SoC03 Mfumo wa kukutanisha wawekezaji na wabunifu kupitia kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC)

SoC03 Mfumo wa kukutanisha wawekezaji na wabunifu kupitia kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC)

Stories of Change - 2023 Competition

Mjukuu wa Hassan-Juma

Senior Member
Joined
Dec 3, 2022
Posts
123
Reaction score
120
Bila shaka unawafahamu marafiki zako wengi wenye mawazo makubwa ambayo hawajafanikiwa kuyafanyia kazi kutokana na sababu mbalimbali. Hebu fikiri tena jinsi mawazo yao yalivyo mazuri na muhimu lakini yamelala, wala hayatambuliki duniani, na unaweza kudhani hayapo kabisa.

Sababu zinazopelekea kutokufanikiwa kwa mawazo haya ni nyingi, ikiwemo ukosefu wa mitaji, elimu ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara, elimu ya sheria na mikataba na kadhalika. Kiujumla madhara ya ukosefu wa mambo haya muhimu yameenea kuanzia kwenye mawazo ya biashara, biashara zinazoanza zinazohitaji uwekezaji mdogo na hata biashara zinazotaka kukua zaidi zinazohitaji uwekezaji mkubwa.
logo.png


Nembo ya TIC (picha mtandao)

Tanzania tuna kituo kinachojihusisha na masuala ya uwekezaji kilichopo chini ya wizara ya Viwanda, biashara na Uwekezaji. TIC inajihusisha na kutoa elimu kwa yeyote anayehitaji kuwekeza nchini Tanzania, awe mwekezaji wa ndani au mwekezaji kutoka nje ya nchi. Kituo hichi huwa kinasajili miradi (projects) mbalimbali inayokubaliwa kwa ajili ya kuwekezwa nchini kwenye sekta kama vile kilimo, usafiri, mawasiliano, utalii, maliasili na kadhalika. Kituo kinajihusisha pia na utoaji wa elimu kupitia makongamano mbalimbali nje ya nchi kwa kutumia balozi zetu na ndio sehemu muhimu sana ambayo wawekezaji wanatambua na KUAMINI kuhusu fursa zilizopo Tanzania na kuzichangamkia.


Pamoja na utendaji kazi wake mzuri, bado ni muhimu kwa TIC kushiriki kwenye kukuza na kuvutia wawekezaji kwenye ugunduzi na mawazo mbalimbali bunifu ya watanzania na bora zaidi ni mawazo hayo kutangazwa kupitia mfumo maalum ambao wawekezaji na wabunifu watakutanishwa huku TIC ikiwa kama kiungo muhimu.

MAELEZO YA MFUMO UNAOPENDEKEZWA

Mfumo unatakiwa uundwe ili kutumiwa na washirika wakuu watatu muhimu ambao ni;

(1) kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC)
(2) wabunifu/wagunduzi na
(3) wawekezaji.

Na kukamilika kwa matumizi ya mfumo huu kunategemea sana ufanisi wa kila mshirika japokuwa TIC ina wajibu wa kudhibiti matumizi sahihi ya mfumo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na ni mfumo utakaotumia aplikesheni ya simu kurahisisha matumizi yake.

Wabunifu na wagunduzi watatakiwa kujisajili kwenye mfumo kama unavyojisajili kwenye mifumo mingine mfano mitandao ya kijamii n.k lakini hapa watatumia taarifa muhimu zaidi mfano namba ya NIDA ili kuthibitisha uraia wao na taarifa nyinginezo na kisha kutengeneza akaunti binafsi. Zoezi hili la kusajili akaunti binafsi linapaswa kuhakikiwa vizuri na TIC ili kuhakikisha usahihi wa taarifa za mhusika.

Baada ya kukamilika kwa zoezi la utengenezaji wa akaunti mbunifu mwenye wazo anatakiwa kuandaa mpango kazi wa wazo lake na kuwasilisha kwa TIC ambao watakuwa na jukumu la kupitia ubora wa wazo husika kabla ya kuliruhusu kuwa kwenye mfumo ambapo wakati huu linaweza kuonekana kwa wawekezaji na watu mbalimbali wanaotembelea mfumo huu.

MAJUKUMU YA WASHIRIKA KWENYE MFUMO UNAOPENDEKEZWA

Majukumu yafuatayo yanapaswa kutimizwa na washirika ili kuupa mfumo maana iliyokusudiwa;

(1) KITUO CHA UWEKEZAJI TANZANIA (TIC)
Kazi muhimu zitakazofanywa na TIC ni;

• Kusimamia utendaji kazi na usalama wa mfumo kila wakati.

• Kukagua ubora wa kazi za ugunduzi na kuzithibitisha kabla ya kuziruhusu kuonekana.

• Kutoa ushauri muhimu wa kitaalamu hasa kwa wabunifu na wagunduzi wapya wenye uzoefu mdogo hasa kwenye mambo ya mikataba na uendeshaji wa miradi.

• Kutoa mwongozo wa namna ya kupata msaada wa kisheria kwa wabunifu ambao wawekezaji wameonesha nia ya kuwekeza kwenye mawazo yao.

• Kuchakata maombi ya wawekezaji wanaohitaji kuwekeza kwenye mawazo ya ubunifu yaliyowavutia.

• Ni kiungo muhimu cha mawasiliano kati ya wawekezaji na wabunifu ili kuondoa ukakasi wa mikataba na utekelezaji wa wazo la biashara/uwekezaji.

(2). WABUNIFU NA WAGUNDUZI
Miongoni mwa wajibu wa kazi za wabunifu na wagunduzi kwenye mfumo huu ni pamoja na;

• Kuwasilisha taarifa sahihi za usajili wa mbunifu na mgunduzi husika.

• Kuwasilisha mawazo yao bora kwa ajili ya kuyatangaza na kupata mwekezaji.

• Kuandaa wazo la ubunifu au kazi ya ubunifu kwenye mpango bora ambao unaweza kuvutia wawekezaji huku akijumuisha na picha kama ugunduzi wake umeanza kufanya kazi.

• Kuboresha mawazo yake kama atakavyoshauriwa na wataalam wa TIC.

(3). WAWEKEZAJI
Wawekezaji watakuwa na majukumu tofauti ikiwemo yafuatayo ;

• Kutathmini mawazo yaliyopo na kutambua wazo ambalo mwekezaji husika anaweza kulifanyia kazi.

• Kuwasilisha taarifa zake muhimu kwa TIC wakati ambapo amevutiwa na wazo na anahitaji kuwekeza kwenye wazo husika.

• Kukubaliana na utaratibu na muundo wa uwekezaji ambao TIC wameuweka ili kufikia ufanisi wa uwekezaji unaotarajiwa.

FAIDA ZA MFUMO KWA WATANZANIA

Zipo faida nyingi ambazo watanzania na taifa kwa ujumla itanufaika nazo kutokana na uwepo wa mfumo huu ikiwemo;

• Kuongeza wigo wa upatikanaji wa mitaji kwenye mawazo na ugunduzi unaofanyika na watanzania ambayo pengine ambayo utekelezaji wake ungekwama kutokana na kukosekana kwa mtaji.

• Kuongeza pato la taifa kutokana na kupanuka kwa shughuli za uwekezaji

• Kusaidia kutatua tatizo la ajira kwa kuwawezesha watanzania wabunifu kujiajiri kupitia kazi zao za ubunifu na ugunduzi.

gold-coins-growth-plant-them_83111-132.jpg

Picha na mtandao

MAMBO YA KUZINGATIWA WAKATI WA MATUMIZI YA MFUMO HUU.

Mambo makuu mawili ya kuzingatiwa ni usalama na uhakika au usahihi wa taarifa zinazowasilishwa na wabunifu pamoja na wawekezaji ili kudhibiti faragha na taarifa zao za siri.

Lakini pia elimu ya matumizi ya mfumo husika inapaswa kutolewa ili kuwataarifu watanzania hasa mavyuoni na nchini kote juu ya uwepo wa mfumo huu na namna wanavyoweza kunufaika nao.

HITIMISHO: Zipo taratibu zingine ambazo wagunduzi huwa wanawasilisha kazi zao ili kuvutia wawekezaji, mfano maonesho mbalimbali kama sabasaba n.k, utofauti ni kwamba maonesho haya yanalenga zaidi kulitangaza wazo/ bidhaa/ ubunifu kwa watumiaji wa mwisho zaidi na ufanisi wake wa kusaidia mgunduzi kupata mwekezaji sio mkubwa sana.

Kupitia mfumo huu wa kutangaza ugunduzi unaofaa kuwekezwa kupitia TIC kutaongeza ufanisi wa upatikanaji wa wawekezaji kwasababu ugunduzi utakuwa umetangazwa sehemu sahihi zaidi.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom