Parabolic
JF-Expert Member
- Dec 3, 2013
- 2,922
- 3,252
Ni miaka mitatu ya hasara kwa mashirika makubwa ya umma, ndivyo unavyoweza kueleza. Hasara hizo zimetajwa katika ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za mwaka 2021/22, 2022/23, 2023/24 matawalia zikigusa mashirika ya Reli Tanzania (TRC), Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Akikabidhi ripoti ya ukaguzi wa Serikali kwa mwaka 2023/24 Machi 27, 2025 ikulu ya Dar es Salaam, CAG Charles Kichere alitaja mashirika kadhaa yaliendelea kupata hasara jambo alisema linaloashiria uwepo wa changamoto za kiutendaji wa kiuongozi.
Alisema TRC ililopata hasara ya Sh224. bilioni kwa mwaka 2024 ikilinganishwa na Sh102 bilioni kwa mwaka 2024.
Mwaka 2021/22 TRC ilipata hasara ya Sh31.2 bilioni.
Hata hivyo, alisema hasara ya 2023/24 haihusishi hesabu za usafirishaji kwenye treni ya kisasa (SGR).
Hasara nyingine ni ya ATCL ya Sh91.8 bilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 62 kutoka kutoka Sh56.6 bilioni mwaka 2023.
Mwaka 2021/22 kampuni hiyo ilipata hasara ya Sh35.2 bilioni.
TTCL nayo imeendelea kupata hasara, ambapo kwa mwaka wa fedha 2023/24 limepata hasara ya Sh27.78 bilioni likiwa ni ongezeko kutoka Sh4.32 bilioni ya hasara kwa mwaka 2022/2023.
Mwaka 2021/22, TTCL ilipata hasara ya Sh15.56 bilioni.
Hata hivyo, akizungumzia hasara ya TTCL wakati wa mahojiano yake na Clouds TV, Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa aliwatoa Watanzania wasiwasi akisema hiyo ni hasara ya kawaida.
"Mfano Shirika la TTCL ambayo chini ya wizara yangu, ingekuwa mashirika haya yanapata hasara kwa aina hiyo ambayo ni hasara ya kawaida ambayo tunaijua kwenye biashara zetu ndogo ndogo maana yake yangesimama, yangekufa. Lakini unavyo-compute hasara kwenye shirika zipo hesabu nyingi ambazo unaziweka kwenye hesabu zako," alisema.
Alisema sababu iliyotajwa na CAG ni kuhamishia Mkongo wa Taifa TTCL na hivyo kusababisha hasara hiyo ambayo isingekuwepo.
Video: Waziri Jerry Silaa
Shirika la Posta Tanzania (TPC) nalo limepata hasara ya Sh23.63 bilioni ikilinganishwa na Sh1.34 bilioni mwaka 2022/23. Mwaka 2021/22 TPC ilipata hasara ya Sh16.21 bilioni.
Tanesco
Hasara nyingine imetokea katika Kampuni Tanzu ya Tanesco ya Kutengeneza Nguzo za Zege Tanzania, baada ya kampuni hiyo kushindwa kutekeleza jukumu lake la msingi licha ya kupokea Sh6 bilioni kutoka Tanesco.
Kwa mujibu wa CAG, kati ya Sh6 bilioni, Sh4 bilioni zilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanda na Maabara ya kupima ubora wa nguzo na Sh2 bilioni kwa ajili ya gharama za uendeshaji.
“Licha ya mipango hiyo fedha nyingi zilitumika kulipa gharama za kawaida na kulipa wazabuni wa nje wanaotengeneza nguzo badala ya Kampuni yenyewe kufanya kazi hiyo kwa zaidi ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, kampuni ilikuwa bado haijaanzisha uzalishaji wa Nguzo wala kuwa na Maabara yake ya ndani.”
Mbali na hasara hizo, CAG alisema Tanesco inadaiwa Sh238 bilioni na kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), ambapo kati ya kiasi hicho, bilioni 111 ni deni la msingi, huku bilioni 127 zikiwa ni riba.
Hata hivyo, alisema yapo mashirika yaliyopata faida kwa mwaka 2023/24, likiwemo Shirika la Maendeleo ya Petrol (TPDC) lililopata faida ya Sh248.75 bilioni, Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) lililopata faida ya Sh242.9 milioni na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imepata faida ya Sh140.8m milioni.
Akipokea ripoti hizo, Rais Samia Suluhu Hassan alisema Serikali inakwenda kuzifanyia kazi dosari zilizobainishwa na CAG na Taasisi ya Kupambana na Kudhibiti Rushwa (Takukuru) ili zisijirudie mwaka ujao.
“Ripoti hizi zinachangia maboresho ndani ya Serikali na mashirika ya umma. Dosari hizi tutakwenda kukaa tuzifanyie kazi kisawasawa, turekebishe na mwakani pengine hizi hazitajirudia, tutakuwa tumesogea,” alisema.
Uwajibikaji
Akizungumzia uwajibikaji wa Serikali kwa mashirika yanayopata hasara, CAG mstaafu Ludovick Utouh, alisema Msajili wa Hazina anapaswa kuunda timu ya utaalamu kuchunguza sababu ya mashirika hayo kupata hasara na kutafuta suluhisho la kudumu.
“Msajili wa Hazina ndio aliyepewa mamlaka kisheria kusimamia mashirika ya umma kwa niaba ya rais na wananchi, aunde timu ya wataalamu, wachunguze sababu za mashirika hayo kupata hasara,” alisema.
Hata hivyo, alisema baadhi ya mashirika yalikuwa na hali ngumu, hivyo kupata hasara sio habari ya kushangaza. “Kwa mfano TRC lilikuwa limekufa kabisa hasa njia ya kwenda mikoa ya Kaskazini, lakini kwa sasa angalau, japo CAG hajazungumzia hesabu za treni ya kisasa (SGR), mchambuzi hawezi kujua wala kuchambua, lakini angalau tunaona kuna uhai.”
Ametoa mfano wa kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) akisema hasara zake zimetokana na umiliki.
“Kwenye ripoti ya 2022/23 tulifuatilia hasara yake kwa undani, tukagundua tatizo ni umiliki; kwamba Serikali iliona ikisajili ndege zake moja kwa moja, zinaweza kukamatwa zikiwa nje ya nchi, hivyo ikazisajili kupitia Wakala wa Ndege za Serikali.
“Sasa zinapotakiwa kufanyiwa matengenezo ya haraka, Wakala wa Ndege atakuwa na bajeti hiyo? Hilo ndilo tatizo linalosababisha hasara,” alisema.
“Tatizo lingine ni mashirika kuanzishwa yakiwa na mitaji midogo, unakuta shirika linahitaji mtaji wa Sh5 bilioni, lakini linaanza na Sh2 bilioni, kwa hiyo linaanza kusuasua tangu mwanzo, mwisho linazalisha hasara.
“Kwa hiyo Msajili wa Hazina aunde timu ya wataalamu wachunguze, hasara zinasababishwa na utawala? Au ni wizi, au usajili au nini?”
Alisema wananchi wana wajibu wa kuipigia Serikali kelele ili kuhakikisha hasara hizo zinadhibitiwa.
“Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya 8 inasema, Serikali itapata madaraka yake kutoka kwa wananchi, hivyo wananchi wana wajibu wa kupiga kelele ili Serikali itekeleze majukumu yake.”