SoC04 Mfumo wa elimu ya juu uhusike kutengeneza wajasiriamali nchini

SoC04 Mfumo wa elimu ya juu uhusike kutengeneza wajasiriamali nchini

Tanzania Tuitakayo competition threads

Raziel

New Member
Joined
Jul 25, 2022
Posts
1
Reaction score
0
Tanzania kama zilivyo nchi nyingi zinazoendelea zinakabiliwa na kiwango kikubwa cha umasikini ambao unapelekea huduma za kijamii kama elimu, afya, barabara, umeme na mambo mengine kupatikana kwa hali isiyoridhisha na hali hii inatokana na serikali kuachiwa mzigo mzima wa kutatua changamoto hizi kwa kutumia bajeti ndogo isiyo toshelevu.

Kama taifa tunatakiwa kuwekeza Zaidi katika kuimarisha mifumo itakayowasidia watu kuweza kumudu mahitaji yao ya leo na kesho kuliko kuja kutumia gharama kubwa Zaidi kuja kuwapa huduma za bure kama elimu,afya tukiamini kuwa kwa kufanya hivyo ndio tutakua tumeisaidia jamii yetu.

Mfumo wetu wa elimu: Tangu tulipopata uhuru,umekua ni mfumo unaowaandaa watu kuwa wafanyakazi serikalini na kwenye taasisi binafsi na sio mfumo unaosaidia watu kuweza kujenga biashara na taasisi ambazo zitakuja kuchochea uchumi wa nchi yetu.

Mfumo wetu wa biashara: Tumeamini kwa kiasi kikubwa kuwa suala zima la ufanyaji wa biashara ni matokeo ya mtu aliyeshindwa kwenye masomo au mtu aliyekosa fursa ya ajira na katika juhudi za kuhakikisha anapata mkate wa siku inambidi afanye biashara yoyote ili siku ziende,utashi huu umesumbua pia kwenye fursa za kilimo kwa watu kuamini kuwa kilimo ni umasikini.Tunataka kuona juhudi za makusudi zikiwekwa ambazo zitamfanya kijana wa Tanzania kuchagua biashara au kilimo kuliko ajira na hili linaanzia kwenye kujenga misingi ya kujiamini na kumuwezesha mtu kuona fursa.

CHANGAMOTO ZINAZOIKABILI BIASHARA NYINGI TANZANIA

  • Ukosefu wa taarifa sahihi juu ya biashara za ndani na za kimataifa.
  • Ukosefu wa mitaji
  • Gharama kubwa za uendeshaji wa ofisi mf:Kodi za pango
  • Uwingi wa kodi kwa biashara zinazoanza
  • Kukosekana kwa usimamizi/wafanyakazi makini
  • Bidhaa zisizo na ubora unaovutia
  • Ushindani unaosababishwa na bidhaa toka nje ya nchi.
  • Kukosekana na ujuzi wa kuunda na kusimamia vikundi
NAMNA AMBAYO ELIMU YA JUU INAWEZA KUTENGENEZA WAJASIRIAMALI NA UTATUZI WA CHANGAMOTO ZA BIASHARA NCHINI.

Tunataka kuona elimu ya juu inayotolewa kwenye vyuo vyetu kwa hatua mbalimbali za elimu wakienda mbali Zaidi katika kuhakikisha wanazalisha wajasiliamali na kupunguza utitili wa masomo ambayo mwanafunzi anaweza kuja kuyasoma anapofanya mitihani ya bodi za kitaaluma na kuna masomo ambayo mwanafunzi haji kuyatumia maarifa hayo hata anapofika kazini.Vyuo vikuu viwekeze nguvu katika utafiti wa fursa mbalimbali za biashara pamoja na teknolojia,vifanye tafiti juu ya mahitaji ya nchi kwa miaka 10 hadi 30,50 ijayo.

Wanafunzi wanapodahiliwa chuoni pawepo na somo ambalo linaweza kufundishwa kwa lugha ya kingereza ama Kiswahili kadri itakavyoonekana inafaa, (Kuruhusu Kiswahili Kwenye jambo hili ni kuondoa kikwazo cha lugha kumkwamisha mwanafunzi kulipenda somo) somo hili liwe na ufundishaji wa majadiliano baina ya wanafunzi na walimu kwani tunaamini kuwa biashara ni maisha na hakuna ambaye hastahili kujifunza kutoka kwenye uzoefu wa mwenzake.Wanafunzi kwa mwaka wa kwanza wajifunze mambo yafuatayo:

  • Usimamizi wa fedha kwa lugha rahisi
  • Namna ya kuunda vikundi kisheria na kuvisimamia ili kupunguza gharama za uendeshaji
  • Namna ya kufanya majadiliano ya bei(Negotiation)
  • Namna ya kuandika mikataba na mambo ya kuzingatia kabla ya kuingia makubaliano
  • Taratibu za kufanya biashara/manunzi ya mtandao
  • Namna ya kupata wazo bora la biashara
  • Masuala ya kodi
  • Jinsi ya kuanzisha viwanda
  • Jinsi ya kufanya biashara za kimataifa
  • Jinsi ya kuiga teknolojia
  • Namna ya kufanya tafiti ya soko
  • Namna ya kuandaa mpango wa biashara
  • Mifumo mbalimbali ya utunzaji wa taarifa. N.k
Programu hii inaweza kuhusisha wizara zote na ofisi zetu za kibalozi, kila wizara ikaandaa maadhui ambayo yatamrahisishia mwanafunzi kuweza kuona fursa na kufanya maamuzi ila tunatarajia wizara ya elimu,wizara inayohusika na biashara pamoja na wizara ya fedha kuongoza mpango huu.

Kwenye kila somo wanafunzi wapate majaribio(assignment) ambayo watatakiwa kufanya tafiti kwenye mazingira halisi na kuwasilisha matokeo ya kazi yao, wanafunzi watapata kutafiti aina mbalimbali ya biashara kwenye fursa za usafirishaji, kilimo, uvuvi, huduma za afya, Sanaa n.k wanafunzi wapate nafasi za kujifunza kwa vitendo toka kwenye taasisi za ndani na nje ya nchi kadri itakavyowezekana.

Kwa kozi zinazotamatika Mwaka wa tatu tunatarajia, wanafunzi wawe kwenye makundi ya idadi mbalimbali wakiandaa mpango mkakati wa biashara na kupitiwa na jopo maalumu litakaloundwa kwenye hatua ya chuo ambapo kazi yao itakua ni kuukosoa mpango kazi wa wanafunzi na kuuboresha na wanafunzi kufanyia marekebisho juu ya mapungufu mpaka pale ambapo utapatikana unaoshawishi kwenda hatua nyingine ya uwezeshwaji.

Serikali iandae jopo huru lingine lenye wajibu wa kupitia mipango ya biashara yote iliyochujwa kutoka kwenye vyuo vyetu na kupitishwa itakayopelekwa wizara ya fedha kwa ajili ya kupata uwezeshwaji wa serikali.
Kila kikundi kitakachofaidika kitakuwa kinasimamiwa na chuo husika,wizara ya fedha na wizara husika kutegemea na aina ya biashara au uwekezaji waliochagua.

MIPANGO MKAKATI ITAKAYOFANIKIWA KUPITISHWA NA SERIKALI.

  • Wahusika wasaini mkataba maalumu wa kukubali kusimamia mpango wao mpaka mwisho
  • Wahusika wasipewe pesa taslimu kwa ajili ya kununua aseti Zaidi walete Ankara na serikali itanunua vitu vyote kulingana na mpango kazi.
  • Wahusika kwenye kila kikundi watapewa pesa za kujikimu kwa muda usiozidi siku 90 toka kuanza kwa utekelezaji.
  • Wahusika yani wanakikundi,wizara,vyuo vitaingia makubaliano ya kisheria kuzuia aina yoyote ya vikundi hivi kutohujumiwa na wafanyabiashara wasiohusika kujipenyeza kwa lengo la kujinufaisha.
  • Vikundi vyote vipewe muda si chini ya miaka mitano vya msamaha wa kodi zote.
  • Taarifa zote za uzalishaji na mapato,matumizi ya vikundi hivyo vipitie kwenye mfumo maalumu utakaoundwa kwa ajili ya kuvisimamia.
  • Vikundi vyote ni lazima viwe na TIN pamoja na mashine ya kutolea risiti.
  • Kila mwaka vikundi vitatakiwa kuwasilisha taarifa zao za fedha
  • Baada ya kipindi cha neema kuisha vikundi vitarudi kuendelea na biashara uraiani na kuwa kampuni kamili.
  • Kampuni itakayoajili vijana wengi itapunguziwa kiwango cha mkopo walichopokea toka serikalini.
Kwa kufanya utaratibu huu, tutarajie matokeo makubwa ndani ya miaka kumi hadi hamsini ijayo,idadi ya viwanda, biashara, hospitali kuongezeka. TCU haitoshi kubakia kuhusika na udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu pekeake, wanatakiwa kuwafikilia kesho ya wanaowadahili leo kesho wataenda wapi, wizara ya biashara na viwanda lazima wafikilie namna ya kutengeneza na kuzalisha biashara kwa njia tofauti tofauti.Wizara ya fedha kupitia TRA lazima ihusike kujenga walipakodi wapya kwa siku zijazo.

Naomba kuwasilisha.
MUNGU IBARIKI TANZANIA
 
Upvote 5
Back
Top Bottom