Wakuu,
Mfanyabiashara wa huduma za kifedha (wakala), Davis Mandari (48), mzaliwa wa Kilimanjaro na mkazi wa Kwa Mrefu, jijini Arusha, ameripotiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha. Inadaiwa kuwa kabla ya kutoweka, alituma ujumbe mfupi kwa mke wake akidai kuwa amechukuliwa na jeshi la polisi.
Mke wa Davis, Marcy Mandari, amesema kuwa mume wake alitoweka mnamo Machi 9, 2025. Kulingana na maelezo yake, siku hiyo Davis aliaga anakwenda kanisani, lakini akiwa njiani, alimtumia ujumbe mfupi wa simu (SMS) akisema kuwa ameshikiliwa na polisi.
Hata hivyo, baada ya kupokea ujumbe huo, Marcy alijaribu kumpigia simu mumewe lakini haikupokewa. Tangu siku hiyo, simu ya Davis imeendelea kuwa kimya.
Marcy amesema amefanya jitihada kubwa kumtafuta mume wake kwa kutembelea vituo vya polisi, hospitali na mochwari mbalimbali jijini Arusha, lakini hajafanikiwa kumpata.
Ameeleza kusikitishwa na tukio hilo akisema kuwa mume wake hakuwa mtu wa makundi, mgomvi, wala hakuwa na uhusiano wowote wa kisiasa, hivyo anashindwa kuelewa alipo.
Ameiomba serikali na jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina ili mumewe apatikane, kwani familia yao inamtegemea, hasa watoto wao watatu ambao wote bado wanasoma.
Source: Jambo TV