Mwanamwana
Platinum Member
- Aug 1, 2011
- 9,604
- 22,722
Mluya ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma, mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania urais katika ofisi za NEC, akiwa ameambatana na mgombea mwenza wake, Saodun Abraham Khatibu.
Amesema mfumo wa kikokotoo umekuwa kero kubwa kwa watumishi wa umma kwani umesababisha malipo ya mafao yao kuwa madogo kulinganisha na muda waliotumikia.
"Tunakwenda kufuta kilio cha kikokotoo kwa watumishi. Haiwezekani mtu afanye kazi kwa miaka 33 halafu alipwe mafao ya shilingi milioni 13 hadi 14. Hili tunakwenda kuliondoa," amesema Mluya.
Aidha, Mluya ameahidi kuwa serikali ya DP itawajengea nyumba watumishi ambao wamekaa ofisini zaidi ya mwaka bila kuhusishwa na tuhuma za makosa, lengo likiwa ni kupunguza mianya ya rushwa sehemu za kazi.
Kuhusu sekta ya ulinzi na usalama, amesema serikali yake itaboresha maslahi ya Jeshi la Magereza na majeshi mengine, kuhakikisha wanafanya kazi katika mazingira bora. Pia ameahidi kuboresha hali ya magereza nchini.
Katika sekta ya afya, Mluya amesema akinamama watajifungua bure na watoto watapewa lishe kwa miezi mitatu. Aidha, ameahidi kuwa marehemu hatatozwa gharama za matibabu na familia itakabidhiwa mwili kwa maziko bila malipo.
Akizungumzia sekta ya kilimo, Mluya amesema serikali ya DP itahimiza kilimo cha umwagiliaji ili kuhakikisha uzalishaji wa chakula unakuwa wa uhakika na endelevu.
Chanzo: Nipashe