Man Chussey
Member
- Aug 2, 2022
- 5
- 1
Jina: Hussein Juma Jitihadi
1.0 UTANGULIZI
Elimu ni chachu katika maendeleo ya kila kitu, mfano teknolojia, uchumi, biashara n.k. Maendeleo ya nchi yoyote duniani yanatokana na athari chanya kutoka katika mfumo wa Elimu ulio imara na wenye kubadilika ili kukidhi mahitaji. Elimu hutumika kutatua kila aina ya tatizo; lililopo, linalotokea na litakalotokea, na hivyo basi, elimu inakuwa moja kwa moja yenye tija katika jamii husika.
Ikitokea taifa la aina yoyote duniani likashindwa kutatua matatizo yake na kutegemea taifa lingine kwa asilimia kubwa zaidi, mfano 70%, basi elimu katika taifa hilo ina mapungufu na haikidhi matakwa ya taifa lake.
Kwanini Tanzania imekuwa nyuma sana na dhaifu katika elimu licha ya kupata uhuru Mapema?
Mababu zetu hawakuwa na maono ya kujikomboa kimaarifa zaidi ya kiuhuru, hivyo, walitumia muda mwingi kutafuta uhuru pasipo kujua taifa linahitaji elimu pia ili likue. Kwakuwa shida yao kubwa ilikuwa ni uhuru wa kawaida, hawakuweza kufikiria tena namna ya kupata uhuru wa elimu kwani wakoloni walikuwa wamesha tengeneza mifumo ya elimu.
2.0 MFUMO WA ELIMU YETU WA SASA
Mfumo wetu wa elimu unagubikwa na changamoto nyingi sana ambazo zinahitaji kutafutiwa suluhisho la haraka. Mfumo wowote wa elimu katika dunia ya sasa ni lazime uwe unabadilika kulingana na mazingira. Changamoto zilizokuwepo zamani (mfano1970 kurudi nyuma) nyingi zilitatuliwa kwa mifumo ya elimu ya zamani, lakini mfumo wa elimu wa mwaka 1970 hauwezi kutatua changamaoto ambazo zinatokea 2022 kwa asilimia kubwa kwani dunia imebadilika kwa kasi sana, na mbinu mpya za utatuzi wa changamoto zinahitajika.
Zifuatazo ni baadthi ya sifa za mfumo wetu wa elimu wa Tanzania
- Elimu isiyo na tija; mfumo wetu wa elimu unaegemea zaidi kumfanya mwanafunzi atambue vitu na si kufanya vitu, Tuna wataalamu wengi wenye kujua vitu vingi na si kufanya vitu au kutatua changamoto nyingi.
- Nadharia zaidi ya vitendo; mfumo wetu haulengi kumfanya mwanafunzi kutatua changamoto bali kumfanya azijue changamto. kwa maana hiyo, unashindwa kumpeleka mwanafunzi moja kwa moja kwenye uwanja wa kutatua changamoto.
- Elimu isiyoendana na wakati; dunia inakuwa kwa kasi sana lakini mfumo wetu wa elimu upo palepale (usiokuwa). Maarifa yaliyopitwa na wakati na yasiyo na tija kwa dunia inayokuwa kwa kasi yamejaa katika elimu yetu na kumfanya mwanafunzi asiweze kuendana na matakwa ya mwajiri/ajira. Mfano, mpaka leo hii wanafunzi wa kidato cha pili somo la kemia wanasoma kiasi cha gesi ya ukaa kaboni daioksaidi kwenye anga ni 0.03% au 300ppm, ambapo zaidi ya miaka 5 imepita iliripotiwa kuongezeka na kufikia 0.04% au 400ppm. Kiufupi, wanafunzi wanasoma vitu vingi ambavyo haviendani/havihitajiki katika kutatua changamoto za dunia ya sasa.
- Elimu yenye kunchanganya mwanafunzi; mfumo wetu wa elimu umepanga kuanzia darasa la I – 7 lugha ya kufundishia ni Kiswahili, kidato cha I – IV lugha ya kufundishia ni Kiingereza na kuendelea mbele. Matumizi ya lugha hizi mbili kwa pamoja zinaleta mvurugiko kwa mwanafunzi kwani mwanafunzi anajengewa msingi wa elimu kwa Kiswahili na akifika sekondari anaanza kupewa maarifa yaleyale kwa lugha ya kigeni (kiingereza), hii ni sawa na kutengeneza msingi wa udongo na boma la mawe na kutarajia msingi utahimili boma.
- Elimu ya makaratasi; mfumo wetu wa elimu una hamasisha zaidi mwanafunzi awe na maarifa tu na si kumfanya aweze kufikiri.
Mfumo wetu wa elimu umeweza zalisha matokeo yafuatayo:-
- Mhitimu mwenye changamoto kubwa ya kupata ajira
- Mhitimu asiyeweza kutengeneza ajira na kusaidia wengine.
- Mhitimu asiye na uwezo wa kutatua changamoto zake na hata zinazomzunguka.
- Mhitimu aliye muoga na asiye na uthubutu wa kufanya jambo lenye tija kwake na taifa zima.
- Mhitimu mwenye maarifa mengi yasiyo na tija kwa dunia inayokuwa.
- Taifa kukosa wataalamu tegemezi katika mambo ya maendeleo ya nchi mfano teknolojia, uchumi n.k
- Utegemezi wa zaidi ya asilimia 50 katika teknolojia (technology transfer) kutoka mataifa mengine ili kutatua changamoto mbalimbali za kitaifa.
- Wanafunzi kukosa maono (vision) juu ya maarifa wanayopata shuleni.
Ili kutengeneza mfumo wa elimu unaotufaa, hatuna budi kujiuliza maswali yafuatayo:-
- Tunahitaji taifa la aina gani, leo na kesho?
- Tunahitaji watu wa aina gani katika ujenzi wa taifa letu?
- Tunahitaji teknolojia gani inayoweza kutufikisha tunapotaka na kwenda sambamba na dunia inayokuwa kwa kasi?
Yafuatayo ni mambo ya kufanya ili kuboresha mfumo wetu wa elimu:-
- Lugha ya kufundishia; lugha moja inatakiwa kutumika kwa ajili ya kufundishia katika ngazi zote za elimu, kama ni Kiswahili au kiingereza, lakini Kiswahili ni bora zaidi kwani itachochea uelewa zaidi kwa wanafunzi.
- Kuondoa vitu visivyo na tija; elimu yetu ni muhimu iwe na maarifa yenye tija na yanayotakiwa katika dunia inayokuwa kwa kasi sana. Maarifa ambayo hayahitajiki ni muhimu kuondolewa ili kupisha nafasi ya yanayohitajika.
- Elimu ya vitendo zaidi ya nadharia; serikali inapaswa kuwekeza zaidi katika hili kwani kujifunza kwa kutenda kutamfanya mwanafunzi kuelewa vizuri na kufanyia kazi alichojifunza, angalau iwe vitendo 60% na nadharia 40%.
- Namna ya kufikiri; mfumo wa elimu unatakiwa umjenge mwanafunzi awe na uwezo wa kufikiri na kuja na majawabu yakibunifu (creative thinking).
- Elimu ya kijasiriamali; kozi hii ni muhimu ianzishwe kwa ngazi zote za elimu kuwafanya wanafunzi wawe na uwezo wa kubadilisha changamoto kuwa fursa.
- Elimu ya fedha (financial education); ni muhimu wanafunzi wawe na maarifa ya fedha, namna ya kutengeneza, kupanga bajeti, kuwekeza n.k.
- Elimu ya kujitegemea; elimu yetu inatakiwa imsaidie mwanafunzi aweze kutambua kusudi la maisha yake, kutambua vipawa (talents) na kukuza na namna ya kubadilisha kipaji kuwa fursa ya kiuchumi.
Tumeangalia vitu vya kuboresha katika mfumo wetu wa elimu hapo juu, pia kuna mambo ya ziada ya kufanya ili kuboresha zaidi:-
- Serikali haina budi kuwekeza zaidi kwenye tafiti na kufanyia kazi kinachotafitiwa.
- Tutumie mifumo wezeshi ya kitehama ya kuwezesha na kurahisisha ujifunzaji kwa mwanafunzi. Hii itampunguzia kazi mwalimu na kuongeza ufanisi zaidi.
- Wanafunzi wapate elimu ya Tehama kutokea elimu ya awali hadi chuo kikuu ikihusisha zaidi utengenezaji wa mifumo na program za kompyuta.
- Serikali inaweza kutafuta namna ya kuongeza bajeti ya elimu ili kufikia malengo yake.
Upvote
0