pamoja na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii, akiwa na wabunge waliojipambanua kuwa ni wapambanaji wa ufisadi, imezidisha hofu na mgawanyiko ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Uchunguzi wa Tanzania Daima Jumapili pamoja na mahojiano ya baadhi ya makada wa chama hicho, vimebainisha hofu iliyoanza kuingia ndani ya chama hicho katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwakani.
Mmoja wa makada aliyezungumza na Tanzania Daima Jumapili kwa sharti la kutotaka jina lake liandikwe, alisema baadhi ya wabunge, hasa walio kambi tofauti na ile ya wapambanaji wa ufisadi, wanaona hatua hiyo ni mapambano ya wazi kati ya kambi hizo ambazo hivi sasa zimekuwa zikiwindana na kushutumiana kwa kificho na hadharani.
Anabainisha kuwa kujitokeza hadharani kwa Mengi na kuanza kuzunguka na baadhi ya wabunge, ambao hivi sasa wamejipatia umaarufu kwa madai ya kupambana na ufisadi, kumezidi kuleta mgawanyiko, maana baadhi ya wanachama wanaona hali hiyo inakidhoofisha zaidi chama badala ya kukijenga.
Chanzo hicho kimedokeza kuwa Mengi amekuwa mhimili mkubwa wa baadhi ya wabunge, ambao hivi sasa wamekuwa na wakati mgumu katika majimbo yao, kutokana na kile kinachodaiwa baadhi ya watu kupandikiza watu wao ili wawang'oe katika uchaguzi mkuu.
Miongoni mwa wabunge wanaodaiwa kukabiliana na hali ngumu katika majimbo yao ni Fred Mpendazoe (Kishapu), Christopher ole Sendeka (Simanjiro), Lucas Selelii (Nzega), na wengineo ambao tangu kutokea kwa kashfa ya Richmond wamekuwa wakitembea kifua mbele.
Baadhi ya makada wa CCM wamekuwa wakihusisha juhudi hizo za Mengi na kuwania uongozi wa siasa, licha ya Mengi mara kadhaa kuelezea dhamira yake ya kutotaka kuwania uongozi wowote wa kisiasa hapa nchini, kwa madai kuwa yeye ni mfanyabiashara asiyependa kuingia katika ulingo wa kisiasa.
Mengi alikuwa akihusishwa na kuwania urais, hasa baada ya serikali kubwagwa katika kesi ya kupinga kuruhusiwa kwa mgombea binafsi katika nafasi ya urais.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaainisha kuwa mbali na mfanyabiashara huyo kuzusha hofu na mgawanyiko katika chama hicho tawala, amesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza kushughulikiwa kwa wabunge waliopo mstari wa mbele katika mapambano ya ufisadi.
Wanaeleza kuwa uungwaji mkono anaoupata mfanyabiashara huyo na kundi la wabunge analoliunga mkono kutoka kwa wananchi, ndiyo imekuwa silaha kubwa kwa viongozi wakubwa wa CCM kuwashughulikia wabunge wao kwa hofu ya kukosa kura.
Wachambuzi hao wanasema kitendo cha baadhi ya wanachama kujadili na kutaka kadi ya mfanyabiashara huyo aliyoikata hivi karibuni isikubaliwe na chama, lilikuwa ni jaribio muhimu la kuonyesha nguvu ya mfanyabiashara huyo ndani na nje ya chama.
Wanabainisha kuwa hatua ya mfanyabiashara huyo kutangaza wazi kuwa yeye ni mwanachama wa chama hicho tangu mwaka 1977, na alichukulia kadi katika Tawi la Kisutu, Dar es Salaam, iliwachanganya viongozi wengi waliokuwa wakimuona kuwa ni miongoni mwa wafadhili na wanachama wa upinzani.
Wanasema makada waliokuwa wakitaka kadi ya mfanyabiashara huyo isitambulike, walikosa nguvu pale uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam ulipotoa taarifa ya kumtambua Mengi, jambo lililotafsiriwa kuwa ni maagizo kutoka ngazi za juu za chama.
Wakati baadhi ya wanachama wa CCM, wananchi na wapinzani wakishangazwa na kutafakari hatua ya Mengi kutangaza hadharani uanachama wake, mfanyabiashara huyo ameamua kuhamisha uanachama wake kutoka Tawi la Kisutu, Dar es Salaam, kwenda Mkoa wa Kilimanjaro.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kilimanjaro, Jonas Semu, ndiye aliyetoa taarifa za kumpokea Mengi, huku Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuph Makamba, akiiambia Tanzania Daima kuwa utaratibu wa kuhamisha uanachama ni wa kawaida na kila mwanachama anayo haki ya kufanya hivyo.
"Huo ni utaratibu wa chama na hata mimi nilipokuwa mkuu wa mkoa nilihamisha uanachama wangu kutoka Kivukoni kwenda Mikocheni, na baadaye nilitaka kuishi katika nyumba yangu mwenyewe nikahamishia tena uanachama wangu huko Tegeta.
"Kama hutahamisha uanachama wako ina maana huwezi kupiga kura za maoni, na ukitaka kugombea ubunge ni lazima uwe mwanachama wa eneo hilo," alisema Makamba.
Wadadisi wa masuala ya siasa wanaweka wazi kuwa ufafanuzi huo wa Makamba na hatua ya Mengi huenda ndiyo ikawa ishara ya mfanyabiashara huyo kuingia katika medani ya kisiasa badala ya kuendelea kuwasaidia baadhi ya wabunge.
Wanabashiri kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ndani ya CCM utakuwa mgumu, kwa kuwa ufa wa kutokuelewana kwa makundi ndani ya chama hicho, umezidi kushamiri na kuingia kwa Mengi kumeongeza chachu ya ugumu.
Aidha, wachambuzi hao wanabainisha kuwa huenda pia hofu ya baadhi ya wanachama ikawa sahihi kuwa Mengi ana lengo la kugombea nafasi ya kisiasa ili apambane na baadhi ya wanasiasa wanaotuhumiwa kwa ufisadi, lakini bado wanaendelea kuwa wawakilishi wa wananchi na chama.
SOURCE:
http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=10339