Trafiki kutemewa mate:Jeshi la Polisi launda tume
Written by Administrator Friday, 11 December 2009 11:07
Na Waandishi Wetu, jijini
KUTOKANA na kitendo cha ofisa wa Balozi wa Canada kumtemea mate askari wa kikosi cha usalama barabarani na mwandishi,
Jeshi la Polisi limeunda tume ya kufuatilia kwa kina shambulio hilo.
Hayo yamesemwa na Insptekta Jenerali wa Polisi, Saidi Mwema, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo.
Amesema jeshi la polisi limesikitishwa na kitendo hicho cha udhalilishaji kilichofanywa na raia wa Canada, Jean Touchatte (48), ambaye ni Katibu Muhtasi wa ubalozi huo.
Kamanda Mwema amesema tume hiyo inaanza kazi leo na mara baada ya kukamilisha kazi yake, taarifa itatolewa kwa wananachi ili hatua ziweze kufuata na ikiwezekana raia huyo kuondolewa nchini.
Jana Kaimu Kamanda Mkoa wa Dar es Salaam, Charles Kenyela, alisema tukio hilo lilitokea juzi eneo la Banana baada ya trafiki mwenye namba E 1653, Cpl Samsoni, akiwa kazini ghafla mtuhumiwa, akiwa anatokea Ukonga kuelekea Uwanja wa Ndege akiwa na gari namba T 17 CD 178 Toyota Land Cruiser Prado rangi ya bluu mali ya ubalozi wa Canada, alifungua kioo cha gari kisha kumtemea mate trafiki huyo.
Amesema baada ya kufanya kitendo hicho raia huyo aliondoa gari kuelekea mjini ambapo askari huyo alitoa taarifa juu ya kitendo hicho na kuanza kulifuatilia gari hilo na kisha kufanikiwa kulikamata katika Barabara ya Nyerere eneo la Kamata.
Kamanda amesema muhusika huyo alipelekwa Makao Makuu ya Polisi Trafiki
na wakati akiendelea kuhojiwa Mwandishi wa habari wa TBC 1, Jery Muro, alifika ili kujua sababu za raia huyo kufanya kitendo hicho cha udhalilishaji, lakini naye alitemewa mate.
Kutokana na hali hiyo, Muro alilazimika kufungua jalada la shambulio lenye namba CD /1R/ 4818/2009. Hata hivyo, mhusika huyo alipohojiwa na polisi kuhusu kitendo hicho hakuwa tayari kutoa maelezo kwa madai kwamba hadi awepo Balozi wake.
DarLeo, Powered by
Business Times Ltd!