ISAYA Yunge, kijana Mtanzania mwenye asili ya jamii ya Wasukuma, ameingia katika hatua mpya ya maisha baada ya kutambulishwa kama mchumba wa Charlene Ruto, binti wa Rais wa Kenya, William Ruto.
Uhusiano huo umefahamika zaidi baada ya hafla ya uchumba iliyofanyika nchini Kenya Agosti 8, ambapo Charlene alimtambulisha Isaya kama mwanaume anayetarajia kufunga naye ndoa.
Hata hivyo, jina la Isaya si geni katika maeneo ya uongozi wa vijana, teknolojia na ubunifu barani Afrika. Safari yake ilianza mapema, huku akiwa miongoni mwa vijana waliopewa nafasi ya kushiriki katika shughuli za kitaifa na kimataifa kabla hata hajafikisha miaka 20.
Katika elimu, Isaya alisomea Bachelor of Science in Insurance and Risk Management katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Tanzania.
Uongozi wake wa vijana ulianza kuonekana akiwa bado katika umri mdogo. Kati ya mwaka 2006 na 2007, aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Tanzania Junior Council, nafasi iliyompa fursa ya kuiwakilisha sauti ya watoto katika majukwaa mbalimbali.
Mwaka uliofuata, akiwa na miaka 17, alichaguliwa kuwa Balozi wa Vijana wa UNICEF Afrika kwa kipindi cha 2007β2008. Kupitia nafasi hiyo, alishiriki katika mijadala na majukwaa ya kimataifa yaliyolenga kutetea haki na ustawi wa watoto, ikiwemo Mkutano wa G8.
Miaka iliyofuata ilimfungulia milango zaidi katika matumizi ya teknolojia kama nyenzo ya kuleta mabadiliko katika jamii. Mwaka 2018, juhudi hizo zilitambuliwa kimataifa baada ya Isaya kutunukiwa The Queenβs Young Leaders Award na aliyekuwa Malkia wa Uingereza, Elizabeth II.
Tuzo hiyo ilitolewa kwa kutambua mchango wake katika kutumia teknolojia na ubunifu kutengeneza suluhisho zenye manufaa kwa jamii.
Mbali na tuzo hiyo, Isaya pia aliwahi kutajwa katika orodha ya Forbes Africa 30 Under 30, inayowatambua vijana wenye mafanikio na ushawishi katika sekta mbalimbali barani Afrika.
Katika ulimwengu wa teknolojia na biashara, Isaya ni mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Goodsam Technologies. Pia amehusika na Smart Kaya, inayolenga kutumia teknolojia katika kuendeleza dhana ya nyumba janja barani Afrika.
Jina lake pia linahusishwa na SomaApp, jukwaa la kidijitali linalolenga kurahisisha upatikanaji wa vitabu na maudhui ya kusoma kupitia mtandao.
Falsafa yake kuhusu maisha na kazi inaonekana pia kupitia utambulisho wake wa βThe Unshakable Optimistβ, huku kauli yake ya kazi ikiwa βBuilding the Gateway to Africaβs Digital Economy.β
Kwa hiyo, zaidi ya kuwa jina lililovuma baada ya kuhusishwa na familia ya Rais wa Kenya, Isaya Yunge ana historia ya safari ya uongozi wa vijana, utetezi wa haki za watoto, teknolojia na ujasiriamali.
Kutoka Tanzania na katika familia yenye asili ya Wasukuma, safari hiyo sasa imemfikisha katika hatua nyingine muhimu ya maisha yakeβkuwa mume mtarajiwa wa Charlene Ruto, na hivyo kuunganisha simulizi yake binafsi na familia ya kwanza ya Kenya.