TI yataka mchakato wa uenyeji Kombe la Dunia usimame
Send to a friend Tuesday, 30 November 2010 20:21 0diggsdigg
ZURICH, Uswisi
SHIRIKA la Kimataifa la Kupambana na Rushwa la Transparency International (TI) limelishauri Shirikisho la Soka la Kimataifa, Fifa kuahirisha uchaguzi wa nchi ambazo zitaandaa fainali za Kombe la Dunia ambao unafanyika Ijumaa.
TI imeshauri mchakato huo wa kupata wenyeji wa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 na 2022 usimame kutokana na madai mapya ya rushwa.
Kamati ya utendaji ya Fifa inatarajiwa Ijumaa kupiga kura kuchagua nchi ambazo zitakuwa wenyeji wa fainali hizo kubwa za soka duniani.
"Tunashauri uchaguzi wa nchi ambazo zitaandaa fainali za 2018 na 2022, Desemba 2 usubiri kwanza madai yote ambayo yamechapishwa na vyombo vya habari yachunguzwe na kubainishwa ," ilieleza T I, tawi la Uswisi katika taarifa yake.
"Madai hayo yametia doa mpango mzima wa kupata wenyeji wa fainali zijazo za Kombe la Dunia ili kuepusha utata unaoweza kujitokeza ," iliongeza taarifa hiyo.
Gazeti la Tages-Anzeiger la hapa liliripoti kuwa Ricardo Teixeira wa Brazil, bosi wa soka wa Afrika, Issa Hayatou na mwenzake wa Amerika Kusini, Nicolas Leoz wanahusika katika ripoti ya siri ya malipo kutoka kwa mshirika wa Fifa aliyefilisika, ISMM/ISL zaidi ya miaka 10 iliyopita.
Kampuni hiyo ilifilisika mwaka 2001 kutokana na utata wa madai ya kutoa rushwa ili kupata haki za televisheni za kuonyesha mechi za kombe hilo, madai ambayo yalifikishwa mahakamani na Fifa, kisha kufutwa.
Mahakama moja ya Uswisi iliwatoza faini maofisa watatu waandamizi wa ISMM/ISL mwaka 2008 kwa matumizi mabaya ya fedha au makosa yanayohusiana na masuala ya uhasibu.
Leoz, pia alikuwa tayari ameorodheshwa kama mmoja wa watuhumiwa wa upokeaji malipo kutoka kampuni hiyo iliyokuwa ikijihusisha na masoko, kashfa ambayo iliyahusisha pia makampuni mengine kadhaa, madai ambayo yalifunguliwa katika mahakama za Uswisi mwaka 2005.
TI imeogeza kuwa hata kama madai ya sasa hayataweza kuthibitishwa, yanahitaji kuchunguzwa na tume huru ili kupat ukweli badala ya kamati ya maadili ya Fifa.
Maombi ya kupata timu wenyeji wa fainali za mwaka 2018 na 2022 ziliingia doa baada ya timu ya waandishi wa habari wa gazeti moja la Uingereza kufichua madai dhidi ya maofisa wawili wa kamati ya utendaji ya shirikisho hilo, Reynald Temarii, raia wa Tahiti na Amos Adamu kutoka Nigeria kuomba rushwa kwa lengo la kuuza kura zao.
Kumekuwa na hisia kuwa kura hiyo ya siri inaweza kuathiriwa na kukosekana kwa mwakilishi wa Shirikisho la Soka la Oceania (OFC) , ambalo limeombwa nafasi ya Temarii ijazwe kwanza na mtu mwingine.
Ingawa Fifa imesisitiza kuwa kura zitapigwa na wajumbe 22 kati ya 24 wa kamati yake ya utendaji, lakini mkuu wa timu ya maombi ya England ya fainali za 2018, Andy Anson aliwaambia waandishi wa habari kuwa anaamini wapigakura watakuwa 23.
"Ninaamini kuwa OFC watapewa nafasi ya kupiga kura ," alisema Anson .
Naye mwanasheria wa Temarii , Geraldine Lesieur, aliliambia Shirika la Habari la AFP kwamba Fifa ilimtaka aachane na mpango wake wa kukata rufaa kwa niaba ya mteja wake kupinga kufungiwa mwaka mmoja, baada ya kusafishwa dhidi ya tuhuma za hongo.
Hata hivyo , Temarii hajapokea ripoti kamili ya uamuzi wa suala hilo, hatua ambayo kisheria ina umuhimu mkubwa kumwezesha kuamua kukata rufaa au la, alieleza mwanasheria wake.
"Mteja wangu (Temarii)m ataamua baada ya kuarifiwa rasmi kupitia hukumu dhidi yake," alisema Lesieur. "Tunaendelea kusubiri."
Temarii ameiambia AFP kwamba kura yake angeitoa kwa nchi mbili ambazo zingechaguliwa na wakuu wa shirikisho la soka la Oceania.
Rais wa Fifa, Sepp Blatter ameahidi kuwa 'Fifa mpya' utateua watu makini kuandaa fainali za 2018 na 2022, akisema mabadiliko mengine yatafuata baadaye kwenye shirikisho hilo.
England, Russia, Hispania/ Ureno na Uholanzi/Ubelgiji zinaomba uenyeji wa 2018 wakati Australia, Marekani, Japan, Qatar na Korea Kusini zinaomba fainali za 2022.
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, Mwana wa Mfalme William, Waziri Mkuu wa Russia, Vladimir Putin, warithi wa ufalme wa Qatar na Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton watakuwa miongoni mwa wazito ambao watahudhuria mkutano huo wa kamati ya utendaji ya Fifa leo na kesho kuwashawishi wajumbe.