Vyama vyasema bilioni haitoshi
CCM wataka ifikie Sh. bilioni 10
Wapinzani wataka Sh. bilioni tano
Vyama vya Siasa vimekosoa mapendekezo ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, kuwa mgombea wa urais asitumie zaidi ya Sh. bilioni moja kuanzia mchakato wa kuteuliwa na chama hadi kampeni wakati wa Uchaguzi Mkuu, kwa maelezo kuwa kiasi hicho ni kidogo.
Wakizungumza jana na Nipashe, viongozi wa vyama hivyo walisema kiasi hicho ni kidogo na hakiwezi kumwezesha mgombea urais kufika mikoa yote 26.
Wanasiasa hao juzi na jana walikutana na Tendwa kujadili rasimu ya kanuni na taratibu zitakazotumika wakati wa uchaguzi kwa mujibu wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Matson Chizii, alipendekeza angalau kiasi hicho kiongezwe hadi kufikia Sh. bilioni 10 ili zimwezeshe mgombea kuwafikia wananchi katika maeneo yote ya nchi.
"Hao waliopendekeza kiasi hicho walikisia tu bila kwenda kuona hali halisi na sijui vigezo walivotumia …waangalie gharama za kufikia kata zote kwa jimbo moja inakuwa kiasi gani, mafuta, vipaza sauti, vipeperushi, picha za wagombea na wasifu wa wagombea," alisema Chizii. Aliongeza kuwa Sh. bilioni moja haziwezi kutosha kukodisha magari na mafuta ya kuzunguka mikoa yote 26 na kwamba kiasi hicho kwa mtu anayegombea urais kinaweza kukatika kwa kampeni za mikoa miwili tu.
"Mgombea urais ana majimbo 232 ambayo lazima ayafikie wakati wa kampeni zake, sasa atakuwa na miujiza gani ya kuyafikia hayo yote kwa bilioni moja tu, ni kweli tunataka kudhibiti rushwa, lakini kuwawekea wagombea kiasi kidogo siyo dawa ya rushwa na kwa mawazo yangu, naona mtu akiwekewa kiwango kikubwa ndipo ataachana na kutoatoa rushwa," alisema Chizii.
Mwenyekiti wa United Democratic Party UDP), John Cheyo, alisema ingawa ni vigumu kufanya makadirio ya gharama halisi za mgombea urais, kiasi kilichotajwa na Tendwa ni kidogo sana kwa kuwa kugombea nafasi hiyo ni jukumu zito.
Alisema kutokana na miundombinu mibovu, inakuwa vigumu kuwafikia wananchi, hivyo baadhi ya wagombea hulazimika kutumia helikopta ambayo ni gharama kubwa kuikodisha.
"Mimi nimegombea urais, najua ugumu wake, unajua ukigombea pia lazima utumie vyombo vya habari, huna ujanja lazima ujitangaze na matangazo ni gharama kubwa sana," alisema na kuongeza:
"Tusiogope mgombea kutumia fedha nyingi, isipokuwa tuangalie anazitumiaje, kama atazitumia kununua watu ni kosa, lakini akizitumia kuwafikia watu na kuwaeleza sera zake kuna tatizo gani hapo?"
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, alisema kwa gharama ya Sh. bilioni moja haiwezi kuwa rahisi kwa mgombea urais kwani gharama za maisha zimepanda kwa kiwango kikubwa.
Alipendekeza angalau kiwekwe kiwango cha Sh. bilioni tano kwa mgombea urais na Sh. milioni 50 kwa wagombea wa ubunge.
Alitoa mfano kuwa Sh. milioni 20 zilizopendekezwa na Tendwa haziwezi kufika popote kwa mgombea ubunge kwani baadhi ya majimbo ya mijini yana vituo hadi 800 vya kupigia kura hivyo mgombea lazima awalipe mawakala wake wote. "Siku ya uchaguzi tu yenyewe unaweza kutumia milioni nane kuwalipa mawakala, sasa haiwezekani mgombea ubunge kutumia milioni 20 kwa kampeni zake zote," alisema Mnyika.
Mwakilishi wa NCCR-Mageuzi, Beati Mpitabakana, ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, alisema kiasi hicho hakitoshi na alipendekeza kiongezwe hadi kufikia angalau Sh. bilioni tano.
Alisema kutokana na miundombinu kuwa mibovu, wagombea wanalazimika kukodi magari ya uhakika na wakati mwingine ndege ili kufika kwa wakati kwenye mikutano ya kampeni.
Rais wa Tanzania Democratic Alliance (Tadea), John Lifa Chipaka, alisema kiasi hicho ni kidogo sana na kupendekeza kiongezwe hadi kufikia Sh. bilioni tano. Alisema mgombea urais lazima awe na wapambe wa kumsaidia kufanya kampeni mikoa yote 26, hasa pale ambapo hawezi kufika yeye mwenyewe hivyo fedha nyingi lazima zitumike.
"Mimi mwenyewe kama nagombea urais kwanza nahitaji timu ya watu 100 wa kunisaidia na Sh. bilioni tano za kampeni, hawa watanisaidia kuandaa mikutano yangu nchi nzima sio kwamba watakuwa nyuma yangu wanakula na kunywa tu, watafanya kazi na lazima wale na walale na utawapa posho, maana wana familia zao," alisema Chipaka.
Mwenyekiti wa Chama cha Ustawi Tanzania (Chausta), James Mapalala, alisema Sh. bilioni tano hazitoshi kwa mgombea urais ambaye chama chake ni kipya na hakijawa na mtandao mkubwa wa nchi nzima.
Alisema kugombea urais kunahitaji fedha nyingi zaidi ya zilizotajwa na Tendwa kwani mgombea anatakiwa kuwafikia wapiga kura wengi ambao wamesambaa mikoa yote 26.
"Kwa vyama vipya, bilioni moja siyo kitu ila wenzetu CCM hata ukiwapa milioni 100 inawatosha maana wana mtandao wa nchi nzima, ila mimi Mapalala hata nikipewa milioni 200 tu nigombee urais nitamchachafya hata mgombea aliyepewa bilioni moja," alisema.
Mbunge wa Karatu (Chadema), Dk. Willbroad Slaa, alisema kiasi hicho kinaweza kutosha kama vyama hivyo havitahonga wapiga kura na alitoa mfano kuwa mwaka 2005, Chadema ilitumia Sh. milioni 700 katika kampeni zake. Alisema kwa kiasi hicho walikodi helikopta, magari na kujaza mafuta kila siku kwa kuwa hawakuwa wakitoa rushwa kama vinavyofanya baadhi ya vyama.
"Nasema bilioni moja inaweza kutosha, inategemea unataka kufanya nini, kama unataka kuhonga honga na kununua wapiga kura, hizo haziwezi kukufikisha popote na hapo ndipo patamu maana waliozoea kuchapisha kanga, fulana, kofia na kugawa ovyo watashindwa, walidhani hii sheria itawabana wapinzani tu kumbe itawabana hadi wao,"alisema Dk. Slaa.
Naye Tendwa aliiambia Nipashe kuwa ofisi yake ilitoa mapendekezo hayo ili wadau wayajadili, lakini kiasi hicho si uamuzi wa mwisho kama baadhi ya watu walivyotafsiri.
"Jamani nilichotoa ni mapendekezo tu na hawa wadau ndio wanapaswa kujadili na waseme kama kiasi hicho ni kidogo au kikubwa. Sikusema kwamba kiasi hicho kinatosha, wanaoweza kusema kinatosha au hakitoshi ni wao ambao huwa wanaenda kugombea, sio mimi na ndio maana tuko hapa kujadiliana," alisema Tendwa.
Alisema ofisi yake itawapa muda wanasiasa hao kuendelea kutoa mapendekezo yao hadi keshokutwa na yatachukuliwa na kufanyiwa kazi.
Alisema Aprili 6, mwaka huu, kikosi kazi cha ofisi yake kitakaa kuangalia kama mapendekezo ya vyama vya siasa yamefanyiwa kazi na kisha watamwandikia Waziri na baadae rasimu hiyo itapelekwa kwa Waziri Mkuu ili asaini na ianze kutumika kama kanuni halali.
"Maoni yao yote tutayachukua, maana hii kanuni inawahusu wao, wao ndio wanaokwenda kugombea hivyo lazima tuwasikilize na ikishakuwa kanuni sasa tutaanza kubanana kwa wale wanaokiuka," alisema Tendwa.