Hii imetoka kwenye Gazeti la Mtanzania Kuna Paragraph huko Chini imenifurahisha , aliwapa Waandishi 40thou kila mmoja kuwasaidia kurudi nyumbani
Londa azungumza
na beatrice moses
MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Alhaji Salum Londa, ameibuka na kudai kuwa tuhuma zote zinaripotiwa kwenye vyombo vya habari dhidi yake zinalenga kumdhalilisha.
Meya Londa alitoa madai hayo jana, alipozungumza na waandishi wa habari kutoka katika vyombo mbalimbali vya habari nchini, kwenye Ukumbi wa Manspaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, Londa alisema amesikitishwa na kuchapishwa kwa kwa tuhuma hizo, kwa sababu hazina uthibitisho, na zinaweza kuleta madhara makubwa katika jamii.
Alidai kuwa, chini ya uongozi wake, Manispaa ya Kinondoni, ni moja ya manispaa ambazo zimeongoza kwa utawala bora.
Akizungumzia kuhusu tuhuma za gari ambalo alikuwa akilitumia awali, alidai kuwa siku zote anayejua ubovu wa gari ni dereva, na ndiye aliyetoa taarifa za ubovu wa gari hilo, ambalo ni kweli lilitengenezwa kwa Sh milioni 9, lakini kwa kufuata utaratibu wote unaostahili kiutendaji.
"Mimi nafikiri hapo cha kuangaliwa ni kwamba fedha zilizotumika kugharamia matengenezo ya gari hilo zilitolewa vipi? Zilifuata utaratibu unaokubalika, na gari halikupelekwa kutengenezwa kwenye gereji ya Londa, kwa hiyo zikaingia kwenye mfuko wake.
"Hapo labda kungekuwa na jambo la kuhoji, nilifikiri kwamba ningeonewa huruma, walitaka kuona Meya anatembea kwa miguu, maana gari lingine lililoagizwa lilichelewa kufika," alisema Alhaji Londa.
Alisema, anashangaa kuandikwa kwamba alitaka kulinunua gari hilo kwa Sh milioni 3, wakati yeye alitaka kulinunua kwa milioni 3.5. kwenye zabuni, hata hivyo alikiri kushindwa kwenye zabuni hiyo, ambayo alishinda mtu aliyetajwa kuwa ni A. S .Mohamed kwa Sh milioni 14,200,000.
"Mimi nashangaa sana jamani ndugu waandishi, zabuni hiyo sikuomba peke yangu, hata Mkuu wa Mkoa, Abass Kandoro, aliomba, ingawa yeye alitaka kununua Isuzu Tipper, lakini hakufanikiwa kupata, hii yote nawathibitishia kuwa Kinondoni kuna utawala bora, maana isingekuwa hivyo, angepewa bila taratibu za zabuni kufuatwa, na bila hata kuangaliwa kiasi chake cha pesa ambacho kilikuwa Sh milioni 3." alisema Londa.
Meya Londa pia alikanusha kutumia madaraka yake vibaya kutaka kumpeleka Amina Salehe Londa, ambaye ni mtoto wake Marekani, kwa kumjumuisha katika orodha ya madiwani vijana waliokuwa wamealikwa jijini Florida, mwaka jana na Taasisi ya Sister City International.
"Mimi nina watoto 12, wa kike sita, na wakiume sita, kati yao wengi wanaishi huko tangu mwaka 1996, Amina siyo mtoto wangu, ila ni kweli nilimchagua kwa sababu kwa nafasi yangu naruhusiwa kuchagua madiwani wawili.
"Sijakatazwa kuchagua hata mwanangu, ili mradi awe na sifa zinazostahili, hivyo nilimchagua huyo pamoja na mwanangu Haji Londa, lakini gharama za safari hazikutolewa na manspaa, bali walijigharamia wenyewe, ingawa Amina hakufanikiwa kupata visa," alifafanua.
Pia alikanusha kuiuzia Manispaa kompyuta, akidai kuwa hajawahi hata kuiuzia kalamu achilia mbali hizo kompyuta ndogo (laptop) 20, ambazo alidaiwa kurejea nazo kutoka Marekani kwenye safari hiyo ya madiwani vijana. Ilidaiwa kuwa, aliuza kila kompyuta kwa Sh milioni 3, bei ambayo ni kubwa ikilinganishwa na iliyopo kwenye soko.
"Sijawahi kuuza hata penseli kwa Manispaa, ingawa pia sizuiwi kurejea na kitu chochote halali na kukiuza, ili mradi tu natakiwa kufuata taratibu zilizowekwa," alisisitiza.
Akizungumzia kuhusu mgogoro wa kiwanja namba 965, Meya Londa ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kawe, alikanusha vikali kuhusika na uuzwaji wa kiwanja hicho, ambacho alisema kuwa kilikuwa ni mali ya Kiwanda cha Tanganyika Packers, na kilipimwa mwaka 1996.
"Kiwanja hicho kimeanza kuwa na mgogoro tangu miaka ya 1990, ambapo kuwa wakati ambapo Mkuu wa Wilaya alikuwa ni Hawa Ngulume alipokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa Kiislamu kuwa wameamua kuvamia na kujenga msikiti kwenye kiwanja hicho.
"Kwa sababu tayari kuna makanisa matatu yamejengwa katika eneo hilo, lakini hakuna hata msikiti, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya iliamua kusimamisha ujenzi wa msikiti huo ambao ulikuwa kwenye linta, na kuamuru wavamizi hao wafuate taratibu za kuomba kiwanja hicho," alisema.
Alisema, hivi sasa kiwanja hicho kinamilikiwa kihalali na Waislam hao baada ya kufuata maelekezo yote waliyopewa, ili kuweza kupata kibali cha kumiliki, ambapo walichagua taasisi yao ya Qiblatain, ili kuweza kuwasaidia kupaendeleza mahali hapo kwa kujenga msikiti, madrasa na shule ya awali.
Meya Londa alipoulizwa iwapo yupo tayari kujiuzulu kutokana na tuhuma hizo, alisema hawezi kujiuzulu kwa mambo ambayo hayana ushaidi, hivyo alitaka mtu yeyote ambaye ana ushahidi wa kweli kuhusiana na tuhuma hizo ajitokeze, na kuziwasilisha kunakohusika.
Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Meya Londa aliwapatia Sh 40,000 kila mmoja, ili kuwawezesha kurejea salama kwenye vyumba vya habari.