Miaka 73 tangu kuzaliwa Bob Marley

Miaka 73 tangu kuzaliwa Bob Marley

CHA The GREAT

JF-Expert Member
Joined
Nov 11, 2010
Posts
651
Reaction score
854
Happy Birth Day: Bob Marley.


Robert Nesta Marley , maarufu zaidi kwa jina la Bob Marley au alizaliwa nchini Jamaika tarehe 6-2-1945 kwa mama Mjamaika--Cedella Malcolm Booker, mwenye asili ya Afrika; na baba mzungu—Norval Marley mwenye asili ya (United Kingdom) Uingereza.


Bob Marley alianza kujishughulisha na muziki akiwa na umri mdogo kwenye miaka ya 1960 ambapo alifundishwa upigaji gitaa na rafiki yake wa karibu—Peter Tosh ambaye baadaye walikuja kuunda kundi lililojulikana kama The Wailers. Prodyusa wao wakati huo aliyejulikana kwa jina la Lee ‘Scratch’ Perry, alisaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha kazi mbalimbali za mwanzo za kundi la The Wailers, hivyo kufanya kundi hilo kuwa bora zaidi nchini Jamaika. Wanamuziki wengine waliounda kundi la The Wailers mbali na Peter Tosh, walikuwa Neville O'Riley Livingston maarufu kama Bunny Wailer, Aston ‘family man’ Barrett, Rita Anderson Marley, Judy Mowatt na Marcia Griffiths.


Mwaka 1974, baadhi ya wanamuziki akiwamo Peter Tosh, na Bunny Wailer, walijiengua toka kundi hilo. Peter Tosh alijiengua kutoka kundi hilo kwa hisia kwamba, prodyusa wa The Wailers wakati huo mwenye asili ya Uingereza-- Chris Blackwell alimpa upendeleo zaidi Bob katika uimbaji kama leading vocal, na kufanya Tosh kutokuonekana au kuonesha uwezo wake na kufanya Bob kuonekana na kung’ara zaidi ya wengine kwenye kundi hilo. Tosh alimtuhumu Chris Blackwell kwa upendeleo huo kwa Bob akiwa na hisia kwamba, asili (uzungu) ya baba wa Bob ambayo kimsingi inafanana na asili ya Chris Blackwell, kuwa sababu ya upendeleo huo kiasi cha kufanya Peter Tosh kumbatiza Chris Blackwell jina lingine la Chris Whitewell.


Bob Marley na The Wailers, walitoa kazi nzuri hivyo kufanya watambulike Kimataifa na kufanya ziara nchi nyingi duniani kama vile Germany, Amerika, United Kingdom, barani Asia n.k. kadhalika alifanya ziara mbili barani Afrika kwa nchi za Gabon na Zimbabwe. Inaelezwa kwamba, kwenye uhuru wa Zimbabwe, serikali ya nchi hiyo ilitoa mualiko kwa kutuma ujumbe kwenda kumueleza Bob Marley nia yao ya kutaka Bob afanye onesho kwenye siku ya uhuru wa nchi hiyo. Menejimenti ya Bob Marley ilitaja gharama za kumpeleka Bob Zimbabwe. Gharama hizo zilionekana kuwa kubwa kwa serikali hiyo changa hivyo kueleza wazi kuwa wasingeweza kumudu. Kutokana na umuhimu wa siku hiyo na kutokana na mapenzi ambayo Bob alikuwa nayo kwa bara la Afrika, alifanya uamuzi wa kufanya onesho la bure ambapo vifaa vya muziki vilisafirishwa kwa gharama zake mwenyewe toka London hadi Harare Zimbabwe.


Bob Marley alikuwa mwana Pan-Afrika, aliyeamini katika umoja wa watu weusi ulimwenguni kote. Hili linaonekana kwenye nyimbo zake za ‘Africa Unite’ ‘Buffalo Soldier’ ‘Zimbabwe’ ‘Keep On Moving’ ‘Black Man Redemption’ na nyinginezo. Ni moja ya wanamuziki bora kwa mauzo ya kazi zao kwa wakati wote, na kupitia muziki wake ameweza kuhamasisha mamilioni ya watu duniani kote na ni moja ya watu walioutambulisha na kuupa umaarufu utamaduni wa RASTAFARI. Rais wa 44 wa Amerika—Barack Obama ni moja ya watu waliokiri kuhamasishwa na Bob kupitia muziki wake wa Reggae. Bob Marley alipinga ubepari ‘babylon system’ kundi nomino inayotumika na Rastafari kumaanisha vitu ambavyo viko kinyume na matakwa ya Mungu, na alikumbatia zaidi ujamaa.


Kwa vitendo na kuonesha kupinga ubepari ’babylon system’ na kuukumbatia ujamaa, watu wa maisha ya chini Jamaika, waliweza kupata misaada toka kwa Bob Marley kila walipomtembelea nyumbani kwake mtaa wa 56 Hope Road. Watu hao walisaidiwa ada za shule kwa ajili ya watoto wao, na inaelezwa msaada wa kifedha aliotoa kwa waliomtembelea kwake, haukuwa kwa ajili ya chakula au mavazi tu, bali msaada wa kifedha ambao uliwasaidia kuanzisha kitu cha kuwasaidia kimaisha.


Licha ya mafanikio makubwa aliyoyapata kutokana na kazi yake ya muziki, iliyofanya auze mamilioni ya nakala za albamu zake na kufanya ziara karibu ulimwenguni kote; Bob Marley alijishusha na kuishi maisha ya unyenyekevu ya kuheshimu watu kwa sababu ya ubinadamu wao. Hii inachangiwa pia na imani yake ya RASTAFARI inayoheshimu na kujali ubinadamu kuliko mambo ya kidunia ‘MATERIALISM’. Mwanaye wa kwanza David ‘ZIGGY’ Marley anasema licha ya mafanikio makubwa, bado baba yake aliwachukua na kwenda nao kutembelea marafiki kabla ya mafanikio yake.


Mwanahabari mmoja aliwahi kumhoji Bob iwapo yeye ni tajiri kutokana na kazi yake ya muziki, Bob alihoji…’utajiri unamaanisha nini’? mwanahabari huyo….akamwambia…’je una fedha nyingi kwenye akaunti yako benki’? ‘je, una mali nyingi sana’? ndipo Bob akajibu….’sina aina ya utajiri huo…mimi utajiri wangu ni maisha ya milele’.


Bob Marley alipata umaarufu na mafanikio zaidi kupitia nyimbo zake za ‘One Love’ ‘Zion Train’ ‘Iron Lion Zion’ ‘No Woman No Cry’ ‘Buffalo Soldier’ ‘Zimbabwe’ ‘Africa Unite’ ‘Three Little Birds’ ‘Waiting In Vain’ ‘Is This Love’ ‘Get Up Stand Up’ ‘Positive Vibration’ ‘Wake Up And Live’ ‘Redemption Song’ ‘Exodus’ na nyinginezo nyingi. Wimbo wake wa ‘Get Up Stand Up’ alioimba akiwa na Peter Tosh, unatumika kama wimbo wa uhamasishaji wa kupigania haki za kibinadamu na Taasisi ya kutetea haki za kibinadamu ulimwenguni—Amnesty International. Nyimbo zake mbalimbali zimetumika kwenye filamu maarufu zilizochezwa na wacheza sinema maarufu wa Amerika. Wimbo wa ‘Three Little Birds’ umetumika kwenye filamu ya Will Smith—I am Legend. Wimbo wake ‘War’ umetumika kwenye filamu ya Idris Elba (akiigiza kama Mandela)—Long Walk To Freedom n.k.



Alama za kibiashara:



Jina lake kwa sasa linatumika kwenye alama za kibiashara ambazo nyingi zinazzalishwa na makampuni yanayomilikiwa na familia yake. Makampuni hayo yanazalisha bidhaa kama vile vinywaji baridi—juisi, mavazi—t-shirts, viatu, makoti na kofia. Kadhalika makampuni yake yanazalisha bidhaa kama vile mabegi (hand bags) ya wanawake, pamoja na bidhaa za urembo kama vile lotion, mafuta ya ngozi, mafuta ya nywele, na marashi. Makampuni yote hayo yanayotambulika kama Bob Marley Group Of Companies, yanasimamiwa na mwanaye wa kike anayejulikana kama Cedella Marley. Cedilla Marley mbali na usimamizi wa makampuni hayo, pia ni mbunifu wa mavazi. Utajiri wake kwa makadirio ya miaka ya hivi karibuni kwa mujibu wa jarida la forbes, unaelezwa kuwa dola milioni 130$ kwa mujibu wa mtandao wa www.therichest.com


Mahusiano:

Bob alikuwa na mahusiano na wanawake wengi akiwamo mrembo wa dunia wa mwaka 1976 Cindy Breakspeare.. Watetezi wake wanaeleza kuwa Bob hakuwa womanizer (au mpenda wanawake kuliko kawaida) kama inavyosemwa na baadhi ya watu, bali wanawake wenyewe ndiyo walijitongozesha kwake na inaelezwa kuwa alikuwa ni mtu mwenye aibu sana. Baadhi ya wanawake walieleza kuvutiwa na sura ya Bob kitu kilichopelekea kujiingiza kwenye mahusiano naye. Judy Mowatt mwanamuziki wa kundi la The Wailers, anasema licha ya visa vya Bob katika suala zima la mahusiano, mkewe Rita, alikuwa na heshima kubwa sana kwa Bob licha ya kujua kila kilichoendelea. Hadi anafariki dunia, Bob aliacha watoto 11 wawili wakiwa wa kuasiliwa yaani Sharon na Stephanie ambao Rita aliwazaa na wanaume wengine.

  1. Cedella aliyezaliwa 23/8/1967, na Rita.
  2. David "Ziggy", aliyezaliwa 17/11/1968, na Rita
  3. Stephen, aliyezaliwa 20/4/1972, na Rita
  4. Robert "Robbie", aliyezaliwa 16/5/1972, na Pat Williams
  5. Rohan, aliyezaliwa 19/5/1972, na Janet Hunt
  6. Karen, aliyezaliwa 1973 na Janet Bowen
  7. Julian, aliyezaliwa 4/6/1975, na Lucy Pounder
  8. Ky-Mani, aliyezaliwa 26/2/1976, na Anita Belnavis
  9. Damian, aliyezaliwa 21/7/1978, na Cindy Breakspeare
Pia aliwahi kuwa na mahusiano na mtoto wa Rais wa Gabon, Omar Bongo aliyeitwa Pascaline. Mtoto huyo wa Omar Bongo, ndiye aliyefanikisha ziara ya Bob nchini Gabon mwaka 1980.

Siasa:

Bob Marley, alinusurika kuuwawa kwa nyumba yake kushambuliwa na wahalifu waliotumia bunduki. Shambulizi hilo lilitokana na chuki za kisiasa zilizokuwa zikiendelea nchini humo kwenye miaka ya sabini ambapo, upande mmoja wa kisiasa uliamini Bob Marley alikuwa upande wa pili dhidi ya upande mmoja. Alipoulizwa iwapo alikuwa na upendeleo kisiasa, Bob Marley alikanusha kwa kusema hamuungi mkono Michael Manley wala Edward Seaga wa chama cha (JLP—Jamaica Labour Party). Kutokana na hali hiyo, Bob Marley aliondoka Jamaika na kwenda kuishi uhamishoni nchini Uingereza (United Kingdom) ili kujinusuru na hatari ambayo ingetokea dhidi yake.

Baada ya kuwa ameondoka, hofu na wasiwasi mkubwa ulipanda kutokana na pande zote mbili kuzidisha uhasama. Uhasama huo ulipelekea watu kuuana na kuumizana kwa mashambulizi ya silaha. Kutokana na umuhimu wake, ushawishi wake nchini humo, serikali ya Jamaika ilituma ujumbe kwenda kwa Bob Marley (wakati huo akiwa Uingereza) ili arudi Jamaika kwa ajili ya kusaidia kutuliza hali iliyokuwa ikiendelea. Bob alikubali na liliandaliwa onesho alipoulizwa na mwanahabari kwa nini anarudi Jamaika, alisema…’maisha yangu si muhimu kama siwezi kusaidia watu wengi’. Siku aliporudi nchini Jamaika, uwanja wa ndege ulifurika maelfu ya watu kumpokea.
bobmarleylegend-png.691205

Picha ya Bob Marley kwenye moja ya album zake maarufu iliyobeba jina la LEGEND.

obama-in-jamaica-png.691212

Barack Obama (Rais wa 44 wa Amerika) akiwa ndani ya Makumbusho ya Bob Marley, mwaka 2015 alipotembelea Jamaika.

bob-on-stage-copy-jpg.691243

Bob Marley, akiwa kwenye moja ya maonesho yake.




Baadhi ya interviews zake.


Bob Marley documentary iliyotoka mwaka 2012.


Dondoo:


*Alikataa kuandika wosia wa nani amiliki mali zake, kwa sababu aliamini kufanya hivyo ni kukiri kuwa kuna kifo kitu ambacho Rastafari hawaamini.

*Alikuwa muumini wa kanisa la Orthodox lenye asili yake Ethiopia.

*Madaktari waliokuwa wakimhudumia na kumtibu, walisema alikuwa mtu mvumilivu na mwenye subira kipindi chote alichokuwa akihudumiwa huko Germany.

*Kabla ya umaarufu wake, familia ya upande wa baba yake ambao ni wazungu hawakumtambua kama sehemu ya familia kwa madai kuwa hawana taarifa yoyote kuwa ndugu yao Norval Marley alikuwa na mtoto aliyeitwa Robert, hivyo kumkataa. Kutokana na kukataliwa huko aliimba wimbo uliotokana na mistari ya Biblia ‘Stone That The Builders Refused—Shall Always Be A Head Corners Stone’.

*Miaka mingi baadaye alipokuwa maarufu na baada ya kifo chake, familia hiyo ilimtambua Bob kama sehemu ya familia na kujivunia Bob Marley kuwa ameliweka jina la Marley duniani kote.

*Bob, alimiliki gari aina ya BMW, na inasemekana kwamba, alinunua gari hiyo kwa kuvutiwa na herufi tatu ambazo zinatengeneza jina la gari hiyo ‘BMW’. Kwa Bob, herufi hizo zilimaanisha—Bob Marley & The Wailers.

*Siku za mwisho akiwa kitandani hospitali, rasta zake zilinyolewa kutokana na hali aliyokuwa nayo kiafya .

*Alipenda sana mchezo wa mpira wa miguu (soka—kandanda) na hata nyumbani kwake, alitenga eneo maalum kwa ajili ya kucheza soka nyakati za jioni.

*Ni moja ya wanamuziki wachache maarufu hata baada ya kifo. Ukurasa wake wa mtandao wa facebook.com kuna ‘likes’ 72,932,700 (milioni sabini na mbili laki tisa thelathini na mbili elfu na mia saba) na ‘followers’ 68,554,334 (milioni sitini na nane laki tano hamsini na nne elfu mia tatu thelathini na nne) kwa takwimu za tarehe 4-2-2018.

Bob Marley alifariki akiwa na umri wa miaka 36 tu mjini Miami, Amerika mwaka 1981/Mei/11. Na angekuwa hai, basi tarehe: 6/2/2018 angekuwa anatimiza miaka 73 tangu kuzaliwa kwake.

Makala hii imeandaliwa kwa kutumia vyanzo mbalimbali hasa:

Mtandao wa www.wikipedia.com ,www.bobmarley.com, www.marleydrinks.com,

TheRichest - The World's Most Entertaining Site

Filamu ya The Marley iliyotoka mwaka 2012, kama ilivyoongozwa na Kevin Macdonald

Filamu ya Will Smith—I am Legend.

Filamu ya Idris Elba (Mandela)—Long Walk To Freedom.

Filamu ya Dwayne Johnson—Journey 2 Mysterious Island.
 
Tetesi kwamba Bob Marley aliuliwa na CIA ni za kweli?
 
Semq mbon alipenda sana chini miaka 36 watt 11
Uwe lijali af una umaarufu km wa Bob, ungetegemea kuwa na watoto wangapi? Kuzaa na miss world unaweza kuhisi alikuwa katika mazingira gani. Wanawake huwa wanapenda wanaume wenye majina, pesa, handsome, wapole, wenye aibu kidogo, warefu kidogo na asiwe bwege. Bob alikuwa navyo vyote wakuu.
 
Uwe lijali af una umaarufu km wa Bob, ungetegemea kuwa na watoto wangapi? Kuzaa na miss world unaweza kuhisi alikuwa katika mazingira gani. Wanawake huwa wanapenda wanaume wenye majina, pesa, handsome, wapole, wenye aibu kidogo, warefu kidogo na asiwe bwege. Bob alikuwa navyo vyote wakuu.
Jf sio maarufu Ila tayari nina watoto watatu kwa mama tofauti, hapo ni mambo ya pm tu Na post za chai za hapa Na pale. Ningekuwa kama Bob ningekuwa Na kijiji
 
Back
Top Bottom