UONGOZI wa Yanga umesema licha ya Kocha wake Mkuu, Kostadin Papic kutangaza kubwaga manyanga kuifunza timu hiyo, wao
bado wanamtambua kama kocha wao kwa kuwa hajaandikia barua ya kuachia ngazi.
Papic wiki alitangaza kubwaga manyanga kuifunza timu hiyo kwa madai kwamba uongozi haumshirikishi katika mambo ya kiufundi ikiwemo kumwajiri Kocha Msaidizi, Felex Minziro.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu alisema pamoja na kocha huyo kutangaza kujiuzulu, lakini uongozi wa Yanga haujapata taarifa yoyote ya maandishi.
"Kisayansi ni kwamba Papic, bado ni kocha wetu kwa kuwa hajawasilisha barua yoyote inayosema amejiondoa Yanga, muhimu ni yeye kuandika barua na kuleta kwa uongozi ili tuweze kuipitia kisheria," alisema Sendeu.
Alisema ni kweli suala la yeye kujiuzulu si geni kwa kuwa amekuwa akitangaza mwenyewe kwenye vyombo vya habari na isitoshe alikwenda kuwaanga na wachezaji wake, lakini pamoja na yote hayo hajawasilisha barua.
Yanga ipo kambini kujiandaa na mchezo wake wa kesho wa michuano ya CAF dhidi ya Dedebit ya Ethiopia, lakini ikiwa na Minziro ambaye atakuwa na jukumu ya kuliongoza jeshi hilo la Jangwani akiwa na Meneja wake Salvatory Edward.
Katika hatua nyingine, Dedebit ambayo jana ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam wametamba kuibuka na ushindi katika mechi hiyo.
Sinema ya kifo cha Mzee Yussuf ‘Mfalme' hii hapa
Abdallah Menssah
TANGU Jumamosi iliyopita, taarifa za uzushi zilizomshtua kila mdau wa mipasho zilisambaa kama uyoga, kuwa galacha wa miondoko hiyo, Mzee Yussuf ‘Mfalme', amefariki dunia. Nikiwa miongoni mwa waliopata wakati mgumu kutokana na uzushi huo, nililazimika kufika katika Hospitali ya Bulele, Kibaha kwa Mfipa, Pwani alikokuwa amelazwa Yussuf baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti ili kujua zaidi. Huko nilikutana na umati mkubwa wa mashabiki na wadau wa muziki wa taarabu ambao nao walikuwa wamefika hospitalini hapo kushuhudia wenyewe, kwani nao walikuwa wamepata taarifa kama hizo. Lakini, kila aliyekuwa amefika hapo nilimkuta akiwa katika hali ya namna yake kutokana na majibu waliyopewa na wauguzi pamoja na madaktari wa hospitali hiyo maarufu. Kuwa eti Yussuf hajafa na badala yake alikuwa amepata nafuu na kuruhusiwa kurejea nyumbani ikiwa ni siku mbili tu baada ya kukamilika kwa zoezi la upasuaji hospitalini hapo. Shughuli sasa ya kumpata Yussuf mwenyewe kwa uhakika zaidi ndiyo ilikuwa ngumu kupita maelezo kutokana na kuwa, alikuwa hapatikani kwenye simu zake zote za mkononi. Nilichokifanya nikaamua kupiga mguu hadi nyumbani kwa wake zake, mkubwa na mdogo, yaani Magomeni na Mbagala, ambako nako sikupata jibu lililokuwa sahihi baada ya kuzikuta nyumba zikiwa tupu. Nilipojaribu kuongea na baadhi ya viongozi wa kundi lake la Jahazi Modern Taarab niliambiwa kuwa Yussuf yuko hai, amepata nafuu karuhusiwa kutoka hospitalini na kuamua kurudi nyumbani. Yuko wapi sasa? Mbona majumbani kwake kote hayuko? Nikaanza kuhisi kama vile labda nafichwa kitu fulani, hasa kwa vile mimi ni paparazzi. Nilijaribu kuwasiliana na baadhi ya watu wa karibu sana na Yussuf, akiwamo Mkurugenzi wa Kampuni ya Screen Masters, Said Mdoe, aliyeniweka wazi kuwa jamaa ameruhusiwa kutoka hospitali alikokuwa amelazwa. Mdoe akaniambia kuwa taarifa za kuwa eti amefariki ni uzushi tu unaojaribu kuenezwa na kundi la watu wachache wasiomtakia mema katika maisha yake, hasa ya kimuziki. Akanipasulia kuwa baada ya kuruhusiwa kutoka Hospitali, Yussuf ameamua kwenda kupumzika nyumbani kwao Michenzani, Zanzibar akijiuguza taratibu na wazazi wake. Aliponiambia hivyo, kwakuwa mimi si mgeni kisiwani Zanzibar na hususan hapo nyumbani alikozaliwa Yussuf, nilikata shauri la kwenda mojakwamoja kushuhudia kwa macho yangu ili nipate cha kuandika. Ila kwakuwa jua lilikuwa limeshakuchwa, nilisubiri siku ya pili yake, yaani Jumapili ambako niliingia ndani ya boti la alfajiri na kutua kisiwani Zanzibar mapema mno, moja kwa moja hadi nyumbani kwa kina Yussuf Michenzani nyumba namba 2, ghorofa ya 3 na ngazi namba 4. Nilipofika nyumbani kwao nikakutana na mama mzazi wa Yussuf, Mwanajuma Mzee, aliyeniambia kuwa mwanawe yuko ndani ambako alikwenda kuniamshia kwakuwa alikuwa yungali amelala. Punde Yussuf alitoka chumbani kwake kwa kuchechemea akisaidiwa na magongo maalum aliyopewa hospitalini, tukaanza kupashana habari. Katika mazungumzo yetu, sebuleni kwao Yussuf alisikitishwa mno na namna nchi nzima inavyozizima kwa uvumi wa kifo chake, hali ya kuwa, yeye mwenyewe bado yuko hai. "Nimezipata taarifa hizo, ambapo wanaonipenda wengi wamenipigia simu kutaka kujua ukweli wa mambo na mimi nikawajibu kadiri ninavyoweza," anasema Yussuf aliyewekewa POP mguuni. Anasema simu za watu waliokuwa wakitaka kupata uhakika wa taarifa walizozisikia zilikuwa zikimiminika kama maji, kiasi sasa akaamua kuzima simu ili kupata muda wa kupumzika kama alivyoshauriwa na tabibu. Hata hivyo, anasema kuwa anaendelea vyema japo itamchukua takriban majuma matatu au manne hadi kuanza kuonekana tena katika jukwaa la Jahazi Modern akiimba na kucheza kwa nakshi. Anaeleza kuwa hali haikuwa kama wengi walivyosikia kwani alikwenda mwenyewe hospitali ili kupata utatuzi wa tatizo hilo la goti lililomsumbua kwa muda mrefu baada ya kupata hitilafu mpirani. "Sikuwa hoi, nilikwenda hospitali mwenyewe kwa miguu yangu na baada ya kufanyiwa upasuaji, niliruhusiwa na kuamua kuja kupumzika huku," anasema Yussuf, mahiri kwa utunzi, uimbaji na upapasaji wa kinanda. Aidha, Yussuf anasema, ameathirika sana kwa uvumi huo, kubwa zaidi ni kuwayumbisha mashabiki wake wengi huku akifafanua kuwa walioueneza uvumi huo walikuwa na lengo la kumpunguzia umaarufu. Anasema bado yupo na kama Mungu atapenda aendelee kuwapo basi uzushi na uvumi hautasaidia kitu, kwa sababu yeye ndiye anayetazamwa na wanadamu wote hapa ulimwenguni. Anaeleza kuwa, zaidi uvumi huo utaishia kuwashitua na kuwaathiri mashabiki, wasanii na wadau wengi tu, kwani siku ya kwanza kuanza kuvuma, hata mkongwe wa Taarab Asilia, Fatuma binti Baraka ‘Bi Kidude' alitaharuki sana na kumwaga machozi. "Mimi nipo kwetu huku Zanzibar na wazee wangu nikingoja kupata nafuu zaidi, wanaoeneza uvumi wa kuwa nimekufa sina budi nao, na waanze tu kunikusanyia michango," alisema Yussuf. Aidha, Yussuf anawaomba mashabiki na wapenzi wake wasiwe na wasiwasi kwani anaendelea vizuri ambapo amewataka kutulia katika kipindi hiki kigumu atakachokuwa haonekani jukwaani. Kadhalika anasema atakaporudi jukwaani atashusha kibao kipya kuhusiana na tukio hilo kinachokwenda kwa jina la ‘Bado nipo nipo kifo mipango ya Mungu', atakachokiimba yeye mwenyewe.
Fahamu kilichomfanya ‘TX Moshi' kuvua magwanda Polisi Jazz
Juma Kasesa
KARIBU mpenzi msomaji wa safu hii ya Jamvi la Kulonga. Ikiwa ni Ijumaa nyingine tunakutana jamvini katika kudadavua na kujuzana haya na yale yanayotokea na yaliyowahi kutokea katika tasnia ya sanaa na burudani. Leo katika Jamvi hili nataka nikujuze kisa kilichomfanya mwanamuziki mtunzi na mwimbaji ambaye alikuwa nguli wa muziki wa dansi hayati Ally Muhoja Kishiwa ‘TX Moshi William' kuamua kuvua magwanda ya Jeshi la Polisi akiwa na bendi ya ‘Wanavangavanga' na kujiunga na Juwata Jazz. Lakini kabla Jamvi hili halijakupa kisa hicho kwa undani limeona ni vyema kukudadavulia kwa kifupi mchango wa TX Moshi katika muziki wa dansi wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Katika mafanikio ya muziki huo nchini huwezi kuacha kuzungumzia jina la mwanamuziki huyo ambaye enzi za uhai wake alifanya jitihada nyingi kuhakikisha anatunga na kuimba nyimbo zenye kuburudisha na kuelimisha jamii ambazo ziliunyanyua kwa kiwango kikubwa na kuuweka katika ramani muziki wa dansi. Moshi, ambaye alizaliwa mwaka 1954 katika Kijiji cha Hare, mkoani Tanga, anatarajiwa kutimiza miaka mitano ya kumbukumbu ya kifo chake Machi 29, mwaka huu tangu alipofariki baada ya kuugua kwa muda mrefu mguu kufuatia ajali ya gari aliyoipata mwaka 2004 eneo la Mivinjeni. Jamvi la Kulonga linatambua kwa nguvu zote mchango wa Moshi katika kukuza muziki wa dansi akiwa ni mwanamuziki ambaye kifo chake kiliishitua tasnia ya muziki huo na kuiacha ikiwa imepigwa butwaa kutokana na jitihada zake mbalimbali alizokuwa akizifanya ambapo hadi leo nyimbo zake zinaendelea kuvuma. Moshi ni mwanamuziki ambaye inakadiriwa kuwa mpaka mauti yanamkuta alikuwa ametunga nyimbo takriban sabini na ambazo zote zilimjengea umaarufu yeye na bendi yake kuanzia Polisi Jazz na hata alipohamia Juwata. Licha ya uwezo wa kuimba na kutunga aliokuwa nao Moshi pia alijaaliwa uwezo mkubwa wa kupiga gitaa la solo na muandaaji mzuri wa muziki, ikiwa ni funzo kwa wanamuziki wa sasa kujitahidi kuwa watundu kama alivyokuwa Moshi. Baadhi ya nyimbo zilizomjengea umaarufu enzi za uhai wake akiwa Polisi Jazz ni ‘Mwaka wa watoto', ‘Teddy' ‘Mama baba yuko wapi' na ‘Narudi Kijijini' ambao aliuimba kiufundi na Hassan Jalala. Alipotua Juwata mwaka 1982 aliwika na nyimbo kama ‘Ashibaye' ‘Hamida' ‘Kimanzichana, ‘Nyabasi Mwanangoreme' ‘Baba Mai', ‘Tupatupa' ‘Fatuma' ‘Msafiri Kakiri' ‘Queen Kase', ‘Belinda' ‘Asha Mwana Seif', ‘Bahati' ‘Binti Maringo', ‘Tuma' na ‘Gloria'. Nyimbo nyingine ambazo Jamvi la Kulonga linazifahamu kuwa zilimpatia umaarufu Moshi ni ‘Rehema' ‘Kasheshe' Nyamizi, ‘Demorasia ya Mapenzi', ‘Ndoa Ndoano' ‘Kilio Cha Mtu Mzima', ‘Piga Ua Talaka Utatoa,' ‘Mtoto Makutubu', ‘Piga Ua Talaka Utatoa', ‘Harusi ya Kibene', ‘Kaza Moyo' ‘Kalunde' na ‘Ajali' ukiwa ni wimbo ambao wachambuzi wa masuala ya muziki wanasema alikuwa ajitabiria maisha yake. Tukirudi katika hoja yetu ya leo ambayo Jamvi hili lilikuwa linataka kukujuza kuhusu kilichomfanya Moshi kuacha ajira ya serikali kupitia Jeshi la Polisi na kujiunga na Juwata Jazz mwaka 1982. Sababu ambayo Moshi kabla ya kifo chake aliwahi kuliambia Jamvi hili ni kwamba katika mwaka huo wa 1982 bendi ya Polisi ilipata vyombo vipya lakini kiongozi mmoja wa juu ndani Jeshi la Polisi aliamuru vyombo hivyo viuzwe na kusema muziki ni anasa ndani ya jeshi. Kauli ya kiongozi huyo ilimuudhi Moshi kwa kiwango kikubwa kwakuwa yeye aliingia jeshini kupitia fani ya muziki na kusema muziki ni anasa ni jambo lililokuwa likiashiria kuota mbawa kwa ajira yake. Kauli ya kuuzwa kwa vyombo iliendeleza sononeko moyoni mwake na wakati huo nyota yake kimuziki ilikuwa iking'ara ndipo bendi ya Juwata Jazz kupitia kiongozi wake na mpiga solo mahiri, Saidi Mabera, ilipoanza jitihada za kumshawishi ajiondoe na kujiunga Juwata. Kabla ya kujiunga na Juwata alifanya uamuzi wa kuvua magwanda na kujiunga na Udda Jazz iliyokuwa chini ya Kassim Mapili, lakini hakukaa sana akatua Vijana Jazz na kuanza mazoezi lakini kabla hajarekodi na bendi hiyo ndipo juhudi za Mabera zikazaa matunda na kutua Juwata Jazz ambako alivuma hadi mwisho wa uhai wake. Hiki ndicho kisa ambacho kilimtoa TX Moshi Wiliam Polisi Jazz na kujiunga na Juwata Jazz, ambapo Jamvi hili linakuahidi kukudodosea kisa kingine kuhusu mwanamuziki mwingine mkongwe wa muziki wa dansi. Kwa leo nalikunja Jamvi hadi Ijumaa ijayo, nikikutakia wikendi njema.
MKURUGENZI wa Tanzania One Theatre (TOT) John Damian Komba, Ijumaa iliyopita alifungua rasmi kambi ya kundi lake kwa upande wa fani za dansi na taarabu. Kwa maelezo yake hiyo ni katika mikakati ya dhati ya dhamira yao ya kuinyanyua TOT na kuirudisha tena kileleni baada ya kuonekana imepoteza makali kwa kipindi kirefu sasa. Tunaoifahamu TOT Plus Band tangu enzi zile ambako Komba alikuwa akirapu katika bendi hiyo iliyokuwa ikitumia mtindo wa ‘Achimenengule', tunakubali kuwa kweli imepoteza makali. Hata katika taarabu, hii ya sasa bado haijatangazika kiasi cha kuifikia ile ya enzi za ‘Kasheshe', ‘Nyama ya Bata', ‘Mtwangio', ‘Kimburumatari', ‘Manamba' ‘Natanga na Njia' na ‘Sheshi Beshi'. Mbali ya kuwa hivi sasa vijana wa taarab pamoja na dansi, wote wanajitahidi kuumiza vichwa na kuibuka na tungo zinazowachoma wengi hadi wengine kuamua kuzifungia. Nilipozungumza naye Komba ofisini kwake, CCM Mwinjuma, Mwananyamala jijini Dar es Salaam, Komba mwenyewe naye anakubali kuwa TOT imeshuka, hasa upande wa dansi. Anasema kushuka kwa TOT kumetokana na pilikapilika zao za zaidi ya miaka miwili, walipokuwa katika kampeni za chaguzi ndogondogo na ule mkuu uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana. Hata hivyo, anasema hivi sasa hawana pilikapilika, kwa hiyo baada ya kumaliza kambi Februari 14, watazindua kutumbuiza kwa onyesho kubwa kwenye ukumbi wa Hoteli ya Travertine iliyopo Magomeni, jijini Dar es Salaam. Binafsi, nawatakia kila la heri wana TOT, katika dhamira yao hiyo ya kujipanga na kurudi upya kwenye chati, ili nao wawe miongoni mwa washindani kamili wa kimuziki. Hii ni kwa sababu, TOT ambayo sasa inajulikana kama ‘TOT Fair Play Wazee wa Mzuka' ni kati ya bendi za Kitanzania, yenye mashabiki pamoja na wapenzi wengi karibu kila kona. Naamini kabisa kuwa pamoja na mimi, wako wengine wengi wanaosikitika na kusononeka kutokana na hili la bendi yao hii kutofanya vyema katika kutoa burudani. Nina imani kuna wale ambao walikuwa wakijiuliza sababu ya TOT kurudi nyuma kadiri siku zinavyosonga, ilhali ina kila kitu kuanzia ukwasi wa pesa, wasanii mahiri na vyombo vya kisasa. Changamoto ninayoitoa kwa uongozi wa TOT ni kuwa baada ya kumaliza kipindi chao cha kukaa kambini na kuanza maonyesho, wahakikishe wanapigana kwa hali na mali ili kuinusuru bendi hiyo. Kwa leo napenda niishie hapa nikiwaacha wadau wangu na kaulimbiu isemayo: ‘Ukikimbiza ndege kwa baiskeli ya miti utapasuka mapafu…' Wadau wangu wa ukweli leo hii ni Dogo Baraka ‘Jembe', Aziza Issa, Mohammed Mtwale, Said Makorokoto, Asha Salum pamoja na mapacha Hassan na Hussein Idd. Wengine ni Ikota Mhamila, Ben Mtwanga, pamoja na Rajab Mhamila ‘Super D. Mnyamwezi' anayetuongezea heshima watoto wa kiume kwa dawa bomba ya ‘Enzoy'.
SALAAM aleikum mpenzi msomaji wa busati sfafu ambayo imekuwa ikikufikia kila ifikapo siku ya Ijumaa. Ama baada ya salamu ningependa kuanza kwa kero mbalimbali ambazo huwa nazipata kwa kupitia safu hii, jamani ewe msomaji na mdau tafadhalini saana nawaomba muache kuwa wasumbufu hasa kwa kutumia vibaya namba yangu ya simu kwani lengo la kuiweka hapa si baya ni la kikazi zaidi na mnanikera mnavyoitumia ndivyo sivyo. Natumaini hadi hapo tutakwenda sawa na mtu yeyote awe uhuru kuitumia kwa ustaarabu na adabu ipasavyo simu hii na si vinginevyo. Kama hilo limeeleweka, sasa tuzungumze kuhusu mada yetu ya leo. Limekuwa jambo la kawaida kwa wasanii wetu maarufu kuzushiwa vifo pindi wanapopatwa na madhila ya hapa na pale, hususan ugonjwa. Mara kadhaa tumeshuhudia jambo hilo, ambapo kwa kweli kila linapotokea huleta fadhaa, mshituko na taharuki kubwa kwa mashabiki, wapenzi pamoja na wadau mbalimbali. Katika hili sina haja ya kutoa msururu wa mifano juu ya hilo, kwani sote wenye macho na masikio ni mashahidi wazuri, kwani ni jambo ambalo limekuwa likiizunguka jamii muda wote. Binafsi nimelazimika kusema hili kutokana na mshtuko nilioupata siku ya Jumapili. Ilikuwa hivi, nikiwa Gongo la Mboto - Majohe, ambako nilikwenda katika kisomo cha hakika ya mtoto wa kaka yetu, Shaaban Msonga, aliyekuwa akitoka siku 40 baada ya kuzaliwa, katikati ya kisomo simu yangu ikaanza kutikisika (vibration), nikaitazama na kuona jina la anayenipigia. Alikuwa Dina Ismail, ambaye ni mtu wangu wa karibu sana, hivyo nikajua anataka kunijulia hali kwa kuwa ni kawaida yetu kusalimia kila ifikapo asubuhi. Mara baada ya kupeana salamu akaniliuliza kama nina habari yoyote ya kumpa, nikamwambia sina. Yeye akaniambia kama hauna acha mimi nikupe. Akasema: "Mzee Yusuf hatunaye duniani." Ghafla nikang'aka na kama ilivyo kawaida mtu ukiambiwa habari za kifo mara zote huwa tunakataa, hivyo nikamwambia ahakikishe habari hizo kwa watu wa karibu sana na Mfalme, tena nikimsisitiza ampigie Said Mdoe ‘Screen Masters' na kumwomba anipashe lolote litakalojiri. Baada ya kukata simu watu niliokuwa nao shughulini hapo ambao wote tulikuwa wana ndugu wakaniuliza: "Vipi bibie, kulikoni mbona umebadilika?" Nikawaambia kuhusu habari iliyonichanganya, lakini hapohapo na mimi nikapata wazo la kumpigia Mdoe Screen Masters, lakini jambo la kushangaza alipopokea simu yangu akapokea na kicheko huku akiniambia, "Pole sana Khadija, Mzee Yusuf hajafa wanazusha tu, hii simu yako ni ya 20 kupokea, Mzee Yusuf yupo Zanzibar kwa mapumziko, mara baada ya kufanyiwa upasuaji kama ilivyokuwa awali." Msomaji wangu, binafsi nilikereka nikatamani kumpata mtu wa kwanza aliyevumisha taarifa za kifo hicho, hivyo nikaagana na Mdoe na kukata simu, baada ya hapo nikapokea tena simu kutoka kwa Dina, akanambia maneno kama aliyoniambia Mdoe, kwa sababu na yeye alizungumza naye. Jambo hilo la kuzushiwa kifo kwa Mzee Yusuf limekuja mara baada ya msanii huyo kusimama kazi kutokana na ugonjwa wa mguu, ambapo amefanyiwa upasuaji na kuuguza kidonda. Ninachoshangaa mimi, hivi wasanii hawatakiwi kuumwa kama watu wengine? Au wanapoumwa na kuzushiwa kufa sisi jamii tunapata nini? Naomba tubadilike, si kwamba hawatakufa, watakufa lakini ni kwa ahadi yake Rabana na si kwa matakwa yetu sisi viumbe tusiokuwa na utimilifu hata chembe. Takriban siku 28 tu tangu mwaka mpya wa 2011 uanze, tayari kadhia hiyo imeshawakumba wasanii wetu wawili wakubwa katika fani za muziki wa dansi pamoja na mipasho. Nao si wengine bali ni mwimbaji mkongwe wa bendi ya Msondo Ngoma Music, Muhidin Maalim Gurumo na hivi karibuni Mfalme wa mipasho kutoka kundi la Jahazi Modern Taarab Mzee Yussuf Mwinyi. Ingawa ni kweli kuwa wote wawili Gurumo na Yussuf wako kitandani, lakini bado si halali kwao kuzushiwa vifo, hasa ikizingatiwa kuwa hali zao zinaendelea vizuri. Yussuf aliyefanyiwa upasuaji wa goti la mguu wake wa kushoto Januari 11 na habari hiyo ilichapishwa katika gazeti la Tanzania Daima ikiwa na kichwa cha habari: ‘Mzee Yussuf apigwa kisu', yuko mapumzikoni, nyumbani kwao Michenzani Zanzibar akiendelea kupata nafuu siku hadi siku. Kwa upande wa Gurumo anayesumbuliwa na ugonjwa wa figo ameshatoka hospitali siku nyingi baada ya kuonekana anaendelea vizuri na sasa anajiuguza nyumbani kwake Tabata jijini Dar es Salaam. Lakini mbali ya kuwa taarifa za kuendelea vyema kwa hali zao zimekuwa zikiwekwa bayana, bado wazushi wamekuwa wakiwaandama nguli hao mara kwa mara kuwa eti wamekufa. Hivi ni nani anayefanya makusudi haya ya mara kwa mara kuzusha vifo kwa wasanii na wanamuziki wetu hapa nchini na nini lengo lake hasa? Ina maana hafahamu kuwa uvumi huo usio na maana yoyote unawaathiri vilivyo wahusika, familia zao pamoja na watu wao wa karibu kama vile mashabiki pamoja na wapenzi? Je, anafaidika nini kila pale anapozusha na kuvumisha taarifa zisizo za kweli kama hizo ambazo zinapowafikia walengwa ambao ni mashabiki, hupatwa na simanzi? Ama tuseme hii ndiyo fadhila pekee wanayoona wanastahili kulipwa wasanii na wanamuziki wetu kwa mchango wao mkubwa wa kuielimisha pamoja na kuiburudisha jamii? Je, hali hii ya wapendwa wetu hawa wasanii pamoja na wanamuziki kuzushiwa vifo kila pale wanapougua kidogo ama kupata ajali itakoma lini na kivipi? Kwa sababu, wao si wa kulipwa madhila ya uzushi wa namna hiyo, kwa vile ni watu muhimu sana katika jamii yetu ambao hutusaidia katika ujenzi wa maadili. Kwa kuwa uzushi ni mbaya, hasa kama huu wa kifo, ambapo hata nilipozungumza nao wenyewe Gurumo na Yussuf walionyesha kufadhaika. "Awali sikuwa nafahamu kwamba tunaowaimbia na wao kuja kututunza, miongoni mwao ni nyoka na mashetani wasiotutakia mema," anasema kwa uchungu Gurumo. Aidha, kwa upande wa Yussuf, mwingi wa mizaha na ucheshi, anasema binafsi anawataka wanaomzushia kifo waanze kumkusanyia michango. "Si wanasema nimekufa, basi na waanze kunikusanyia michango, tena siku hizi kuna M-pesa na Tigo Pesa, mambo pooa kabisa," anasema Yussuf. Hata hivyo, pamoja na kuwa wasanii wetu hujikaza na kuzungumza kiungwana kila pale wanapozushiwa namna hii, bado ukweli wa kuwa wanaumia utabaki pale pale kwani nao wana roho na mioyo iliyoumbwa kwa nyama laini si vyuma. Hii ni kwa sababu, wao ni watu wazima wenye mawazo timilifu kama sisi, ambapo bila shaka hulinganisha mchango wao kwa jamii na fadhila wanazolipwa hatimaye. Hakuna asiyefahamu jinsi wasanii pamoja na wanamuziki wetu wanavyobeba jukumu zito la kufundisha, kuhimiza, kutia moyo, kufariji na kutoa burudani kwa watu wa rika zote. Wanapoteza muda wao mwingi kwa kukuna vichwa na kutumia akili na maarifa kutupakulia kazi ambazo hugeuka liwazo kwetu kila tunaposawajika kimawazo. Sidhani kama atajitokeza wa kunibishia nitakaposema kuwa tunazitegemea nyimbo pamoja na filamu zao kututia nguvu kila pale tunapotawaliwa na uchovu wa mawazo. Nafikiri, umefika wakati sasa wa sisi wote kuangalia namna ya kuwa waungwana na wastaarabu kwa kuzizuia ndimi zetu zinapojisikia kuropoka yasiyostahili. Pia wahenga walisema, ulimi ni kiungo kidogo lakini matatizo yake ni makubwa.
Dedebit wapania kuiduwaza Yanga • Kocha ajivunia ‘mapro' Waghana, nyota wa taifa na Dina Ismail
WAKATI kesho Yanga inashuka katika dimba la Taifa kuanza kampeni yake katika Kombe la Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), wapinzani wao Dedebit ya Ethiopia wamewasili alfajiri ya jana huku wakiwa na imani kubwa ya kuwaduwaza wenyeji wao. Timu hiyo imetua na msafara wa watu 30, wakiwemo wachezaji 18 na viongozi 12 na kufikia hoteli ya Durban Mnazi Moja jijini Dar es Salaam. Wachezaji hao ni Behalu Assefa, Dawit Fekadu, Getaneh Kabede, Danile Debra, Mengstu Assefa, Mickle Sisay, Efram Zero, Grume Syeyome, Mulget Merte, Wendsone, Tadle Menasha na Temsgen Tekele. Wengine ni Jebrale, Adrnu, Benyme Habtmu, Semer Yemna, Beruno Bogle na Mesfine. Kocha wa Wahabeshi hao, Gembremed Haile, ametamba kupata matokeo mazuri kwenye mechi hiyo, licha ya timu yake kuwa mpya na mara yake ya kwanza kushiriki CAF. Alijinasibu kuwa kikosi chake kina nyota watano wa timu ya Taifa na wanne wa kulipwa, wakiwapo Waghana wawili, kiungo na beki wa kati. Alisema, anajivunia nyota hao, ingawaje anaiheshimu sana Yanga, kwani anaijua tangu miaka 20 iliyopita. Alisema, timu yake ni mara yake ya kwanza kufika Afrika Mashariki, hivyo amejipanga vema kuhakikisha anafanya vizuri, licha ya Yanga watakuwa na faida ya kuchezea uwanja wa nyumbani. Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema yamekamilika ambapo timu yao iko katika hali nzuri chini ya kocha msaidizi Fred Felix Minziro isipokuwa Shamte Ali anayeendelea na matibabu, pamoja na Ernest Boakye anayesumbuliwa na maumivu ya nyama za paja. "Pamoja na yote, tumejiandaa ipasavyo na mechi hiyo na lengo letu kubwa ni kuhakikisha tunashinda mechi hiyo ili kujiweka katika mazingira mazuri, tunaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi ili kuwashangilia wachezaji wetu na kuwatia nguvu," alisema. "Pamoja na yote, tumejiandaa ipasavyo na mechi hiyo na lengo letu kubwa ni kuhakikisha tunashinda mechi hiyo ili kujiweka katika mazingira mazuri, tunaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi ili kuwashangilia wachezaji wetu na kuwatia nguvu," alisema. Katika hatua nyingine, aliyekuwa kocha Mkuu wa Yanga, Mserbia Kostadin Papic, jana aliwasilisha rasmi barua ya kujiuzuru. Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga, alithibisha kupokea barua hiyo na kusema kuwa Papic hajaweka wazi sababu zilizomfanya ajitoe kuifundisha timu hiyo, kabla ya mkataba wake kumalizika. Nchunga alisema, baada ya kuipokea anatarajia kumuandikia barua kocha huyo ya kutaka kuelezea baadhi ya mambo kabla hajaondoka nchini. "Papic ameshawasilisha barua kwa uongozi... tutaisoma kabla ya kumuandikia na sisi ya kwetu ya kutaka atueleze baadhi ya vitu, kabla hajaachana na sisi, kwani tunataka tuachane kwa usalama," alisema Nchunga. Mapema wiki hii, Papic alitangaza kujitoa kuifundisha timu hiyo, akidai kupuuzwa kuhusiana na ujio wa Minziro ambao alikuwa akiupinga.
WAZEE wa klabu ya Yanga wameibuka na kutaka viongozi wao wote waliojitoa madarakani kurejea kwenye nafasi zao akiwemo aliyekuwa Meneja Emmanuel Mpangala na kocha wao Kostadin Papic kabla ya mechi na Dedebit huku wakimuonya Mwenyekiti wao Lloyd Nchunga. Katibu Mkuu wa Wazee hao, Ibrahim Akilimali, alisema jijini Dar es Salaam kuwa wanataka viongozi hao warejee ili kuongeza nguvu katika timu yao inayokabiliwa na mashindano ya kimataifa. Akilimali alisema, baada ya mechi hiyo wamepanga kukutana na wadhamini wao Yussuf Manji, Mama Fatuma Karume na Francis Kifukwe kuzungumzia mzozo unaoendelea Yanga ili kufikia muafaka. Aidha Akilimali alimtaka Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga, kuwa makini na utawala wake, kwani wao wanaijua Yanga kuliko yeye.
WAWAKILISHI wa Tanzania katika ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ya jijini Da res Salaam wamesema mechi yao ya awali dhidi ya Elan de Mitsoudje ya Comoro itakayopigwa kesho ugenini itakuwa ngumu. Akizungumza kwa simu kutoka Comoro jana, Meneja wa Simba, Innocent Njovu alisema kwamba ugumu wa mechi hiyo unatokana na wapinzani wao kuwa na wachezaji mahiri na wenye uwezo wa hali ya juu. Alisema, umahiri wa timu hiyo unatokana na kuwa na wachezaji sita wanaoichezea timu ya Taifa ya Comoro, huku pia wengine watatu wakiwahi kucheza soka la kulipwa nchini Ufaransa. Hata hivyo, Njovu alisema kuwa, wamejiandaa kikamilifu kuhakikisha wanashinda mechi hiyo ili kujiwekea mazingira mazuri katika mechi yao ya marudiano. "Tunafahamu wapinzani wetu ni wazuri hali inayobashiri mechi kuwa ngumu, kwani hata sisi tumekiandaa vema kikosi chetu na wachezaji wana ari ya ushindi," alisema Njovu. Aidha, Njovu aliongeza kuwa jana timu ilifanya mazoezi asubuhi na jioni wachezaji walipata mapumziko tayari kwa mechi hiyo itakayopigwa keshokutwa. Akizungumzia mechi hiyo, kiungo wa timu hiyo, Rashid Gumbo alisema Watanzania wawaombee dua tu ili waibuke na ushindi mnono.
WAPINZANI wa timu ya Yanga, Dedebit FC kutoka Ethiopia, iliwasili jana alfajiri ikiwa na wachezaji watano wa kulipwa tayari kwa mechi ya
michuano ya CAF, itakayopigwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Timu hiyo imewasili na wachezaji 18 na viongozi 12 ambapo kati ya wachezaji hao, watano wanacheza soka la kulipwa.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema tiketi za mchezo huo zitaanza kuuzwa leo kuanzia saa nne asubuhi katika vituo saba jijini.
Alivitaja vituo hivyo kuwa ni Big Born, Ubungo, Tandika sokoni, Buguruni, Ohio na Uwanja wa Taifa ambaye aliwaomba mashabiki kununua tiketi mapema, ili kuondokana na usumbufu unaojitokeza mara kwa mara.
Mbali na hilo, Sendeu aliongeza kwamba kiungo wao, Ernest Boakye yupo hatihati kucheza mchezo huo kutokana na kuwa majeruhi.
Aliwataja wachezaji wa Dedebit ambao wamekuja nchini ni Behailu Assefa, Dawit Fekapu, Getaneh Kebede, Danile Derba, Mengstu Assefa, Mickle Sisay, Efrah Zero, Grume Syeyome, Mulget Merte na Wendeson.
Wengine ni Tadle Menasha, Temsger Tekele, Jebrale, Adanu, Beniyme Habtmu, Semer Yemna, Beruno Bogle na Mesfine.
Phiri: Ushindi kesho lazima Thursday, 27 January 2011 21:11
Kocha wa Simba, Patrick Phiri
Andrew Kingamkono, Comoro
KOCHA wa Simba, Patrick Phiri amewaondoa hofu mashabiki wake akiahidi kufanya vizuri kwenye mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika hapo kesho dhidi ya mabingwa wa Comoro, Elan.
Akizungumza na Mwananchi kwenye Hoteli ya Karthala nje kidogo ya jiji la Moroni, Phiri alisema: "Najua wapinzani wetu ni timu bora kwakuwa ni mabingwa wa hapa, lakini ushindi ni lazima.
"Nafahamu Elan ina wachezaji sita wa timu ya taifa ya Comoro, niliwaona ilipocheza na Zambia japo walifungwa 4-2, lakini walicheza vizuri. Natarajia kupata ushindi mkubwa licha ya kuwa wao watakuwa nyumbani mbele ya mashabiki wao."
Aliongeza Phiri kusema: "Kutokana na ubora wao, nimewaanda vema wachezaji wangu na kuwataka wasahau yaliyotokea dhidi ya Azam na kujipanga kwa mchezo huu.
Akifafanua juu ya matokeo ya Azam, Mzambia huyo alisema "Siwezi kutumia matokeo yale kama kipimo kwa Simba kwenye mchezo huu wa Afrika," alisema Phiri na kuongeza kuwa " wachezaji wake wengi walikuwa kwenye Taifa Stars na wengine ni majeruhi hivyo kulikuwa na kutoelewa kwa aina fulani uwanjani.
Phiri alisema kuwa kama watakishinda mchezo wao wa kesho, watakuwa kwenye wakati mzuri wa kurudisha hali yetu na kuwafanya mashabiki wasahau yaliyopita."
Kipa huyo wa zamani wa Zambia aliweka bayana malengo yake mwaka huu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ni kuhakikisha anafuzu kwa hatua ya makundi lakini ni lazima waishinde kesho.
Tunahitaji kucheza kwa moyo na kujituma zaidi ili kuhakikisha tunashinda hapa na kusonga mbele wote tunajua kwamba kikwazo chetu cha kwanza ni Elan na tunapaswa kusahau yaliyopita."
Mapema kocha wa Elan, Profesa wa Chuo Kikuu cha Comoro, Ahamada Bachirou 'Dakota' akizunguma na Mwananchi kwenye ofisi za Shirikisho la Soka la Comoro, CFF, alisema anajua ubora wa Simba na uzoefu waliokuwa nao kwenye mashindano haya, lakini ameahidi zawadi ya ushindi kwa Wakomoro.
"Nimetazama Simba kwenye video, Internet ni wazuri kwenye kushambulia na kulinda goli, lakini na sisi hatutokaa nyuma tutashambulia ili tuhakikishe tunapa ushindi mkubwa hapa kabla ya Dar es Salaam.
Kuhusu suala la kumkabili Mussa Hassan Mgosi ambaye alikuwa ametawala kwenye midomo ya wanahabari wa hapa kiasi wengine kumfananisha na Lionel Messi wa Barcelona, Dakota alisema anajua Mgosi ni mfungaji mzuri, lakini tayari amemwandaa kipa bora wa kuzuia.
"Sina shida sana na huyo ila nitaongeza nguvu kwenye mashambulizi ni wachezaji sita wenye uzoefu mkubwa wa mechi za kimataifa. Jambo zuri ni kuwa tunacheza nyumbani hivyo nahitaji kupata matokeo mazuri hapa, kwa kuhakikisha tunalinda goli na kufanya mashambulizi."
Phiri alipoulizwa kuhusu kukamiwa huko kwa Mgosi alisema, " Sina tatizo kwa sababu Simba ni timu inayocheza kitimu zaidi hivyo tunaweza kufunga kupitia viungo wetu.
"Mgosi pekee hawezi kuwa bora kama hakuna ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wenzake anahitaji kushirikiana na wengine ili aweze kufunga na kuwa bora.
Mgosi mwenyewe anasema ni vizuri kusikia hivyo kwa sababu wamewasaidi kazi anachokihitaji ni kushirikiana vya kutosha nawenzake ili waweza kufunga.
MAPOKEZI
Makamu mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange 'Kaburu' anasema amefurahishwa na mapokezi mazuri waliopewa na wenyeji pamoja na CFF kuanzia uwanja wa ndege hadi hotelini.
"Sikutegemea kupata mapokezi ya aina hii na kukaa kwenye hoteli ya hadhi na zuri kama hapa Karthala kutoka na uzoefu wangu na nchini hii.
Tatizo pekee ninaloliana ni kuwa uwanja upo mbali kidogo zaidi ya kilomita 40, kutoka hapa hotelini tunatumia saa 3 njia kwenda na kurudi.
"Kutokana na hali hiyo ratiba ya mazoezi imeharibika timu imekosa vipindi viwili vya mazoezi juzi jioni kutokana na mvua na umbali, pia leo (jana) tumefanya mazoezi asubuhi tu, na kesho (leo) tutafanya jioni pekee kabla ya mechi Jumamosi."
Aliongeza Kaburu kuwa Uwanja wao ni mzuri na unatumia nyasi bandia kama wa Uhuru kwahiyo hakuna tatizo.
"Hapa kama tumekuja kufanya mazoezi ndio maana tumekuja na wachezaji wote isipokuwa wale majeruhi, baada ya mechi hii kutakuwa na mchezo wa Ligi Alhamisi dhidi ya African Lyon.
Simba inataraji kuondoka hapa Comoro Jumatatu kwa ndege ya Air Comoro na kuwasili Dar es Salaam saa 8 mchana.
Yanga wamwangukia Papic Thursday, 27 January 2011 21:03
Waandishi Wetu
UONGOZI wa Yanga ukiongozwa na mfadhili wa klabu hiyo, Yusuf Manji umeanza mazungumzo ya kumshawishi kocha wa timu hiyo aliyetangaza kujiuzulu, Kostadin Papic aendelee kuinoa timu yao.
Papic alitangaza kutema kibarua chake Yanga, na juzi alifika katika mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Uhuru na kuwaaga wachezaji wa timu hiyo ambayo kwa sasa inanolewa na Fred Felix Minziro. Papic pia alimkabidhi Minziro mwongozo wa mazoezi.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinazema kuwa Papic na Manji wamekutana mara kadhaa juzi na jana kwa ajili ya kupata suluhu ya suala hilo. Kocha huyo anamaliza mkataba wake baadaye Julai.
Kiliendelea kusema chanzo hicho kuwa vikao hivyo kati ya Manji na Papic ndivyo vilivyosababisha kocha huyo mpaka jana ashindwe kuwasilisha barua rasmi ya kujiuzulu kwake.
"Huyu jamaa (Papic) amekuwa akishawishiwa na Manji abadili msimamo wake na ndio maana unaona hadi sasa hajawasilisha barua rasmi ya kujizuluzu.Kwa jinsi ninavyoona mimi kuna uwezekano mkubwa Papic akabadilisha uamuzu wake," kilieleza chanzo hicho.
Mwananchi lilipomsaka Papic ili azungumzie suala hilo kwanza alikiri kutowasilisha barua mpaka wakati huo na kusema kuwa :"Ni kweli nimekutana na Manji anataka nibadili uamuzi wangu lakini ni vigumu kubadili uamuzi wangu.
"Lakini kikubwa kilichonifanya nifikie hayo, ni uongozi kutonisikiliza kile ninachodhani kinafaa kwa maendeleo ya klabu pamoja na timu," alisema.
Awali, Papic alisema kuwa viongozi wamekuwa wakimuingilia katika kazi yake pamoja na kutotekeleza mahitaji muhimu kwa wachezaji ikiwa ni pamoja na kutowalipa fedha zao za posho na mshahara kwa wakati.
"Nimefikia uamuzi wa kuondoka Yanga baada ya uongozi wa klabu hiyo kuwa na misimamo yao isiyokuwa na msingi huku wakinipuuza na hawanishirikishi katika maamuzi yanayohusu timu.
"Nilimpendekeza Salvatory Edward awe msaidizi wangu lakini cha kushangaza nikaletewa Minziro, na kitendo cha kuondolewa kwa Meneja Emmanuel Mpangala sikukubaliana nacho kwa kuwa ni mtu niliyefanya nae kazi vizuri na sielewi kwa nini uongozi umemuondoa.
"Vitu vingi vimekuwa vinafanyika mimi navumilia, mtu anakwambia anamleta kocha Mjerumani na hakwambii cha zaidi, sasa wewe hapo unafikiri ni nini, si kwamba hakuhitaji, bora niondoke, kwanza nimepata ofa ya timu mbali mbali, Saudi Arabia, Ghana na Afrika Kusini," alisema Papic kwa nyakati tofauti juzi.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga alikaririwa juzi akisema: "Tumembembeleza sana asitishe uamuzi wake lakini amekuwa mgumu hatuna jinsi, tunasubiri atupe barua rasmi tuanze mchakato wa kutafuta kocha mwingine.
"Tunamshangaa Papic anavyosema hajashirikishwa hakuna kitu ambacho tumefanya bila kumshirikisha kama 'issue' ya Salvatory alimpendekeza kweli lakini hajakidhi vigezo vya TFF kwa kuwa hana cheti hata kimoja, na tulimwambia Papic yeye akawa anang'ang'ania lazima msaidizi wake asiwe amefundisha Ligi Kuu, lakini wenye maamuzi ya mwisho ya kuajiri ni sisi, tumeajiri hakuna mwenye haki ya kukataa," alisema.
Katika hatua nyingine, Nchunga alisema msimamo wa klabu yake kumwajiri Minziro kuwa kocha msadizi umezingatia uzalendo zaidi.
"Ni lazima ifikie wakati tutambue heshima ya makocha wetu wazawa, kimsingi hakukuwa na sababu za msingi za Papic kupinga Minziro asiajiriwe.
"Nani asiyemjua Minziro ni mtu mwenye heshima zake, kwanza ana uzoefu wa kufundisha timu za jeshi, nafikiri kila mtu an ajua utaratibu wa jeshini ulivyo mkubwa akiongea mdogo lazima afuate sasa hapo wangeshindwana vipi?," alisema Nchunga.
Updated Jan 28, 2011 9:24 AM ET Carlo Ancelotti has refused to be drawn on Chelsea's failed £35million bid for Fernando Torres but is happy the club are looking to strengthen.
On Friday morning, Liverpool confirmed they have rejected a bid - believed to be in the region of £35million - from the Blues for their star striker. But Ancelotti said: "I don't want to speak about this, you will have to ask the club. He is not my player and I have to have respect for Liverpool. I don't like to speak about this." Liverpool, though, have warned their rivals that Torres is simply not available. "Chelsea have made a bid for Fernando which has been turned down," a Liverpool spokesman said. "The player is not for sale." Chelsea owner Roman Abramovich is a long-time admirer of the Spain international but has been unsuccessful in past attempts to lure the player away from Anfield and looks set to fail again. There has been much speculation about Torres' future but it began to grow after the club finished seventh in the Premier League last season. He returned to Merseyside as a World Cup winner and, with Chelsea seemingly prepared to make a bid, he insisted his commitment to the Reds was the same as when he signed in the summer of 2007. However, his - and the club's - early-season form did little to dispel those rumours as the striker cut a frustrated and agitated figure on the pitch as Liverpool endured their worst start to a campaign since 1953/54. Matters were not helped when it emerged a £50million buy-out clause had been inserted into his contract - which runs until 2013. But since the appointment of Kenny Dalglish to replace Roy Hodgson nearly three weeks ago Torres has looked a rejuvenated player and in his last four matches has scored three times - which would have been four had he not had an effort against Fulham on Wednesday wrongly ruled out for offside. Owners Fenway Sports Group, who took over the club in October, are keen to invest in the squad to ensure the likes of Torres can satisfy their desire for success with Liverpool. To that end they are still trying to negotiate a deal with Ajax for Uruguay forward Luis Suarez. The Dutch club's coach Frank de Boer has set a Saturday deadline for an agreement to be reached but with the asking price still a sticking point it could yet go right up to the close of the window on Monday. Suarez is keen on a move to Liverpool and reports in Holland claim he feels "cheated" Ajax have not reached a compromise.
JamiiForums uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.