Makamba adai ana miaka mnne ya kuishi ambao afe kwa amani, azikwe kwa heshima
Na Joyce Mmasi
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amewaomba watu wanaomfuatafuata kumuacha ili afe kwa heshima kutokana na kubakiza miaka michache ya kuishi duniani.
Makamba alitoa kauli hiyo juzi alipozungumza kwenye mahafali ya wanafunzi wa Shule za St Anne Marie eneo la Mbezi kwa Msuguli jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Aliwataka watu wasiomtakia mema kuacha kumfuatafuata na badala yake waachwe afe kwa heshima kwa kuwa amebakia miaka minne afikishe umri wa kuishi duniani.
Akinukuu vifungu kwenye Biblia , Makamba alisema umri mtu kuishi duniani ni miaka 70 na wachache ni 74 na akasema yeye amefikisha umri wa miaka 71, hivyo anapaswa aachwe amalizie miaka mine iliyosalia ili azikwe kwa heshima.
“Mimi nina miaka 71 sasa, nimebakiza miaka mine tu nife, lakini kuna watu wananifuata ooh Makamba kafanya hivi, wanataka kuniharibia bure, kwanini wasiniache nife nizikwe kwa heshima†alisema Makamba na kuwaacha watu wakiangua kichezo.
Akizungumzia utendaji kazi kwa walimu nchini, Makamba aliwataka kuongeza upendo kwa watoto wanaowafundisha ili kuweka kichocheo kwa wanafunzi wapende kusoma na kuwa na bidii katika masomo.
Makamba alisema, walimu ni watu muhimu wanaoweza kudumaza au kupandisha kiwango cha kufaulu kwa wanafunzi na kwamba penye upendo pana elimu, na mwalimu mzuri ni yule anayeonyesha upendo kwa wanafunzi na kwa masomo anayofundisha.
Katibu Mkuu aliwakumbusha walimu nchini kwamba wanafunzi wengi ni vijana na ni taifa la kesho na akasema kwa kuwalea katika maadili ya kupenda kusoma ni kusaidia kujenga taifa imara lenye wasomi wengi na wazuri.
Alilaumu tabia ya baadhi ya walimu wanaogoma kufundisha akisema mwalimu anapogoma kufundisha asifikiri anamgomea mwajiri wake au serikali na badala yake wajue kuwa wanawagomea watoto hao.
Awali akizungumza wakati akimkaribisha, Mkuu wa shule hizo Nelson Theonest alisema wanafunzi wote waliomaliza shule waliandaliwa vizuri na wote wapo tayari kujiunga na shule zingine kila mmoja kwa kiwango chake na akawapongeza wanafunzi wote kwa adabu na utii walioonyesha shuleni hapo kwa muda wote waliokuwa wakisoma. Katika mahafali hayo, jumla ya wanafunzi 359 wadarasa la saba, kidato cha nne na cha sita, walimaliza shule na kukabidhiwa vyeti vyao.