Nadhani kuharakisha na kusema CCM inahusika ni kutokuwajibika kwani standard ya ushahidi ni kubwa zaidi. Hata hivyo pia kusema kuwa waliotajwa kwenye ufisadi pia ni kuharakisha zaidi kwani unless kuna ushahidi wa aina fulani ni madai tu yasiyo na msingi.
Hata hivyo, kupuuzia kuwa kuvamiwa kwa Bw. Kubenea ni kitendo cha nasibu na ujambazi tu ni kuwa naive na kutokuelewa maji aliyokuwa amejaribu kuyaogolea. Kwa wale ambao tunafuatilia kazi za Kubenea tunatambua kuwa hii si mara ya kwanza kwa yeye kupatwa na ajali za ajabu kama hizi.
Tarehe 13/6/2007 (hii ilikuwa kabla ya orodha ya Ufisadi) alitumiwa ujumbe wa simu ambao uliweka wazi kuwa kuna watu hawafurahishwi na kazi yake ya "kutaja hata majina" kwenye habari za gazeti lake. Kumbukeni kuwa magazeti mengi yamekuwa yakitaja watu kwa mafumbo tu bila kuwataja wahusika wenyewe kwa hofu ya kufikishwa mahakamani. Gazeti la Mwanahalisi halikopeshi kijiko kinaitwa kijiko na sepetu inaitwa sepetu!
Huko nyuma utaona mahali ambapo Mtot wa Mkulima ameandika kidogo kuhusu Kubenea na Tegambwage na kuonesha matatizo anayoyaona katika maandishi ya watu hawa wawili na sitoshangaa baadhi ya watu wanahisia kama hizo pia.
Soma Hapa mawazo ya Mtot wa Mkulima
Hata hivyo hilo halitoshi, Septemba 28, 2007 Gazeti la Tanzania Daima liliandika makala yenye kichwa cha habari "Mwanahalisi:"Tunatishwa" na ndani yake walisema hivi kuhusu vitisho dhidi ya gazeti hilo:
"Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi Mtendaji wa gazeti hilo, Saed Kubenea, ilieleza kuwa kuna mienendo ya chinichini ya kusambaza vitisho kwa vyombo vya habari hususan MwanaHalisi, wachapishaji wake, wahariri, waandishi na wachangiaji wa makala na taarifa mbalimbali.
Hilo lilikuja baada ya gazeti hilo kuandika habari na kuweka hadharani majina ya waliotajwa kwenye ile orodha ya aibu ya ufisadi. Waweza kusoma makala nzima
HAPA
Katika toleo la 63 la gazeti lake Said aliandika makala yenye kichwa cha habari "Watafuna nchi hawa hapa" na hapo wakayataja majina tena ya wale waliotajwa kwenye orodha ya ufisadi.
Lakini anayefikiria kuwa yawezekana kushambuliwa kwake ni sababu za kisiasa atakuwa amekosea. Said amewahi kuwavaa Waislamu katika makala yake ya "Waislamu wamelogwa na nani?" Katika makala hiyo ambapo alikuwa anajadili mahusiano ya Bakwata na Waislamu. Katika makala hiyo bila ya shaka Said amejijengea maadui wengine; wale ambao hawataki kuoneshwa makosa na mapungufu yao!
Hata hivyo huko nyuma mwaka 2003 Bw. Kubenea alijikuta kwenye makali ya watu wa Rai pale ilipodaiwa kuwa aliandika habari ya mahojiano yake na kiongozi mmoja wa CCM ambapo gazeti la Rai liliandika kuwa Kubenea alikutana na mwanasiasa huyo (Bw. Ngeze). Rai wakaamua kuandika habari ya kuomba msamaha kwa ngeze na wakaandika kuwa watamfikisha Kubenea kwenye baraza la Habari kwa ajili ya usuluhishi na yeye Kubenea pia aliamua kulifikisha Rai kwenye baraza hilo hasa baada ya kuona hakutendewa haki.
Naweza kuendelea kwa kirefu, lakini ninachoweza kusema ni kuwa kushambuliwa kwa Bw. Kubenea siyo kwa bahati mbaya na itakuwa ni naivette of the first class kufikiri hivyo. Kimoja ambacho ni dhahiri ni kuwa kumetokana na kazi yake ya uandishi.
Wahusika ni kina nani? Kwa vile nilivyoonesha hapo juu basi kukurupuka na kusema "fulani amehusika" ni kutojua kina cha tatizo na kutomtendea haki yeye KUbenea na wanaotajwa. Kama waliofanya hivyo ni watu wa serikali na serikali ni ya CCM basi kama vile watu walivyosema kuwa ATC ni serikali na chochote ATC inafanya basi serikali inawajibika basi siyo dhambi kuona CCM inahusika; Kama waliofanya hivyo ni watu binafsi kwa sababu zao binafsi ambazo hatuzijui basi wao wanahusika; kama waliofanya hivyo ni kikundi cha waislamu ambao hawakufurahishwa na Kubenea basi kikundi hicho kinahusika na kama ni baadhi ya vyombo vya habari au waandishi ambao hawafurahishwa na Kubenea basi wao nao wanahusishwa.
Vyovyote vile, kitendo cha Bw. Saed Kubenea kushambuliwa kina lengo malengo mawili makubwa. Moja ni kuinyamazisha sauti hii ya mabadiliko na kulitia hofu gazeti la Mwanahalisi na Mseto ili wafikiri mara mbili huko mbeleni na pili kuwapiga mkwara waandishi wowote wale ambao watakuwa na uthubutu wa kusema na kufanya kama anavyofanya Kubenea. Kama vile Ikulu ilivyosema leo kuwa kama kitendo hiki kilimlenga Bw. KUbenea kwa sababu ya kazi yake basi "kimerudisha nyuma" mafanikio ya vyombo huru vya habari.
Ni kwa sababu hiyo kama ilivyosema Ikulu leo, vyombo vya dola vitumie uwezo wake wote kuhakikisha kuwa wale wote waliohusika na kitendo hiki cha kinyama wanasakwa, wanatiwa mbaroni na kufikishwa mahakamani ili sheria ifuate mkondo wake. Kinyume cha hapo, ni kuendelea kuchora mstari ambao Bw. Kubenea anautambua kuwa yote ni matokeo ya "Mgongano wa mawazo". Ni yale ninayosema "mapambano ya kifikra"
Aluta Continua!