SoC04 Mfumo Utakaotumia Mitandao Ya Kijamii Kuleta Mageuzi Ya Kiuchumi Na Kijamii Nchini

SoC04 Mfumo Utakaotumia Mitandao Ya Kijamii Kuleta Mageuzi Ya Kiuchumi Na Kijamii Nchini

Tanzania Tuitakayo competition threads

Denis Yasada

New Member
Joined
May 31, 2024
Posts
1
Reaction score
1
Utangulizi
Ukuaji wa tenolojia ya mawasiliano na tehama nchini pamoja na ongezeko kubwa la watumiaji wake unazidi kuleta hofu kubwa kwa jamii juu ya maudhui yasiyofaa yanayopatikana hasa kwenye mitandao ya kijamii kwa sababu ya kukosa udhibiti, hali ambayo inadhaniwa kupelekea mmomonyoko wa kimaadili kwa jamii na muda mwingine kutengeneza uraibu wa kuangalia maudhui hayo kila mara na kupelekea kushindwa kufanya uzalishaji mali ili kukuza maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Japo kiuhalisia mitandao ya kijamii ina mambo mengi mazuri kuliko mabaya, changamoto kubwa iliyopo ni namna ya upatikanaji wake na jinsi ya kuyatambua kama ni maudhui chanya kwa jamii miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii hasa vijana. Kwa mujibu wa mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) kufikia Disemba 2023 tayari nchi ilikuwa na watumiaji milioni 36.9 wenye laini hai za simu zinazotumia internet, watumiaji ambao wanaendana sambamba na watumiaji wa mitandao ya kijamii ambapo pia ni ongezeko la takribani 39% kwa mika 5 iliyopita kutoka matumiaji milioni 25.8 mwaka 2019 hadi milioni 36.9 mwaka 2023.
1719779220052.png

Chanzo: www.tcra.go.tz

Taarifa ya Tatizo
Kwa hali ya kawaida ya maisha ya kila siku taarifa sahihi ni kitu muhimu kwa ajili ya kufanya jambo lolote lenye tija kwenye maisha, kukosekana kwa taarifa au kupata taarifa zisizo sahihi mara zote huweza kusababisha mambo mabaya kutokea. Watu wengi hujiunga na mitandao kijamii kama Facebook, Instagram, whatsapp, x (twitter), Telegram na Youtube kwa ajili ya kuhusiana na watu na kupata maudhui mbalimbali lakini hujikuta wakikutana na maudhui tofauti kinyume na matarajio yao, hii hutokana na miundo (algorithms) ya mitandao ya kijamii kuwa na kawaida ya kuonyesha maudhui tofauti tofauti kutoka kwa watu mbalimbali ambayo ni machache sana kati ya mengi yaliyopo kwenye mtandao husika wa kijamii na hapo sasa mtumiaji anaweza kukutana na maudhui yasiyofaa kutokana tu na watu wa karibu na eneo hilo kuyaangalia na kujikuta ameyapenda bila kutarajia maana siku zote vitu vibaya huwa vina mvuto wa kukidhi matamanio ya muda mfupi kama vile maudhui yanayohamasisha ngono, utumiaji wa madawa ya kulevya, ushoga, usagaji, uhalifu wa aina tofauti tofauti n’k, ambapo kama utajihusisha nayo kwa kuyapenda (like), kutoa maoni (comment), shiriki (share) au kuyaangalia basi utakuwa na nafasi kubwa ya kuletewa machapisho ya maudhui hayo kila mara kwenye ukurasa wako wa mtandao wa kijamii husika na kukosa nafasi yakutapata maudhui yatakayokuletea matokeo chanya kwenye maisha yako na jamii kwa ujumla.

Mfumo Pendekezwa
Napendekeza kutengenezwa kwa progamu ya simu na kompyuta (mobile and computer software) itayojumuisha muhutathali na link za account ambazo zitaonekana kuwa na maudhui mazuri kwa ajili ya watu kujifunzia na kupata ujuzi na maarifa ili waweze kujiingizia kipato kwa njia halali na kuboresha hali ya maisha kwa ujumla. Hii itajumuisha na kuwa na timu ya wataalamu kwa ajili ya kufanya mapitio na upembuzi wa maudhui yanayofaa kuwepo kwenye programu hiyo. Programu itahitaji kunadiwa kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo matangazo ya kulipiwa kwenye mitandao ya kijamii na internet kwa ujumla, kwenye vyombo vya habari na majukwaa mbalimbali ya mjumuiko wa watu ili iweze kuwafikia na kutumiwa na watu wengi zaidi. Serikali au taasisi zisizo za kiserikali zitakuwa na jukumu la kugharamia kuanzia hatua ya uundaji wa mfumo hadi uendeshaji wake

Vipengele vya maudhui pendekezwa kwa ajili ya mfumo
Watumiaji watapata kukutana na maudhui mbalimbali yatakayofundisha ujuzi na maarifa ya kufanya mambo tofauti tofauti ya kujiingizia kipato na kuboresha ustawi wa jamii kwa ujumla na yafuatayo ni maudhui pendekezwa yatakayokuwa kwenye mfumo
Ufundi wa vitu mbalimbali kuanzia ufundi wa useremala, mechanikia, ujenzi, elekronikia na umeme ambao hufundishwa kuanzia hatua ya awali mpaka ya juu na watengeneza maudhui kutoka mitandao ya kijamii mbalimbali, ufundi wa aina hii ni mzuri sana kutokana na mtu atakayeupata kuwa na nafasi ya kujiajiri kwa urahisi zaidi
Ufugaji wa samaki kwa kutumia mbinu za kisasa, uhitaji wa samaki nchini bado ni mkubwa sana kutokana na kuwa moja ya nyama nyeupe inayoshauliwa na mataalamu wa afya kama chakula salama na chenye virutubisho vingi vinavyohitajika kwenye mwili wa binadamu, hivyo kufanya soko la samaki kuwa la uhakika
Kilimo cha umwagiliaji, kilimo bado kinaendelea kuwa ni uti wa mgongo wa taifa letu kutokana na zaidi ya 65% ya watanzania wanategemea kama nyanja kuu ya kujipatia kipato na pia kutokana na kuwa na mvua za msimu na tabia ya nchi isiyotabirika kuna umuhimu mkubwa watanzania wakajifunza kilimo cha umwagiliaji kwa njia za kisasa
Ufugaji wa nyuki wa asali, mbinu mpya na za kisasa zinahitajika kwenye ufugaji wa nyuki ili wanaofanya shughuli hiyo na wale watakaoanza wafaidike kwa kupata mazao mengi zaidi
Ufugaji wa kuku, japo inaonekana ni shughuli amabyo haihitaji ujuzi sana ila kwa watokeo wakubwa mbinu mpya na za kisasa zinatakiwa ziwe nyepesi kupatikana ili kuongeza ufanisi wa kuzalisha kuku wengi sana
Unenepeshaji wa ng’ombe na mbuzi kwa ajili ya nyama, hii ni shughuli inayohusisha kuongeza thamani kwa mifugo yetu, hivyo mbinu za kufanya hivyo zinatakiwa zijulikane kwa watu wengi ili na wao kama wataona inaweza kufaa wafanye ili kujipatia kipato cha kukidhi mahitaji
Maudhui yanayofundisha umuhimu wa utunzaji mazingira kiuchumi, kijamii na kiafya na namna bora ya utunzaji wa mazingira kwa faida ya vizazi vilivyopo na vijavyo
Uwepo wa link za kuaminika ambazo mtu anaweza kufanya kazi kama freelancer kama graphics, website design n’k
Namna ya kutoa huduma ya kwanza kwa masuala mbambali ya dharula za kiafya ili kupunguza vifo na ulemavu wa kudumu
Maudhui yatakayoonyesha namna ya kutumuia akili mnemba (artificial intelligence) za aina tofauti tofauti kutokana na teknolojia hiyo kukua sana na kutumika duniani kote kurahisisha utendaji kazi wa mambo mbalimbli, lakini matumizi yake miongoni mwa watanzania yako hafifu sana kutokana na watanzania kukosa uelewa wa matumizi yake

Hitimisho
Matarajio ya mfumo ndani ya miaka 10 ijayo ni kila mtanzania ambaye atakuwa anatumia internet hasa kundi la vijana atatakiwa awe ameshapata taarifa kuhusiana na mfumo jinsi unavyofanya kazi na faida zake na kutokana na urahisi wa upatikanaji wa maudhui hayo inatarajiwa asilimia kubwa ya watu watakuwa wamejifunza ujuzi na maarifa mbalimbali hasa yatakayokuwa yanahitajika zaidi ambayo yatawawezesha kujiingizia kipato na kuboresha maisha yao kwa ujumla.
 
Upvote 4
Back
Top Bottom