Mizengwe ya vyeti yatawala uchaguzi MRFA
Wednesday, 12 January 2011 20:32
Juma Mtanda, Morogoro
WADAU wa soka mkoani Morogoro wameliomba Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, kuingilia kati suala la uchaguzi mkuu wa Chama cha Soka Mkoa Morogoro, MRFA, kwa kuwa baadhi ya wa waombaji kutokuwa na sifa za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wa chama hicho utakaofanyika keshokutwa Januari 15.
Sifa hizo kwa mujibu wa katiba ya MRFA kupitia ibara ya 29 ukurasa wa 18 kifungu cha 1 hadi 7 katika ukurasa wa 19 zimeelezwa sifa za wagombea.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini hapa, Leonard Massawe na Ferinus Mrope walisema ka nyakati tofauti kuwa sifa za baadhi ya wagombea hazikidhi kuwania nafasi za uongozi MRFA ikiwa ni pamoja na kutokuwa na vyeti halisi vya kidato cha nne na kudaiwa kuwa baadhi yao wakiwa na vyeti vya darasa la saba.
Kwa mujibu wa katiba ya MRFA ibara ya 29, sifa za wagombea kifungu cha pili ukurasa wa 18 katika katiba hiyo inamtaka mgombea kuwa na sifa za kiwango cha elimu ya sekondari kuanzia kidato cha nne na kuendelea.
Nafasi ambazo zinatiliwa shaka na wadau katika uchaguzi huo kwa waombaji hao ni pamoja na mgombea nafasi ya mwenyekiti, katibu mkuu, mwakilishi wa klabu pamoja na wajumbe wa kamati ya utendaji.
Mmoja wa wanaowania uenyekiti, anadaiwa kutowasilisha cheti halisi katika mkutano wa usahili uliofanyika Januari Mosi mwaka huu katika ukumbi wa Masuka Village mjini hapa akiwemo pamoja na mgombea wa nafasi ya katibu mkuu na baadhi ya wajumbe wa kamati ya utendaji ambao katika usahili huo baadhi ya wagombea hawakuwasilisha vivuli vya vyeti vyao na kudai kutokana na hilo wameingiwa shaka juu ya waombaji hao katika kuongoza MRFA.
Wadau hao walisema kuwa katika nafasi ya mgombea wa mwakilishi wa klabu kutoka wilaya ya Mahenge anadaiwa kuwa sio mwakilishi halali wa wilaya hiyo licha ya katibu mkuu wa chama cha wilaya kusita kuthibitisha kutambuzi wa mwakilishi huyo wakati akiongea kwa njia ya simu ambapo alidai kuwa taarifa zisizo rasmi alidai anawania nafasi hiyo kutoka klabu ya vijana wilayani humo.
Pia wadau hao walisema kuwa katika nafasi ya wagombea wa kamati ya utendaji, baadhi ya wajumbe hawana vyeti vya kidato cha nne huku wengine wakidaiwa kuwa na vyeti vya darasa la saba.
Wadau hao wametoa ushauri kwa katibu mkuu mpya wa TFF kuweka utaratibu wa kukagua upya vyeti halisi vya wagombea chini ya wataalam kutoka baraza la mitihani Tanzania (NECTA) siku tatu kabla ya uchaguzi na endapo shirikisho hilo hatazingatia ushauri huo wa wadau wa soka mkoani Morogoro watakwenda kuweka pingamizi uchugazi huo kwenye vyombo vya sheria kuzuia uchaguzi huo mpaka taratibu zitakapofuatwa.