Mgosi aipeleka Simba kileleni
Sunday, 06 February 2011 21:30
Oliver Albert
MSHAMBULIAJI Mussa Hassan Mgosi aliiongoza Simba kurudi kileleni mwa ligi kwa kufunga mabao mawili na kuiwezesha timu yake kushinda 2-0 dhidi ya wachezaji 10 wa Polisi Tanzania, huku kipa Juma Kaseja akiwa golini kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Mgosi alifunga bao la kwanza katika ya dakika 53, kipindi cha pili kwa mpira wa adhabu wa umbali wa mita 35, baada ya Mbwana Samata kuangushwa.Mgosi alipiga faulo hiyo na mpira ulikwenda moja kwa moja wavuni na kumwacha kipa Said Kombo asijue la kufanya.
Awali katika dakika ya 44, pia Mgosi alifunga bao kwa mpira wa adhabu aliopiga nje ya eneo la 18 baada ya kuangushwa kwa Nyagawa, lakini mwamuzi Alex Mahagi kutoka Mwanza alilikataa kwa kusema mfungaji alishindwa kufuata kanuni za upigaji wa mpira huo ambao ulitakiwa uguswe na watu wawili kwanza jambo ambalo Mgosi hakufanya na timu hizo kwenda mapumziko kwa suluhu.
Katika kipindi cha pili mshambuliaji Mussa Mgosi alifunga bao la pili katika dakika ya 84, akiunganisha vizuri kwa kichwa krosi ya Haruna Shamte kutoka upande wa kulia na kufikisha mabao sita katika msimu huu.
Kwa matokeo hayo Simba imerudi kileleni baada ya kufikisha pointi 33 ikiwa na pointi moja zaidi ya Yanga iliyo na michezo zaidi ikiwa nafasi ya pili na pointi 32.
Polisi walipata pigo katika dakika ya 63, baada ya mshambuliaji wao Semsue Juma kutolewa nje kwa kadi mbili za njano baada ya kuwachezea vibaya Amir Maftah na Kaseja katika wakati tofauti.
Katika mechi hiyo mshanbuliaji wa Simba,Mbwana Samata alipoteza nafasi za kufunga kwa kushindwa kuunganisha mpira wa kona dakika ya 60 na 71 akiwa yeye na kipa.
Baada ya kukaa benchi mechi mbili mfululizo kipa Kaseja jana alipewa nafasi ya kujirekebisha mbele ya kocha wake Mzambia Patrick Phiri.
Mchezo huo ulianza taratibu huku timu zote zikijaribu kuangalia mapungufu ya mwenzake, lakini Simba walionekana kupwaya zaidi kwenye kiungo ikiwa na Jerry Santo, Ochan Patrick na mkongwe Nico Nyagawa.
Udhaifu huo wa kiungo wa mabingwa hao ulitoa nafasi kwa wenyeji Polisi TZ kujipanga na kufanya mashambulizi katika kipindi hicho cha mwanzo mbele ya mashabiki wao.
Kasi hiyo ya mashambulizi ilimfanya kipa Kaseja kufanya kazi ya ziada katika dakika ya 17, ambapo alipangua vizuri shuti la Ally Khalid lililomfanya aumie mkono baada ya kujigonga kwenye mwamba na mpira kusimama kidogo ili apewe matibabu.
Awali mshambuliaji chipukizi Mbwana Samata alipiga shuti la mbali dakika 14 na kutoka nje kabla ya Ochan kupoteza nafasi ya wazi akiwa yeye na kipa Said Kombo kwenye dakika ya 18.
Katika mchezo huo Simba ilimpumzisha Nyagawa na kumuingiza Shija Mkina wakati Polisi wao walimtoa Deltha Thomas na kumwingiza Bantu Admin.
VIKOSI
Polisi Tanzania:
Said Kombo, Nahoja Haji, Elias Mafutaa, Noel Msakwa, Salmin Kiss, Ismail Nkulo, Sihaba Mkude, Khalid Ally, Semsue Juma, Seif Mohamed na Deltha Thomas.
Simba
Juma Kaseja, Haruna Shamte, Amir Maftah, Juma Nyoso, Kelvin Yondani, Jerry Santo, Nico Nyagawa, Patrick Ochan, Mussa Mgosi, Mbwana Samata na Amri Kiemba.