Serikali yaogopa ufisadi Meremeta
Uchunguzi wabaini madudu ya ajabu
MWANDISHI WETU
Dar es Salaam
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Polisi kwa muda mrefu sasa wamekusanya ushahidi wa kutosha kuhusiana na watu wanaokabiliwa na kashfa ya rushwa ya Meremeta.
Haya yamejulikana sasa pamoja na serikali kusita kuchukua hatua dhidi ya waliohusika na matumizi tata ya zaidi ya bilioni 155/- kupitia kampuni hiyo tata ya uchimbaji dhahabu ya Meremeta Limited.
Uchunguzi wa muda mrefu wa KULIKONI umebaini kwamba, kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2006, vyombo vya dola ikiwamo Idara ya Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi na Takukuru, vimekuwa vikiichunguza Meremeta na wahusika wote walioguswa na kampuni hiyo.
Habari za uhakika zinaeleza kwamba Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (CID), yalianza upelelezi ulioongozwa na SSP Ernest Sakawa Mei, 2006.
Vyanzo vyetu vimeeleza kuwa katika upelelezi huo ushahidi wa kutosha kuhusu kampuni tata ya Meremeta ulikusanywa.
Habari zinaeleza kwamba baadaye mwaka 2007, Takukuru nao waliendelea na upelelezi wao ulioongozwa na Ofisa Mwandamizi wa taasisi hiyo, Dunia Kaongo, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Uchunguzi, akichukua nafasi ya Edward Hoseah, aliyepanda na kuwa Mkurugenzi Mkuu.
Vyanzo vya habari vinaeleza kwamba uchunguzi wa polisi ulikwenda mbali hadi mkoani Mara, ambako walishirikisha maofisa wa polisi mkoani humo uliko mgodi wa Buhemba, uliokuwa ukiendeshwa na Meremeta kabla ya kufilisiwa kiaina na kazi zake kuendeshwa na kampuni nyingine tata ya Tangold Limited.
Hata hivyo, haijafahamika mara moja hatua zilizofikiwa na wachunguzi hao wa vyombo vya dola, pamoja na kutolewa kwa kauli tata kuhusiana na makampuni hayo na mgodi wa Buhemba, ambao kwa sasa umefungwa.
Kampuni ya Meremeta inatajwa kuwa kampuni iliyokomba zaidi ya bilioni 155/- kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kiwango kinachozidi bilioni 133/- zilizochotwa kupitia Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).
Serikali imeunda timu kuchunguza upotevu wa fedha za EPA, chini ya uongozi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, akisaidiwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Saidi Mwema na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Hoseah, lakini haijasema lolote kuhusu Meremeta.
Tayari Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali Ludovick Utouh, ametamka kwamba ofisi yake haiitambui Meremeta kama kampuni ya umma kwa kuwa haijawahi kukaguliwa, huku baadhi ya viongozi wa serikali wakiwamo mawaziri wakidai kwamba ni ya umma.
Habari zinaeleza kwamba Meremeta iliweza kuchota kiasi kikubwa cha fedha kutokana na shinikizo na baraka zote za Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, ambaye anatajwa moja kwa moja kuihalalisha kampuni hiyo alipokuwa madarakani.
Utuoh katika maelezo yake yaliyonukuliwa katika vyombo vya habari, alisema ofisi yake haijawahi kukagua hesabu za Meremeta Limited huku kampuni hiyo tata ikiwa haimo katika orodha ya makampuni yanayomilikiwa na serikali ama serikali kuwa na hisa.
Aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Matern Lumbanga amewahi kuandika barua kwenda benki moja ya Uingereza, ikieleza kwamba Mkapa kupitia kikao cha Baraza la Mawaziri mwaka 2000, alitoa idhini ya kuanzishwa kwa shughuli za uchimbani dhahabu katika eneo la Tembo na Buhemba, mkoani Mara.
Katika barua hiyo ya Lumbanga, Ikulu ndiyo iliyobeba jukumu la kuithibitisha na kuitambulisha kampuni ya Meremeta kwa Deutch Bank AG London, iliyoko nchini uingereza kwa nia ya kupata mkopo wa uendeshaji wa mgodi wa dhahabu wa Buhemba ambao kwa sasa umefungwa.
Tunathibitisha kwamba tunafahamu kuwapo kwa hazina kubwa ya dhahabu nchini Tanzania ambayo haijalinufaisha taifa na serikali kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, ilianzisha mradi wa Meremeta ikiwa na malengo ya kununua dhahabu kwa wachimbaji wadogo.
Baadaye mwaka 2000, Rais (Mkapa) kupitia Baraza la Mawaziri aliazimia uchimbaji mkubwa wa chini ya ardhi katika eneo la Tembo na uchimbaji mwingine wa kawaida katika eneo la Buhemba, kaskazini mwa Tanzania, inaeleza barua hiyo iliyosisitiza kwamba mradi huo utakua na manufaa kwa taifa.
Barua hiyo inataja kampuni ya Nedcor Trade Services Limited ya Afrika Kusini kuwa ndiyo iliyotoa mkopo wa fedha za kuanzishia mradi huo chini ya usimamizi wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, iliyokua inatajwa sana kuwa mmiliki wa mgodi huo hapo awali kabla ya kubainika kuwapo kwa utata mkubwa.
Pamoja na Utouh kuikana Meremeta, kuna taarifa kwamba serikali ya Mkapa kupitia Msajili wa Hazina ilitoa cheti ya kuithibitisha Meremeta kuwa kampuni ya umma tokea Oktoba mosi, 1997 baada ya kudaiwa kwamba serikali ilikua na hisa katika kampuni hiyo.
Hisa zilizodaiwa kuwa za serikali zilikabidhiwa kwa waliokua watendaji wakuu serikalini, ambao hata hivyo hadi sasa wanaendelea kuzishikilia baada ya baadhi yao kuondolewa ama kubadilishwa nafasi zao.
Habari zaidi zinaeleza kwamba watendaji wakuu ndani ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Wizara ya Ulinzi na JKT, walipata hisia za kuwapo kwa mikono michafu katika mradi wa Meremeta na hivyo kutoa ushirikiano mkubwa kwa wenzao wanaochunguza sakata hilo.
Sakata la Meremeta limeelezwa kuweza kuwa kubwa na zito zaidi kutokana na maelezo ya uwezekano wa kuwapo wahusika wanaofahamika duniani katika biashara chafu na hivyo kuibua mjadala mwingine mkubwa utakaovuka hadi mipaka ya Tanzania.
Kwa mujibu wa habari hizo, uchunguzi unaweza kwenda mbali kutokana na kampuni ya Nedcor Trade Services Limited ya Afrika Kusini, kuonekana kuwa na uhusiano na benki ya Nedbank ya Afrika Kusini ambayo sehemu ya fedha hizo zilielekezwa huko, zikitokea BoT, huku baadhi ya wakurugenzi wa kampuni nyingine tata ya Deep Green Finance Limited wakiwa watumishi wa benki hiyo maarufu ya Afrika Kusini.
Deep Green Finance Limited ni kampuni iliyosajiliwa nchini na baadaye kupokea fedha kutoka BoT, kabla ya kufilisiwa bila ya kuwapo maelezo ya kutosha ya madhumuni hasa ya kuanzishwa kwa kampuni hiyo katika kipindi ambacho nchi ilikuwa inaelekea katika uchaguzi mwaka 2005.
Kashfa hiyo ya Meremeta inaelezwa kuwa zaidi ya ile ya EPA kutokana na kuwa uwezekano wa kurejesha fedha hizo ni mdogo kutokana na kuingia katika mkondo unaoihusisha zaidi Serikali yenyewe na watendaji wake wakiwahusisha wafanyabiashara wa kimataifa.
Baadhi ya wakurugenzi wa Kampuni ya Meremeta ambao wanaelezwa kuwa katika nafasi hizo kutokana na nyadhifa zao bado wanaendelea kushikilia hisa hizo akiwamo Gavana wa zamani wa Benki Kuu, Dk. Daudi Ballali, ambaye ajira yake ilisitishwa na Rais Jakaya Kikwete na Andrew Chenge, aliyejiuzulu uwaziri hivi karibuni.
Fedha hizo ambazo zilibadilishwa na kuwa Dola za Marekani 131,736,628.73 kwa maelekezo yaliyotolewa Desemba 20, 2005, siku moja kabla ya kuapishwa kwa Rais Jakaya Kikwete, zilifanyiwa uhamisho kwenda Afrika Kusini na kuingizwa Nedbank, na nyingine kuingizwa katika akaunti za kampuni ya Tangold na Meremeta.
Taarifa za wakaguzi zinaonyesha kwamba baada ya ununuzi huo wa dhamana, Benki Kuu ilizibadilisha sehemu ya dhamana hizo kuwa dola za Marekani 118,396,460.36 ambazo zilipelekwa kwenye akaunti moja isiyojulikana ya Nedbank Ltd. ya Afrika Kusini, benki hiyo ikiwa imezipokea fedha hizo kupitia HSB Bank ya New York, Marekani zikitajwa kuwa malipo ya madeni ya kampuni mufilisi ya Meremeta Ltd.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba sehemu nyingine ya fedha hizo zipatazo Dola za Marekani 13,736,628.73 zililipwa kwa kampuni ya Tangold kwenye akaunti ya kampuni hiyo iliyoko Benki ya NBC Corporate Branch, Dar es Salaam.
Mwaka jana Mbunge wa Karatu Dk. Willibrod Slaa (Chadema), aliliingiza suala hilo katika hoja yake iliyokuja kugonga mwamba.
Katika hoja yake hiyo, Dk. Slaa alibainisha kwamba Meremeta Ltd. ni kampuni binafsi ya kigeni iliyoandikishwa Agosti 19, 1997 katika kisiwa cha Isle of Man nchini Uingereza na kupewa namba ya usajili 3424504, ikimilikiwa na Triennex (PTY) LTD ya Afrika Kusini yenye asilimia 50 ya hisa za kawaida na Msajili wa Hazina (Treasury Registrar) akiwa na asilimia 50.
Kwa upande wa Tanzania, Dk. Slaa alisema Meremeta ilipewa Hati ya kutimiza masharti (Certificate of Compliance) Oktoba, 1997 lakini akasema kwamba Meremeta ilifilisiwa Uingereza Januari 2006.
Hata hivyo, Dk. Slaa ameeleza kwamba pamoja na kampuni hiyo kufilisiwa nchini Uingereza, hakuna ushahidi kuwa kwa upande wa Tanzania kampuni hiyo imefilisiwa au la kutokana na kutajwa katika marejeo mbalimbali kuwa moja ya makampuni yanayozalisha dhahabu.
Taarifa na takwimu muhimu kuhusu Sekta za Nishati na Madini, ya Julai, 2007, inaonyesha kuwa Meremeta bado inafanya kazi, na inazalisha tani 2.27 za dhahabu. Kama Serikali inasema Meremeta imefilisiwa na mali zake kuhamishiwa Tangold hali hii inaelezwa vipi? Taarifa hizi za utata zinaashiria nini? alihoji Dk. Slaa.
Maelezo mengine yanayoibua utata zaidi na ambao Kamati ya Rais inayopitia mikataba ya madini itapata wakati mgumu kuitolea taarifa ni kuhusu Meremeta kudaiwa kuwa ni kampuni iliyoanzishwa kwa lengo la kusaidia JWTZ, Kikosi cha Nyumbu wakati ikiwa imeandikishwa nchi ya kigeni.
Taarifa ya awali ya wakaguzi waliokagua BoT, Juni 2006, ziliibua sakata hilo la Meremeta pamoja na kashfa nyingine lakini haikuweza kufahamika ripoti hiyo ya wakaguzi ilivyoyeyuka na kutoanikwa hadharani kabla ya wakaguzi wengine wa nje kuibua suala la EPA pekee miongoni mwa uchafu mwingi ndani ya BoT na serikalini.
Taarifa hiyo ya wakaguzi ilibainisha kwamba serikali ilitoa fedha hizo kiasi cha Sh. bilioni 155 kwa njia ya dhamana ya hazina ambayo inatakiwa kulipiwa riba ya asilimia 14.92 kila mwaka lakini hakukua na makubaliano yoyote rasmi kati ya Serikali na Meremeta hali inayoibua zaidi utata na kuonyesha hakuna njia yoyote ya kuweza kuzipata fedha hizo.
Ndani ya BoT bado kuna mianya mingi ambayo huenda ikaendelea kuibuka siku hadi siku hususan baada ya Bunge kuonyesha njia kwa kushughulikia sakata la umeme wa dharura uliokabidhiwa kwa kampuni ya Richmond Development LLC ya Marekani, sakata lililosababisha kuanguka kwa mawaziri watatu akiwamo aliyekua Waziri Mkuu, Edward Lowassa.